Wambui mbioni kurejea Simba
Muktasari:
- Wambui, raia wa Kenya, alipata jeraha baya la goti wakati timu hiyo ilipokuwa nchini Kenya ikishiriki michezo ya maandalizi ya Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake michuano ambayo Simba Queens iliishia hatua ya makundi.
KOCHA Mkuu wa Simba Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’ amesema winga wa timu hiyo, Elizabeth Wambui anaendelea kuimarika na wanatarajia atarudi uwanjani baada ya mechi za mzunguko wa pili wa Ligi ya Wanawake unaotarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu.
Wambui, raia wa Kenya, alipata jeraha baya la goti wakati timu hiyo ilipokuwa nchini Kenya ikishiriki michezo ya maandalizi ya Mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake michuano ambayo Simba Queens iliishia hatua ya makundi.
Akizungumzia hali ya mchezaji huyo, Mgosi amesema benchi la madaktari lilimpa Wambui wiki nne za mapumziko na uangalizi maalum, na mpaka sasa tayari zimetimia wiki mbili tangu anze mpango huo wa matibabu.
“Ni kweli mwanajeshi wetu Wambui alikuwa anaumwa ila kwa sasa anaendelea vizuri. Tunategemea hadi ligi itakapoanza mwishoni mwa mwezi huu atakuwa fiti. Hata hivyo, kwa mujibu wa daktari, atakosa mechi mbili za mwanzo za mzunguko wa pili kabla ya kuanza kucheza rasmi,” amesema Mgosi.
Winga huyo mwenye kasi urejeo wake unategemewa kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Simba ambayo imetoka kubeba taji la Ngao ya Jamii kwa wanawake juzi Oktoba 03 ikiwapoka JKT Queens.
Kikosi hicho chini ya Mgosi kinaamini kina nafasi ya kufanya vizuri msimu huu na kutetea taji ambalo inalishikilia na kurejea kwenye michuano ya kimataifa ambayo imekuwa ikishiriki mara tatu.