Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ngao ya Jamii Ilivyotoa taswira ya WPL 2026/27

AFC 0

Muktasari:

  • Mbali na Simba Queens kuibuka na ndoo hiyo baada ya kuichapa JKT Queens bao 1-0 lililofungwa na Aisha Mnunka na Yanga Princess kumaliza mshindi wa tatu, kitendo cha timu hizo kushuka dimbani kimetupa taswira kamili na picha halisi ya jinsi msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) utakavyokuwa na moto ushindani mkubwa.

KIPIMO cha kwanza cha utimamu wa miamba ya soka la wanawake nchini kimetamatika rasmi baada ya kufungwa kwa pazia la Mashindano ya Ngao ya Jamii (Wanawake).

Mbali na Simba Queens kuibuka na ndoo hiyo baada ya kuichapa JKT Queens bao 1-0 lililofungwa na Aisha Mnunka na Yanga Princess kumaliza mshindi wa tatu, kitendo cha timu hizo kushuka dimbani kimetupa taswira kamili na picha halisi ya jinsi msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) utakavyokuwa na moto ushindani mkubwa.

Kwa kutazama michezo iliyopigwa, kuna mambo makuu manne ambayo yatakuwa msingi wa ushindani na mwelekeo wa soka la wanawake kwa msimu mzima wa 2026/2027:


NGA 01

USHINDANI WA NNE BORA

Kama kuna jambo ambalo Ngao ya Jamii imelithibitisha bila kuacha shaka, ni kwamba pengo la ubora kati ya timu za juu linazidi kupungua siku hadi siku. Vita ya kusaka nafasi nne za juu kwenye msimamo wa ligi msimu huu haitakuwa ya kitoto hata kidogo.

Miamba minne iliyoshiriki mashindano haya Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess na Mashujaa Queens imeonyesha wazi kwanini ndiyo inayoshikilia usukani wa soka la wanawake kwa sasa.

Mchezo wa mshindi wa tatu kati ya Yanga Princess na Mashujaa Queens pekee ulikuwa mfano tosha wa jinsi timu za kawaida zinavyoweza kuzipa presha kubwa klabu kongwe.

Mashujaa Queens imeonyesha nidhamu ya hali ya juu ya kiufundi, ikiwa na wachezaji wenye uwezo wa kupambana mwanzo mwisho bila uwoga. Hii ni ishara tosha msimu huu hautakuwa wa timu mbili au tatu pekee.


NGA 02

SIMBA QUEENS MUENDELEZO

Ushindi wa bao 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi JKT Queens kwenye mchezo wa fainali umetoa ujumbe mzito, Simba Queens imerudi ikiwa imekamilika kila idara na ina nia ya kutawala soka la wanawake msimu huu.

Kiwango walichokionyesha Msimbazi tangu mchezo wa nusu fainali walipoichapa Yanga Princess mabao 3-0, hadi fainali na waliwavua ubingwa JKT Queens, kinathibitisha kuwa kocha Mussa Hassan ‘Mgosi’ na benchi lake la ufundi wamefanya kazi kubwa wakati wa maandalizi ya msimu (pre-season).

Simba inaonyesha utulivu mkubwa wa kiufundi, safu ya ulinzi ikiwa na ubora mkubwa na mashambulizi ya kushtukiza yenye madhara makubwa kupitia kwa wachezaji wao wenye kasi kama Aisha Mnunka na Mary Siyame.

Ubingwa huu wa Ngao ya Jamii sio tu unawapa nguvu ya kisaikolojia, bali unawapa ya kuwa timu inayowaniwa zaidi na kila mpinzani pindi Ligi Kuu itakapoanza rasmi.


NGA 03

YANGA PRINCESS BADO KUNA KAZI

Kwa upande wa Yanga Princess, ingawa wamefanikiwa kuondoka na nafasi ya tatu kwa kuifunga Mashujaa Queens kwa mikwaju ya penati, mechi za Ngao ya Jamii zimeanika wazi changamoto kubwa inayowakabili hivi sasa ukosefu wa muunganiko na uelewana wa kitimu.

Asilimia kubwa ya kikosi cha Yanga Princess msimu huu inaundwa na wachezaji wapya kabisa, wengi wao wakiwa wamesajiliwa kutoka nje ya nchi.

Ingawa mmoja mmoja wana uwezo mkubwa na viwango vya juu, bado hawajakaa pamoja muda mrefu wa kutosha kutengeneza mfumo bora na wa kuelewana uwanjani.

 Mtihani huu wa kwanza umeonyesha kuwa timu hiyo itahitaji muda zaidi wa kuzoeana na kujenga muunganiko.

Benchi lao la ufundi lina kazi ya ziada ya kuhakikisha wachezaji wanakaa kwenye mfumo mmoja haraka iwezekanavyo kabla ligi haijachanganya, vinginevyo watapoteza pointi muhimu mapema kwenye mzunguko wa kwanza.


NGA 04

JKT QUEENS IJIPANGE UPYA

JKT Queens, ambayo imekuwa kinara na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu pamoja na Ngao ya Jamii kwa miaka ya hivi karibuni, sasa wamekutana na kigingi kinachowapa picha ya kile kinachowasubiri msimu huu.

 Kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Simba Queens kimeonyesha kuwa wapinzani wao wamesoma mbinu zao na wametafuta dawa ya kuwakabili.

JKT Queens bado ni timu imara yenye wachezaji wenye uzoefu mkubwa wa mechi ngumu, lakini wazi kabisa wanahitaji kujipanga upya na kuongeza mbinu mbadala kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Ushindani wa msimu huu utakuwa mgumu zaidi kuliko msimu uliopita, na kama hawataongeza kasi, watakutana na wakati mgumu kutoka kwa miamba hiyo ya Msimbazi na hata Yanga itakapokaa sawa.

Ngao ya Jamii imetoa picha ya awali na ya kuvutia sana ya Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu. Mashabiki wajiandae kushuhudia msimu wenye msisimko wa aina yake, takwimu mpya na ushindani wa hali ya juu ambapo hakuna timu inayoweza kujihakikishia ushindi kabla ya dakika 90 kumalizika uwanjani.


NGA 05

WASIKIE HAWA

Kocha wa JKT, Kessy Abdallah anasema pamoja na kuondoka mshindi wa pili lakini kuna vitu watakwenda kuboresha kabla ya ligi kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi Oktoba.

“Mashindano yametuonyesha sehemu tunazopaswa kufanyia maboresho hasa eneo letu la mbele tunatengeneza nafasi nyingi lakini hatuzigeuzi kuwa mabao,” anasema Kessy

Kocha wa Simba, Mgosi anakiri licha ya kuwa mabingwa lakini wao kama makocha na benchi lake la ufundi watakwenda kurekebisha baadhi ya maeneo.

“Msimu huu ligi itakuwa ngumu sana kikubwa tutapambana na kuangalia namna gani tunaweza kushinda kila mechi na nizungumze na baadhi ya timu zijipange kwa sababu kila timu inaonekana iko kimkakati.”