Wakenya watikisa KM21, watanzania wang’ara KM10 Yas Zanzibar International Marathon
Muktasari:
- Mbali na ushindani wa kutafuta nafasi za juu, mbio hizo zimeendelea kujijenga kama moja ya matukio muhimu yanayounganisha michezo, afya na utalii. Zanzibar ikitumia fursa hiyo kujitangaza kimataifa kupitia utalii wa michezo.
WANARIADHA mbalimbali wa kimataifa wameonyesha makali yao katika msimu wa sita wa Yas Zanzibar International Marathon 2026, huku ushindani mkubwa ukishuhudiwa katika mbio hizo zilizofanyika mapema leo Septemba 20, 2026 kwenye viwanja vya Maisara, Unguja.
Mashindano hayo yamehusisha mbio za kilometa 21, 10, na 5, yamewakutanisha wanariadha kutoka mataifa mbalimbali huku maelfu ya wakazi wa Zanzibar wakijitokeza kushiriki mbio hizo.
Mbali na ushindani wa kutafuta nafasi za juu, mbio hizo zimeendelea kujijenga kama moja ya matukio muhimu yanayounganisha michezo, afya na utalii. Zanzibar ikitumia fursa hiyo kujitangaza kimataifa kupitia utalii wa michezo.
Mbio za kilometa 21 upande wa wanaume, Wakenya Justus Nyesya, Ransisi Kamito na Simon Kelenzyo, wamemaliza nafasi tatu za juu, huku upande wa Wanawake, Wakenya Valentine Chep na Rahel Miteka wakimaliza nafasi mbili za juu, Mtanzania Failuna Abdi akichomoza nafasi ya tatu.
Kwenye kilometa 10 kwa wanaume, Watanzania Shedrack Damas na Boay Maganga wamemaliza nafasi mbili za juu, Dankan Kipchu wa Kenya akishika nafasi ya tatu.
Wanawake kilometa 10, Mkenya, Faith Jeptum ameongoza mbio hizo huku Watanzania Anna Dolomong akiwa wa pili na Dorcas Boniface akiwa wa tatu.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Juma aliyemuwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amewapongeza waandaaji, wadhamini na wanariadha kwa kuendeleza mbio hizo.
“Michezo ina nafasi kubwa katika kuimarisha afya, kuwakutanisha watu na kuitangaza Zanzibar. Tunapokuwa na mashindano kama haya yanayowaleta pamoja wanariadha kutoka maeneo mbalimbali, tunaitangaza Zanzibar na kufungua fursa katika sekta ya utalii na uchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa michezo katika kutoa mchango wa kukuza utalii.
Kwa upande wake, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura, amesema kukua kwa mbio hizo katika kipindi cha miaka sita ni ishara ya namna Zanzibar inavyoendelea kujenga nafasi yake katika michezo na utalii.
“Kwa miaka sita sasa, Yas Zanzibar International Marathon imekuwa ni zaidi ya mbio, imekuwa sehemu ya kuitangaza Zanzibar, na kuhamasisha uchumi wa buluu,” amesema Rwetabura huku akiwapongeza washiriki wa makundi yote.
Ameongeza kuwa, Yas imeigusa sekta ya Afya kwa kuendesha kambi za huduma za macho bila malipo pamoja na kampeni ya tumaini inayosaidi huduma za afya ya mama na mtoto kwa kutoa vifaa muhimu katika hospitali na vituo vya afya vya serikali.
Msimu wa sita wa Yas Zanzibar International Marathon umehitimishwa kwa wa washindi wa makundi mbalimbali kutunukiwa zawadi huku waandaaji wakieleza dhamira yao ya kuendelea kukuza mashindano hayo na kuvutia washiriki zaidi.