Prime
Wagombea waanza kulia uchaguzi TFF

Muktasari:
- Kilio hicho kimetolewa na mgombea wa urais, Injinia Mustapha Himba akisema mara baada ya kuchukua fomu hiyo, amekumbana na kigingi kigumu kuidhinishwa na wajumbe wa uchaguzi huo.
SAA 24 kabla ya kufungwa kwa zoezi la kuchukua na kurudia fomu za Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), baadhi ya wagombea waliojitosa katika kinyang'anyiro hicho wameanza kulia kwa kutoridhishwa taratibu zilizowekwa za uidhinishaji kupitia wajumbe ili kuruhusu urudishaji fomu.
Kilio hicho kimetolewa na mgombea wa urais, Injinia Mustapha Himba akisema mara baada ya kuchukua fomu hiyo, amekumbana na kigingi kigumu kuidhinishwa na wajumbe wa uchaguzi huo.
Akizungumza na vyombo vya habari mapema leo Alhamisi, Himba alisema mara baada ya kuchukua fomu hizo, amepambana kutafuta wajumbe lakini wameshindwa kumpa ushirikiano akijibiwa tayari uidhinishwaji huo umeshafanyika kwa mmoja wa mgombea mmoja ambaye hata hivyo hakumtaja.
"Kugombea ni haki ya kila anayejiona ana sifa na nilipojipima nikaona natosha na kwenda kuchukua fomu, wote mliona katika huu uchaguzi kuna wagombea wa nafasi ya Rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji," alisema Himba na kuongeza;
"Mimi nilijipima na kutaka kugombea nafasi ya Rais, lakini katika ile fomu kuna eneo linanitaka nipate uidhinishwaji wa angalau wajumbe watano, nimezunguka sana naambiwa watu 46 kati ya 47 walishampa mgombea mmoja.
"Sasa unajiuliza mchakato umeanza juzi tu, leo hii watu 46 waliwezaje kumuidhinisha huyu mtu mmoja tena wengine wakisema mengi zaidi. Tungeambiwa mapema tu kwamba uchaguzi huu una mgombea mmoja tu wa nafasi ya Rais tusingehangaika kuchukua fomu na tumelipa fedha, hiki kwangu hakipo sawa na natafuta haki yangu."
Mgombea huyo aliongeza kwa kusema; "Nampongeza Rais aliye madarakani Wallace Karia amefanya mengi mazuri, lakini nadhani alipaswa kutoa nafasi ili watu tumpime kama yale mazuri aliyoyafanya yakamsaidie kwa wapiga kura, watoe nafasi ya wengine kumpa changamoto, nataka kwenda kumsaidia."
TFF ilitangaza tarehe ya kuchukua fomu ikianza Jumatatu ya Juni 16 hadi kesho Ijumaa saa 10 jioni ambapo kwa nafasi ya Urais fomu inagharimu Sh500,000 na inaelezwa kuna wagombea kadhaa karibu watano wameshachukua fomu mbali na wale wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Mwanasheria wa mgombea huyo, Wakili Aloyce Komba alisema: "Haoni kama kila kitu kinaweza kufanyika siku mbili, hivyo kama kuna namna imefanyika basi ni jinai, vyombo husika vinatakiwa kuchunguza hilo ili watu wote wapate haki, kama watu wameitwa kuchukua fomu inakuwaje akose wadhamini ambao ni wajumbe, sasa pesa za watu zisiende bure."
Hata hivyo, juzi Jumanne (Juni 17), TFF ilitoa angalizo kwa wagombea kwa kuwataka kuhakikisha wanapata Kanuni za uchaguzi huo na kubainisha kuwa kwa wale ambao tayari wameshachukua fomu, walitakiwa kuwasiliana na Sekretarieti ya TFF ili kupata Kanuni hizo.
Mabadiliko ya Kanuni za uchaguzi wa TFF yalifanyika na kupitishwa mwaka 2021 na iliwekwa bayana wajumbe wasiopungua watano wanaweza kumdhamini mgombea, lakini hawapaswi kujirudia kwa maana mjumbe akimdhamini mtu mmoja hawezi kumdhamini wengine.
Kilio kama hiki ndicho kilichowahi kuwakuta wagombea katika uchaguzi uliopita ambao uliwaengua baadhi ya wagombea ambao hawakuwa wamezisoma na kuzielewa kanuni hizo zilizopitishwa katika Mkutano Mkuu wa TFF uliofanyika mjini Kigoma.