Waendesha baiskeli zaidi ya 100 kukutana Pedal Pursuit
Muktasari:
- Mashindano hayo yanayolenga kuwaandaa waendesha baiskeli kwa mashindano ya kimataifa, yamekuja na zawadi ya jumla ya Sh12 milioni kwa washindi wa makundi tofauti, kiwango kinachoelezwa kuwa kikubwa kuwahi kutolewa katika mashindano ya baiskeli Tanzania.
MCHEZO wa baiskeli hapa nchini unatarajiwa kushuhudia ushindani mkali Jumapili hii, Septemba 27, 2026 wakati makundi matano ambayo ni watoto, wanawake, wanaume, wazee na wanaojifurahisha yanayohusisha zaidi ya waendesha baiskeli 100 kutoka mikoa mbalimbali watakapokutana katika mashindano ya Pedal Persuit Training Race yatakayofanyika Coco Beach, Dar es Salaam.
Mashindano hayo yanayolenga kuwaandaa waendesha baiskeli kwa mashindano ya kimataifa, yamekuja na zawadi ya jumla ya Sh12 milioni kwa washindi wa makundi tofauti, kiwango kinachoelezwa kuwa kikubwa kuwahi kutolewa katika mashindano ya baiskeli Tanzania.
Mwenyekiti wa Pedal Persuit Training Race, Hilary Edward Chuwa, amesema kitita hicho kimelenga kuwahamasisha waendesha baiskeli wa ndani, kuwapa utulivu na kuongeza ushindani kabla ya kushiriki mashindano ya kimataifa.
“Hii ndiyo race ya kwanza kuwa na zawadi kubwa kama hii tangu mashindano ya baiskeli Tanzania yameanza. Zawadi zote tulizojiandaa kutoa ni pesa taslimu Sh12 milioni,” alisema Chuwa.
Kulia ni Mwenyekiti wa Pedal Pursuit Training Race, Hilary Edward Chuwa, Kushoto ni Mshawishi wa mchezo wa baiskeli, Beto Zakaria
Chuwa alibainisha kwamba, zawadi hizo kwa upande wa wanaume, mshindi wa kwanza ataondoka na Sh1.5 milioni, wa pili Sh1.5 milioni na wa tatu Sh1 milioni, huku akibainisha kwamba, tatu bora pia itazawadiwa tuzo maalum.
Zawadi hizo zitaendelea hadi nafasi ya 10, ambapo wa nne atapata Sh700,000, wa tano Sh500,000, wa sita Sh400,000, wa saba Sh300,000, wa nane Sh250,000, wa tisa Sh200,000 na wa kumi Sh150,000.
Kwa upande wa wanawake, washindi watano wa kwanza watazawadiwa, ambapo atakayeshika nafasi ya kwanza atapata Sh1 milioni, wa pili Sh700,000, wa tatu Sh500,000, wa nne Sh300,000 na wa tano Sh200,000. Pia wa kwanza na wapili akipata tuzo maalum.
Kwa kundi la Veterans, linalowahusisha waendesha baiskeli wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, mshindi wa kwanza atapata Sh500,000, wa pili Sh300,000 na wa tatu Sh200,000.
Aidha, mshambuliaji bora, maarufu kama Aggressive Rider, atajinyakulia Sh300,000, wakati timu itakayoonyesha mbinu bora za kiufundi (Best Team Tactics) itapata Sh500,000.
Mbio hizo zitafanyika katika mzunguko unaoanzia Aga Khan hadi Masaki, huku mzunguko mmoja ukiwa na urefu wa kilomita 17.
“Wanaume na Veterans watakimbia mizunguko sita, sawa na kilomita 102, wakati wanawake watakimbia mizunguko mitano, sawa na kilomita 85. Kwa upande wa Fun Riders, watakimbia mizunguko miwili,” alisema Chuwa.
Chuwa alisema ada ya ushiriki ni Sh15,000 ambayo ni rafiki kwa kila Mtanzania, huku akibainisha kwamba waendesha baiskeli kutoka Shinyanga, Geita, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro na Zanzibar wanatarajiwa kuwasili kesho Jumamosi.
Ili kuhakikisha mashindano yanaendeshwa kwa kuzingatia viwango na sheria za kimataifa, waandaaji wamewaalika makamisaa na marefarii kutoka Rwanda kwa ajili ya kusimamia mbio hizo pamoja na kutoa elimu ya kiufundi kwa washiriki na waamuzi wa ndani.
Akizungumzia mpango wa kuibua vipaji vya watoto, Mshawishi wa Mchezo wa Baiskeli, Beto Zakaria, alisema wameanzisha mradi wa Kanyaga Mbele, unaolenga watoto wenye umri wa kuanzia miaka mitano.
Alisema mradi huo unalenga kujenga msingi wa mchezo wa baiskeli kuanzia umri mdogo kwa kuwafundisha watoto nidhamu ya uendeshaji, lishe bora kabla na baada ya mbio pamoja na matumizi sahihi ya vifaa vya usalama.
Beto pia alisisitiza umuhimu wa mchezo huo katika kuboresha afya na kukuza sekta ya utalii nchini.
Pedal Persuit Training Race, ambayo imefanyika zaidi ya mara 15 katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, imekuwa jukwaa la kuibua vipaji na kuwaandaa waendesha baiskeli wa Tanzania kwa mashindano makubwa.
Kupitia jukwaa hilo, zaidi ya waendesha baiskeli 10 wamepata nafasi ya kushiriki Mashindano ya Dunia nchini Rwanda, huku wengine 15 wakishiriki Michezo ya Afrika nchini Kenya.
Bingwa wa Tanzania, Boniface Ngwata, ambaye ni zao la jukwaa hilo, alishika nafasi ya sita kati ya washiriki kutoka mataifa zaidi ya 100 katika mashindano yaliyofanyika Dubai mapema mwaka huu.