Vuka Deaf ndio basi tena Ligi ya Viziwi
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Mao kisiwani Unguja, Wakombozi ilitoka nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo uliowafanya sasa kwenda kucheza na Hope City Deaf hatua ya fainali.
KIPIGO cha mabao 2-1 ilichopokea Vuka Deaf katika mechi ya Ligi ya Viziwi Zanzibar iliyochezwa Septemba 24, 2026 dhidi ya Wakombozi, imehitimisha safari ya timu hiyo kucheza fainali.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Mao kisiwani Unguja, Wakombozi ilitoka nyuma na kufanikiwa kuibuka na ushindi huo uliowafanya sasa kwenda kucheza na Hope City Deaf hatua ya fainali.
Khamis Khatib ndiye aliyeanza kuifungia Vuka Deaf dakika ya 31, bao lililodumu hadi kipindi cha kwanza kilipomalizika.
Kipindi cha pili, Seif Hamad akaisawazishia Wakombozi dakika ya 69, kisha Rajab Yahya akaongeza bao la pili lililokuwa la ushindi dakika ya 90.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kocha wa Vuka Deaf, Abdalla Omar, amesema awali alikuwa na matarajio ya kutopoteza mchezo wowote lakini hayo ndio matokeo ya mpira, hivyo anakubaliana nayo.
Amesema anakutana na changamoto kubwa katika ufundishaji wake kwani inamlazimu asubirie hadi kipindi kimalizike ndipo atoe maelekezo kwa wachezaji wake.
“Tumepoteza mechi yetu na nimekubaliana na matokeo hayo kwa sababu ndio mpira, hivyo nitajipa kwa mashindano ya msimu ujao,” amesema.
Pia kocha huyo amewasihi viongozi kuendelea kuipa sapoti ligi hiyo kwani baada ya kumalizika watakwenda Ethiopia kuiwakilisha Zanzibar kimataifa.
Vuka Deaf katika mzunguko wa kwanza ilipocheza dhidi ya Wakombozi, matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1 ambapo mechi hiyo ilishuhudiwa Ibrahim Idd akiitanguliza Wakombozi kwa bao la dakika ya 29, kisha Vuka Deaf ikasawazisha dakika ya 56, mfungaji akiwa Ali Hassan.
Kwa upande wa Hope City Deaf, ilipocheza dhidi ya Zandeaf katika mzunguko wa kwanza, ilipoteza kwa mabao 2-1, ikaja kulipa kisasi mzunguko wa pili kwa ushindi wa mabao 4-1.
Ligi hiyo iliyoanza Septemba 17, 2026 kwa kushirikisha timu nne kutoka Unguja, tamati yake ni Septemba 27, 2026 ambapo lengo la kuanzishwa kwake ni kupata wachezaji wa timu ya taifa ya viziwi kwa ajili ya mashindano ya Kimataifa yatakayofanyika nchini Ethiopia.