VPL ya msimu huu kazi ipo
Muktasari:
- Tayari klabu 16 zitakazoshiriki ligi ya msimu huu zikiwamo tatu zilizopanda daraja, Mbao FC ya Mwanza, African Lyon ya Dar es Salaam na Ruvu Shooting zilizorejea tena VPL zimekaa mguu sawa kuanza mshikemshike wa kusaka taji la ubingwa.
MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara maarufu kama Vodacom Premier League, umefunguliwa rasmi jana Jumatano kwa pambano la Ngao ya Jamii, kati ya Azam na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tayari klabu 16 zitakazoshiriki ligi ya msimu huu zikiwamo tatu zilizopanda daraja, Mbao FC ya Mwanza, African Lyon ya Dar es Salaam na Ruvu Shooting zilizorejea tena VPL zimekaa mguu sawa kuanza mshikemshike wa kusaka taji la ubingwa.
Ratiba ya ligi hiyo ilitolewa mapema siku chache baada ya hafla ya utoaji tuzo za waliofanya vyema kwa msimu uliopita, kabla ya hivi karibuni kupanguliwa kwa baadhi ya mechi za raundi za awali.
Kwa namna timu zilivyojiandaa na kuboreshwa kwa udhamini wa michuano hiyo ni wazi ligi ya msimu huu wa 2016-17 itanoga na Mwanaspoti inaangalia kwa ufupi namna utamu wa ligi hiyo itakavyokuwa na mambo ya kuepuka ili isitie doa.
Usajili wa Uhakika
Licha ya kwamba klabu nyingi zimerudia kufanya usajili kwa kutumia mfumo wa kuita wachezaji na kuwafanyia majaribio, angalau safari hii baadhi ya klabu zilikuwa makini na kufanya usajili mzuri, japo kipimo kizuri ni ligi itakapoanza.
Usajili mzuri na wa uhakika ni ule wa kutumia wataalamu wa kusaka vipaji kwa kuwafuatilia wachezaji miezi kadhaa kabla ya kuwaita kuwafanyia majaribio, lakini pengine mfumo tulionao umekuwa tatizo na kuendelea kuwajaribu na kuwasajili.
Ni wazi kuna ladha tofauti inayotarajiwa kuonekana katika msimu huu kwa kuzingatia maingizo mapya ndani ya klabu hizo 16 zikiwamo Simba, Azam, Mtibwa Sugar na hata Yanga itakayotetea taji lao.
Maandalizi mazuri
Jambo la msingi katika kuandaa timu itakayokuwa na ushindani ni kuwa na maandalizi mazuri ya mwanzo wa msimu (Pre Season) ili kuwajenga wachezaji kwa ajili ya kukabiliana na mikikimikiki ya mashindano.
Kipindi hiki cha maandalizi kabla Ligi Kuu kuanza ni muhimu sana katika kuwajenga wachezaji kwa stamina na kisaikolojia ili waweze kutoa ushindani wa uhakika wakati wa mashindano na kupata mafanikio.
Katika kipindi hiki mbali na mazoezi ya pamoja katika kambi, timu zimekuwa pia zikipata mechi za majaribio ambazo zimeongeza ubora na kuwajenga zaidi wachezaji na kujenga timu imara.
Hata pale penye matatizo, naamini klabu zimefanya marekebisho kabla kipyenga hakijapulizwa Jumamosi kwa mtifuano ndani ya ligi hiyo utakapoanza.
Ratiba isipanguliwe ovyo
Ni jambo zuri kwa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) iliyotoa ratiba ya msimu mpya kuepuka kupangua hovyo, hili ni tatizo kubwa.
Ingawa tayari imeshafanya jambo hilo hata kabla haijaanza, lakini ni lazima liepukwe na kutorudia makosa ambayo yanaonekana kuwa sugu kwa sasa.
Moja ya mambo ambayo yanaondoa ladha ya Ligi Kuu ni kubadilishwa mara kwa mara kwa ratiba jambo linaloondoa msisimko wa mashindano hayo.
Kwa hiyo ni vyema Bodi ya Ligi Kuu na klabu husika zisilazimishe mabadiliko ya ratiba bila ya kuwepo sababu za lazima ambazo haziwezi kuepukika.
Katika nchi za Ulaya mara kadhaa ukisika ratiba imebadilishwa itakuwa imetokana na sababu za majanga kama mvua kubwa au uwanja kujaa barafu lakini sio sababu za shaghala baghala ambazo hazina uzito wowote.
Wadhamini zaidi watafutwe
Pamoja na kwamba Ligi Kuu Bara inadhaminiwa na Kampuni ya Vodacom na Azam Media yenye haki za matangazo na baadhi ya klabu zina udhamini binafsi bado kuna haja ya wadhamini zaidi kutafutwa kwa ajili ya ligi hiyo na klabu zenyewe.
Bado udhamini unaotolewa sasa pamoja na kuzisaidia klabu kupunguza gharama za matumizi, lakini bado fedha wanazozipata hazitoshelezi mahitaji yote jambo ambalo ni la muhimu.
Iwapo klabu zitapata fedha ambazo zitatosheleza mahitaji yake yote, zitakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanya vizuri zaidi katika ligi hiyo.
Mbali na kufanya vizuri pia zitakuwa na uwezo wa kuhudumia timu za vijana ambazo ndilo chimbuko la kuweza kujenga timu imara za baadaye. Hili lina manufaa kwa klabu na taifa.
Waamuzi wawe makini
Moja ya tatizo ambalo linapigiwa kelele katika soka la Tanzania ni suala la waamuzi ambao, wanadaiwa hawachezeshi katika kiwango kinachostahili.
Waamuzi wanapochezesha vizuri na kwa umakini wanasaidia kuongeza uhondo wa ligi, lakini pia wanasaidia kupatikana mshindi halali na hatimaye bingwa wa kweli ambaye atakuwa na nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, waamuzi wakichezesha kwa upendeleo kutokana na ushabiki wa timu au rushwa au sababu nyingine yoyote ile, kuna hatari ya kutotoa haki na kupatikana bingwa ambaye hakustahiki.
UTIMUAJI Makocha OVYO
Ingawa kuna baadhi ya watu wanasema makocha wanaajiriwa ili watimuliwe, lakini ili kujenga timu imara, ni lazima viongozi na wanachama wa klabu hizo kuwapa nafasi makocha.
Hakuna haja ya kumtimua kocha kwa sababu timu imefanya vibaya katika mechi chache bali apewe nafasi ili arekebishe mambo ili timu iweze kufanya vizuri.
Klabu ambayo itakuwa inafukuza makocha kila uchao itakuwa vigumu kufanya vizuri kwani, makocha nao wanahitaji muda mrefu ili kuweza kujipanga na kuiwezesha timu kufanya vyema.
Upangaji matokeo uepukwe
Athari nyingine kubwa katika soka ni kuwepo kwa upangaji wa matokeo wa mechi kwa namna yoyote ile kwani, hausaidii kuinua kiwango cha mchezo huo nchini.
Dhambi kubwa katika mpira wa miguu ni upangaji wa matokeo na hilo linapaswa kuepukwa kwa hali yoyote kwa kuwa inazorotesha mchezo huo nchini.
TFF na Bodi ya Ligi wanapaswa kuwa makini ili kuwachukulia hatua kali wale wote ambao, watabainika wameshiriki kupanga matokeo kwa namna yoyote ile.
Mashabiki wamiminike uwanjani
Moja ya raha ya soka ni kuwa na mashabiki uwanjani, hivyo ni muhimu kujiandaa na kumiminika viwanjani kwa wingi kushuhudia ligi kuu ya msimu ujao.
Hata hivyo, muhimu zaidi kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ni kutoa burudani safi kwa kuonyesha kandanda safi ili kuwavutia mashabiki waende uwanjani kushuhudia mechi hizo.
Huku tukiamini viwanja vingi vimekarabatiwa kipindi cha mapumziko ili kuufanya mchezo huo kuwa rahisi kwa wachezaji uwanjani.
Masoud Sanani ni Mwandishi wa Habari Mwandamizi, amewahi kufanya kazi Televisheni Zanzibar,Uhuru na Mzalendo, Bussiness Times [Mhariri mwanzilishi wa Spoti Starehe] na Mwananchi. Alikuwa mkurugenzi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania [TEF]. Anapatikana kwa email [email protected]. Simu 0712-020020