Vodacom Nyerere Cycling Tour yaenzi fikra za Mwalimu
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ wakati wakishangilia ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Botswana. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Zaidi ya waendesha baiskeli 210 walishiriki katika ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 5 hadi 14, ikiungwa mkono na Vodacom Tanzania Plc. Ziara hiyo imelenga kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia shughuli zinazolenga kuboresha elimu, kutunza mazingira na kuongeza uelewa wa jamii.
Msafara wa Baiskeli ya Nyerere (Vodacom Nyerere Cycling Tour) 2026 imehitimishwa Butiama baada ya waendesha baiskeli kukamilisha safari ya kilomita 1,450 kutoka Bagamoyo, ikiunganisha michezo na juhudi za kuboresha maisha ya jamii zilizopo kando ya njia waliyopita.
Zaidi ya waendesha baiskeli 210 walishiriki katika ziara hiyo iliyofanyika Oktoba 5 hadi 14, ikiungwa mkono na Vodacom Tanzania Plc. Ziara hiyo imelenga kuendeleza urithi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia shughuli zinazolenga kuboresha elimu, kutunza mazingira na kuongeza uelewa wa jamii.
Mbali na safari hiyo ndefu, kampeni hiyo imesaidia ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa, ukarabati wa vyumba 40, usambazaji wa madawati 1,000 katika shule 10 na ujenzi wa vyoo 50. Miradi hiyo inatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi zaidi ya 23,000.
Waendesha baiskeli wakiingia nyumbani kwa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mwitongo, Butiama mkoani Mara, wakati wa kuhitimisha msafara wa Vodacom Nyerere Cycling Tour 2026, msafara huo umedhaminiwa na Vodacom Tanzania Plc na kushirikisha zaidi ya waendesha baiskeli 200.
Aidha, miti 1,100 imepandwa katika shule 11 ili kuhamasisha utunzaji wa mazingira miongoni mwa wanafunzi na jamii zinazozunguka shule hizo.
Mkurugenzi wa Tehama wa Vodacom Tanzania Plc, Athumani Mlinga, alisema ziara hiyo imeonyesha namna michezo inavyoweza kuwaunganisha watu katika lengo moja huku ikichangia maendeleo ya jamii.
“Kufika Butiama ni zaidi ya kukamilisha safari ya baiskeli. Ni ukumbusho kwamba tunapowaunganisha watu na wadau katika kutimiza lengo moja, tunaweza kutumia nguvu ya michezo kuleta mabadiliko yenye maana,” alisema Mlinga.
Mtoto wa hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Madaraka Nyerere (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Vodacom Tanzania PLC na Stanbic Bank Tanzania wakati wa kilele cha msafara wa Baiskeli wa Vodacom Nyerere Cycling Tour 2026 zilizofikia tamati Butiama, mkoani Mara leo. Hafla hiyo ni sehemu ya Vodacom Nyerere Cycling Tour 2026, inayodhaminiwa na Vodacom Tanzania Plc, ili kuenzi fikra za Mwalimu Nyerere kupitia michezo na miradi ya maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, mmoja wa watoto wa Mwalimu Nyerere Madaraka Nyerere, alisema mpango huo unatoa fursa ya kuunganisha urithi wa baba yao na vitendo vinavyowanufaisha Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo.
“Mwalimu aliamini katika umoja, kujitegemea na wajibu wa kila mmoja wetu katika kujenga taifa letu. Thamani halisi ya kuenzi urithi wake haipo tu katika kukumbuka misingi aliyosimamia, bali pia kuitekeleza kwa manufaa ya wananchi wetu, hususan kizazi cha vijana,” alisema Madaraka.
Mwanzilishi wa ziara hiyo, Gabriel Landa, alisema safari hiyo imeonyesha kuwa baiskeli zinaweza kutumika zaidi ya mashindano kwa kuchangia malengo mapana ya kijamii.
“Kila kilomita ilikuwa na changamoto zake, lakini kufahamu kwamba safari hii imehusishwa na mipango inayosaidia shule na utunzaji wa mazingira kulifanya mafanikio haya kuwa na maana zaidi,” alisema Landa.
Waendesha baiskeli walioshiriki Nyerere Cycling Tour 2026 wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Vodacom Tanzania Plc katika kijiji cha Mwitongo, Butiama, mkoani Mara, baada ya kuhitimisha msafara wa kilomita 1,450 kutoka Bagamoyo, uliofanyika kwa lengo la kuenzi urithi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku ukihamasisha maendeleo ya jamii kupitia michezo.
Sambamba na ziara hiyo, shughuli za kuelimisha jamii zilihusisha usalama barabarani, elimu ya fedha na namna ya kujikinga na utapeli wa kidijitali.
Kampeni hiyo iliungwa mkono na Vodacom Tanzania Foundation, Stanbic Bank Tanzania, BYD, Coca-Cola, Huawei, Afroil na ABC Bicycles.
Kukamilika kwa safari hiyo Butiama kumeacha ujumbe unaovuka mstari wa mwisho wa safari: michezo inaweza kuwaunganisha watu, kuenzi misingi ya taifa na kuchochea maendeleo yenye tija katika jamii.