Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Viwanja vya AFCON vyakumbwa na dosari za mabilioni

Muktasari:

  • Kamati yabaini ongezeko la gharama, dosari za zabuni na malipo ya kazi zisizotekelezwa, yataka fedha kurejeshwa na wahusika kuwajibishwa

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Serikali kuchukua hatua za kurekebisha dosari zilizobainika katika miradi ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo vya Arusha, Uhuru na Benjamin Mkapa, ikiwemo kuchunguza taratibu za zabuni, kurejesha fedha zilizolipwa bila stahili na kuwawajibisha waliohusika.

Katika taarifa yake kuhusu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka ya fedha 2023/2024 na 2024/2025, iliyowasilishwa bungeni jana Jumanne, Novemba 3, 2026, Kamati imebainisha changamoto katika usanifu wa miradi, ongezeko la gharama za mikataba, tathmini ya zabuni kupitia mfumo wa NeST, udhibiti wa ubora wa kazi na vifaa pamoja na uthibitishaji wa malipo.

Miradi hiyo ilianza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa lengo la kuboresha miundombinu ya viwanja hivyo, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Katika Uwanja wa Arusha, ukaguzi ulibaini usanifu wa awali ulizingatia kiwango cha Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) Daraja la Tatu badala ya Daraja la Nne, hali iliyosababisha mabadiliko ya wigo wa mradi na ongezeko la gharama la Sh5.99 bilioni bila VAT.

Pia, makadirio ya gharama yaliyokuwa kwenye mfumo wa NeST yalikuwa Sh187 bilioni, lakini mkataba ulitolewa kwa Sh338.54 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 81.

Wizara ilieleza makadirio ya awali hayakuzingatia kikamilifu mahitaji ya uwanja na kiwango cha CAF Daraja la Nne, huku muda mfupi wa maandalizi ya AFCON ukichangia ongezeko la gharama na matumizi ya utaratibu wa ununuzi usio na ushindani.

Uwanja wa uhuru

Hata hivyo, Kamati imeeleza maelezo yaliyotolewa hayakufafanua kwa kina sababu za ongezeko hilo wala namna thamani ya fedha ilivyohakikishwa.

Katika Uwanja wa Uhuru, ukaguzi ulibaini bei ya vifaa vya mwanga wa uwanja iliongezeka kutoka Sh185.8 milioni hadi takribani Sh1.85 bilioni.

Aidha, katika ukarabati wa uwanja huo, wizara ilimpa mkataba mzabuni aliyewasilisha bei ya Sh19.7 bilioni badala ya aliyetoa Sh18.8 bilioni, tofauti ya takribani Sh865 milioni.

Wizara ilieleza mzabuni aliyekuwa na bei ya chini hakuwa na uzoefu wa kutosha katika ujenzi wa viwanja vya michezo, hivyo ikamchagua mwenye uzoefu zaidi ili kupunguza hatari za utekelezaji wa mradi. Hata hivyo, CAG hakupata nyaraka za kutosha kuthibitisha kutokuwa na uwezo kwa mzabuni huyo.

Vilevile, ukaguzi ulibaini malipo yasiyostahili, kazi ambazo hazikufanyika na gharama za ziada katika viwanja vya Benjamin Mkapa, Uhuru na Arusha.

Wizara ilieleza ilikuwa imeanza kufuatilia makato ya malipo yaliyopitiliza, lakini haikuwa imewasilisha kwa CAG taarifa kamili kuhusu kiasi kilicholipwa zaidi, kilichorejeshwa, salio lililobaki na muda wa kukamilisha urejeshaji.

Katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kati ya vifaa vinne vya “switchgear” vilivyonunuliwa, ni vitatu tu vilivyofungwa kutokana na kukosekana kwa nafasi ya kifaa cha nne.

Wizara ilieleza mpangilio wa chumba cha umeme ungeboreshwa ili kukifunga, lakini wakaguzi hawakuwa wamepata uthibitisho wa utekelezaji wa hatua hiyo na uzingatiaji wa viwango vya kiufundi na usalama.

Uwanja wa AFCON Arusha

MAPENDEKEZO YA PAC

Kutokana na upungufu huo, Kamati imependekeza Serikali ihakikishe usanifu na mahitaji ya miradi ya viwanja vya michezo yanaandaliwa kwa usahihi kabla ya kutangaza zabuni, huku ongezeko lolote la gharama za mikataba likithibitishwa kitaalamu na kuidhinishwa kwa mujibu wa taratibu.

Pia, imeitaka Serikali kuchunguza dosari zilizobainika katika tathmini ya zabuni, matumizi ya mfumo wa NeST na uteuzi wa wakandarasi, kisha kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi huo.

Kamati imeweka muda wa utekelezaji wa azimio hilo kuwa ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027.

Pendekezo jingine ni Serikali kuhakikisha malipo yasiyostahili na fedha zilizolipwa kwa kazi ambazo hazijatekelezwa zinabainishwa na kurejeshwa, huku hatua za kuwawajibisha waliohusika zikichukuliwa kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu ubora wa miundombinu, Kamati imetaka kasoro zote za vifaa na kazi za ujenzi zirekebishwe kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu. Pia, imeelekeza kukamilishwa kwa mifumo ya umeme katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kazi husika kupokelewa rasmi.

Aidha, Serikali imetakiwa kuhakikisha mapendekezo yote ya CAG yanatekelezwa ndani ya mwaka wa fedha 2026/2027 na kuwasilisha Bungeni taarifa inayoonesha hatua zilizofikiwa, fedha zilizorejeshwa na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa.

Katika tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo 12 ya CAG kuhusu miradi hiyo, Kamati ilibaini kuwa hadi Agosti 14, 2026, mawili sawa na asilimia 16.7 yalikuwa yametekelezwa, tisa sawa na asilimia 75 yalikuwa katika hatua za utekelezaji na moja sawa na asilimia 8.3 lilikuwa halijaanza.

Uwanja wa Benjamin Mkapa

Wizara ilikuwa imeeleza kuwa inafuatilia urejeshaji wa fedha, kutoa mafunzo kwa wataalamu na kushughulikia changamoto za usajili katika taasisi za ukandarasi. Pia, ilieleza kuwa mchakato wa kuunda Wakala wa Usimamizi wa Miundombinu ya Michezo ulikuwa umekamilika, huku hatua za kumpata Mkurugenzi Mkuu zikiendelea.

Hata hivyo, Kamati ilibaini kuwa Wizara haikuwa imetoa ratiba ya mwisho ya kukamilisha mapendekezo, uthibitisho wa fedha zilizorejeshwa wala taarifa ya kuanza kazi kwa wakala huyo.

Kamati imeeleza kuwa utekelezaji wa mapendekezo hayo ni muhimu katika kuimarisha uwajibikaji, kuhakikisha thamani ya fedha za umma inapatikana na kuboresha usimamizi wa mikataba pamoja na ubora wa miradi ya Serikali.