Pamba, Dodoma Jiji zazidisha matumizi ya fedha, uwekezaji wa Sh2.5 bilioni wazalisha Sh29 milioni
Muktasari:
- Ripoti ya Kamati imebaini Jiji la Mwanza kutumia Sh1.48 bilioni kwa Pamba Jiji FC nje ya bajeti iliyoidhinishwa, huku Dodoma Jiji FC ikizidisha bajeti kwa Sh427.7 milioni, pamoja na udhaifu wa uendeshaji Uwanja wa Tanzanite Kwaraa.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeibua matumizi ya fedha za umma yanayozidi bajeti iliyotengwa kwa ajili ya timu za michezo zinazomilikiwa na halmashauri, huku ikibaini udhaifu katika usimamizi wa viwanja vya michezo nchini.
Katika taarifa yake kuhusu ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka ya fedha 2023/24 na 2024/25, iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma jana Jumanne, Novemba 3, 2026 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ado Shaibu alisema kamati imebainisha Halmashauri za Majiji ya Mwanza na Dodoma kufanya matumizi yasiyozingatia bajeti zilizoidhinishwa kwa timu zao za mpira wa miguu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Jiji la Mwanza lilitumia Sh1.48 bilioni kwa timu ya Pamba Jiji FC, fedha ambazo hazikuwa kwenye bajeti ya mwaka iliyoidhinishwa.
Kwa upande wa Jiji la Dodoma, Ado alisema halmashauri hiyo ilitenga Sh745 milioni kwa ajili ya timu ya Dodoma Jiji FC, lakini matumizi yalifikia Sh1.17 bilioni, hivyo kuzidisha bajeti kwa Sh427.7 milioni.
Kamati imeeleza matumizi hayo yanakiuka Mwongozo wa Uhasibu wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, unaomtaka Mweka Hazina kuhakikisha matumizi hayazidi bajeti iliyoidhinishwa.
Imebainisha kuwa hali hiyo inachangiwa na udhaifu wa mifumo ya ufuatiliaji wa matumizi ya halmashauri, huku ikionya kuwa uchepushaji wa fedha unaweza kusababisha shughuli nyingine zilizopangwa kutotekelezwa.
UWANJA WA SH2.5 BILIONI WAZUA MASWALI
Katika eneo la miundombinu ya michezo, Kamati imebaini udhaifu katika uendeshaji na usimamizi wa Uwanja wa Mpira wa Tanzanite Kwaraa, uliopo Babati, ambako Serikali iliwekeza Sh2.5 bilioni kupitia Halmashauri ya Mji Babati.
Taarifa inaeleza Julai 29, 2024, halmashauri hiyo iliingia makubaliano na klabu ya soka ya Fountain Gate FC kwa lengo la kuboresha utendaji na usimamizi wa uwanja huo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, halmashauri ilipaswa kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kukamilisha miundombinu pamoja na kulipia gharama za umeme na maji, huku Fountain Gate FC ikiwajibika kutunza uwanja kwa gharama zake na kusaidia maendeleo na matengenezo yake.
Hata hivyo, uchambuzi wa Kamati umebaini licha ya uwekezaji wa Sh2.5 bilioni, uwanja huo ulikuwa umezalisha mapato ya Sh29.27 milioni pekee, sawa na asilimia 1.17 ya thamani ya uwekezaji.
Kamati imeeleza kuwa kwa kiwango hicho cha mapato, kurejesha gharama za uwekezaji kunaweza kuchukua takriban miaka 85.
Changamoto nyingine zilizobainishwa ni kukosekana kwa mpango mahususi wa ukarabati na matengenezo ya uwanja, kutowekwa wazi kwa mchango wa Fountain Gate FC katika matengenezo, kutokuwepo kwa sera ya uwekezaji na uendelevu wa uwanja pamoja na kutokamilika kwa baadhi ya miundombinu na ukosefu wa huduma muhimu.
Kamati imeeleza kuwa mapungufu hayo yametokana na halmashauri na Fountain Gate FC kutotekeleza kikamilifu majukumu yao kwa mujibu wa makubaliano, huku hati hiyo ikiwa haina ufafanuzi wa kutosha kuhusu masuala ya fedha na taratibu za uendeshaji.
Akitoa maelezo mbele ya Kamati, Ofisa Masuuli alisema hati ya makubaliano kati ya halmashauri na Fountain Gate FC itafanyiwa marekebisho ili kuweka masharti yaliyo wazi kuhusu michango ya fedha, mgawanyo wa gharama na muda wa utekelezaji kwa kuzingatia matakwa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).
Kutokana na hali hiyo, Kamati imemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Babati kuhakikisha mapungufu yote yaliyobainishwa yanaondolewa haraka ili kuboresha usimamizi na kuongeza tija ya uwekezaji katika uwanja huo.
Taarifa hiyo inaeleza uwekezaji katika michezo ni sehemu ya majukumu ya halmashauri katika kukuza ustawi wa kijamii, kiuchumi, burudani na afya za wananchi, hivyo usimamizi wa fedha na miundombinu yake unapaswa kuzingatia uwajibikaji na tija.