Vigogo wang'oka Simba, Mpira Pesa huru
Geofrey Nyange 'Kaburu'
MWANDISHI WETU VIGOGO wawili wazito na wenye ushawishi mkubwa kwenye maamuzi ya ndani ya Simba wamebwaga manyanga lakini hata kabla barua zao hazijajadiliwa Kamati ya Utendaji imelifungulia tawi la Mpira Pesa la Magomeni. Waliojiuzulu kwa hiari ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope na Makamu Mwenyekiti, Geofrey Nyange 'Kaburu' kutokana na mwenendo mbaya wa klabu kwenye ligi na michuano ya kimataifa. Mwenyekiti wa Muda wa Kikao cha kamati ya utendaji, kilichofikia uamuzi huo, Joseph Itangare 'Kinesi' alisema kuwa sababu kubwa ni kuleta umoja ndani ya klabu. "Hatuhitaji tena mpasuko katika Simba ni wakati wa kushirikiana na kuleta hamasa kwa wachezaji, tunataka kuleta umoja kwa kuwa bado tuko katika mapambano ya kuinusuru timu," alisema Itangare. Kiongozi wa tawi hilo, Masoud Awadh alisema; "Timu imeyumba lazima waone umuhimu wetu, sisi hatuna kinyongo kwa sababu tunafanya kazi kwa maslahi ya timu na si wachezaji wachache, kwanza tunataka Mzee Khamis Kilomoni atambue kesi ipo mahakamani na yeye anatakiwa kuhudhuria Machi 18 kama anavyotakiwa kwani kila anapoitwa anakaidi tunamtaka afanye hivyo mara moja," alisema. Kundi la mpira pesa lilimfungulia kesi Hamis Kilomoni baada ya kudai kuwa wanatumiwa na matajiri wa klabu kuihujumu timu na kwa sasa kesi hiyo ipo mahakamani na itasomwa tena Machi18.