Vigogo Simba wategeana zoezi la uchukuaji fomu
Muktasari:
- Tofauti hiyo imeonekana leo, ambapo idadi ya watu waliojitokeza katika eneo la ofisi hizo imekuwa ndogo ikilinganishwa na siku zilizopita, ambazo zilishuhudia vigogo mbalimbali wa Simba wakifika kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi.
MAZINGIRA ya uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Klabu ya Simba katika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), yamekuwa tofauti na siku zilizopita huku mchakato ukiendelea kwa utulivu.
Tofauti hiyo imeonekana leo, ambapo idadi ya watu waliojitokeza katika eneo la ofisi hizo imekuwa ndogo ikilinganishwa na siku zilizopita, ambazo zilishuhudia vigogo mbalimbali wa Simba wakifika kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi.
Miongoni mwa waliojitokeza kuchukua fomu leo ni Wilfred Nyamwija, ambaye ameingia kwenye mchakato huo kwa kuwania nafasi ya ujumbe ndani ya klabu hiyo.
Jina jingine lililojitokeza leo ni Salum Hamidu, Makamu Mwenyekiti wa Matawi ya Simba jijini Dar es Salaam, ambaye pia alifika kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya uongozi ndani ya klabu hiyo.
Kujitokeza kwa Nyamwija na Hamidu kumeongeza majina mengine katika orodha ya wanaotaka kushiriki kwenye uongozi wa Simba, wakati mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu hiyo ukiendelea.
Hata hivyo, tofauti na siku zilizopita, leo hakukuwa na shamrashamra kubwa wala mkusanyiko wa watu wengi katika eneo la ofisi hizo huku zoezi likiendelea kwa utulivu.
Hali hiyo iliambatana na mazingira ambayo baadhi ya waliojitokeza kuchukua fomu hawakuwa tayari kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua zao au mipango yao katika uchaguzi huo.
Katika siku zilizopita, zoezi hilo lilikuwa likivuta hisia za mashabiki na wadau wa Simba kutokana na majina ya watu waliojitokeza kuchukua fomu, huku kila hatua ikifuatiliwa kwa karibu na wanachama wa klabu hiyo.
Katika siku ya kwanza ya zoezi hilo, Novemba 16, baadhi ya waliojitokeza kuchukua fomu ni Geofrey Nyange Kaburu, aliyekuwa akiwania nafasi ya mwenyekiti, pamoja na Christopher Mwansasu, aliyechukua fomu ya kugombea ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.
Novemba 17, Agness Daniel, maarufu kama Aggy Simba, naye alijitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya ujumbe wa klabu, hatua iliyoendelea kuongeza mvuto katika mchakato huo.
Tofauti na siku hizo zilizotangulia, leo hakukuwa na mkusanyiko mkubwa nje ya geti la ofisi za TFF, kama ilivyokuwa Novemba 17, ambapo baadhi ya watu waliokuwa wamevalia jezi za Simba walifika wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali.
Watu hao walionekana wakitoa kauli za kudai haki yao, sambamba na kuimba nyimbo na kupiga ngoma katika eneo hilo, hali iliyoongeza mvuto wa zoezi hilo.
Hata hivyo, utulivu wa leo umeacha maswali kuhusu hatua zinazofuata za baadhi ya vigogo wa klabu hiyo katika mchakato wa uchaguzi, huku muda wa kuchukua fomu ukiendelea.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Januari 30, 2027, badala ya Januari 3 kama ilivyokuwa imepangwa awali. Viongozi watakaopatikana wanatarajiwa kupokea kijiti kutoka kwa uongozi unaomaliza muda wake chini ya Mwenyekiti Murtaza Ally Mangungu.