Hersi afafanua ishu ya ujenzi wa uwanja Yanga
Muktasari:
- Baada ya kukamilika kwa Uwanja huo, Yanga itamiliki asilimia 50 kwa kuchangia ardhi ya Jangwani, huku Kampuni ya GSM itamiliki asilimia 50 kwa kugharamia uwekezaji wa kifedha.
Rais wa Yanga, Hersi Said, amezungumzia mchakato wa ujenzi wa Uwanja wa timu hiyo ambao mashabiki na wanachama wa Klabu hiyo wamekuwa wakiulizia mchakato wa ujenzi umefikia wapi.
Akizungumza leo Jumatano, Novemba 18, 2026, katika mkutano na wanahabari uliofanyika makao makuu ya Yanga, Jangwani, jijini Dar es Salaam, Hersi amesema baada ya makubaliano ya ujenzi wa uwanja, kumekuwa na mawasiliano ya muda mrefu na serikali katika kupata muongozo na kulifuatilia jambo hilo.
“Naamini wanachama na wapenzi wa Yanga walikuwa wanafuatilia mbona hatuanzi kujenga uwanja.
“lakini niwaambie sisi tumefuata kanuni na taratibu kupitia muongozo wa serikali. Hatuji tu tukasema kwa kuwa tumeshasaini makubaliano, tunaanza kujenga Uwanja,” amesema Hersi.
Amesisitiza kuwa katika hatua wanazopitia ni muongozo wa serikali na wao wanaufuata vizuri kwa ajili ya kuliendea jambo hilo kwa njia ambazo zitakuwa salama kwa pande zote mbili ambazo ni Klabu ya Yanga yenye ardhi na inayomilikiwa na wanachama lakini pia kuna wa mwekezaji.
“Tarehe mbili Novemba 2026 tuliitwa kwenye mkutano na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkutano huo ulishirikisha wajumbe wa baraza la wadhamini, uongozi wa Klabu ya Yanga na uongozi wa mwekezaji.
“Mkutano ule ulikuwa mzuri sana kwa sababu alituonyesha machaguo kadhaa ya ujenzi wa uwanja huo ili kwenda vizuri.
“Tulijifunza na tulipata muongozo mzuri kwenye mkutano huo na baada ya hapo siku ya jana, tarehe 17 tulipokea muongozo wa jinsi gani mradi huu tunaweza kuutekeleza,” amesema Injinia Hersi rais wa Yanga.