CAF yaipoka Kenya ofisi za AFCON, yahamishia Tanzania
Muktasari:
- Licha ya CAF kutotoa sababu za uamuzi huo, tetesi zinadai kwamba imefanya hivyo kutokana na mazingira rahisi ya ufanyaji kazi hapa Tanzania kulinganisha na Kenya.
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limeamua kuzihamisha ofisi za uratibu wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kutoka Nairobi, Kenya hadi Dar es Salaam, Tanzania.
Licha ya CAF kutotoa sababu za uamuzi huo, tetesi zinadai kwamba imefanya hivyo kutokana na mazingira rahisi ya ufanyaji kazi hapa Tanzania kulinganisha na Kenya.
Kutokuwepo kwa utulivu ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizoishawishi CAF kuhamishia shughuli hizo za uratibu wa AFCON 2027 jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo unaonekana unaweza kuwa na faida kubwa kwa Tanzania katika harakati zake za kuwania fursa ya kuandaa mechi ya ufunguzi au fainali ya mashindano hayo.
Inaripotiwa kwamba serikali ya Tanzania tayari imeshawapa ofisi hizo CAF katika Jengo ambalo lina Ofisi ndogo ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki eneo la Posta, Dar es Salaam na shughuli zao zimeanza hapo jana.
Fainali za AFCON 2027, zitaandaliwa kwa pamoja na nchi za Kenya, Uganda na Tanzania mwaka 2027.
Jumla ya timu 24 zitashiriki katika fainali hizo zitakazofanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027.