Utulivu wa Shekhan waigeuza Singida kuwa nyumbani
Muktasari:
- Shekhan katika mechi hizo nne, mbili amemaliza dakika zote tisini dhidi ya Fountain Gate na Kagera Sugar, huku dhidi ya Simba akicheza kwa dakika 85 na dakika 81 mbele ya Polisi Tanzania. Jumla amecheza kwa dakika 346, akikosa dakika 14 pekee.
TANGU kiungo mshambuliaji wa Yanga, Shekhan Khamis atolewe kwa mkopo kwenda Singida Black Stars, nyota huyo amekuwa na kiwango bora akifunga mabao mawili kwenye mechi nne za Ligi Kuu Bara alizocheza msimu huu.
Shekhan katika mechi hizo nne, mbili amemaliza dakika zote tisini dhidi ya Fountain Gate na Kagera Sugar, huku dhidi ya Simba akicheza kwa dakika 85 na dakika 81 mbele ya Polisi Tanzania. Jumla amecheza kwa dakika 346, akikosa dakika 14 pekee.
Kiungo huyo amefunga dhidi ya Simba na Polisi Tanzania, kiwango kinachompa nafasi ya kuanza kuaminika zaidi kwenye kikosi cha kocha Papy Kimoto, tofauti na kipindi chake Yanga ambako alikuwa akipata muda mchache wa kucheza.
Mabadiliko makubwa kwa Shekhan yanaonekana kwenye namna anavyocheza na kufanya maamuzi akiwa uwanjani. Singida imempa nafasi ya kucheza kwa uhuru zaidi, jambo ambalo limemsaidia kurejesha kujiamini na kuonyesha uwezo uliowahi kuonekana alipokuwa JKU ya Zanzibar kabla ya kuhamia Yanga.
Tofauti nyingine inayojitokeza ni utulivu wake kwenye matukio ya mwisho. Shekhan sasa anaonekana kuwa na subira zaidi anapokuwa na mpira, akifanya maamuzi bila papara, kitu ambacho kinaweza kuwa moja ya sababu zinazomsaidia kuwa na mchango mkubwa katika eneo la mwisho.
Mfano mzuri ni mchezo dhidi ya Simba ambao Singida Black Stars ilipoteza kwa mabao 2-1. Shekhan ndiye aliyeifungia Singida bao hilo, akitumia vyema nafasi aliyopata baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jeancy Mboma.
Katika tukio hilo, kipa wa Simba, Hussen Abel, alitoka kujaribu kuokoa mpira, lakini Shekhan hakufanya haraka wala kupoteza utulivu, alitumia nafasi hiyo kuukwamisha mpira wavuni na kuipa Singida bao la kufutia machozi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Shekhan amesema bado hajafikia kiwango chake, akisisitiza kuwa ushindani ndani ya Singida Black Stars ni mkubwa na kila anapopewa nafasi anatakiwa kuitumia kuonyesha kwa nini anastahili kuendelea kuaminiwa na kocha.
“Kwanza sina budi kushukuru, bado sijajihakikishia namba kwa sababu Singida ina wachezaji wengi wazuri, hasa kwenye eneo la kiungo, kwa hiyo ninapoaminiwa na kocha napaswa kuongeza juhudi, kujipanga na kila kitu, kupambana na ligi ngumu. Pengine hapa nilipo ndio njia yangu ya kunifungulia milango au hata kutoka nje, huwezi kujua,” amesema Shekhan.
Msimu uliopita akiwa Yanga, alicheza mechi nane akifunga bao moja lakini hadi sasa amecheza nusu ya mechi za msimu uliopita na tayari amefunga mabao mawili.