Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UPANGAJI MATOKEO: Laana inayolitafuna soka la Tanzania-2

Said El Maamry

Muktasari:

Inaaminika kwamba matukio ya upangaji matokeo hasa katika miaka ya 1980, yalikuwa yakichangiwa na ukweli kwamba timu nyingi zilikuwa chini ya taasisi za serikali.

KATIKA toleo lililopita tuliona jinsi Tukuyu Stars ilivyofanyiwa hujuma mwaka 1984 ili isipande Daraja la Kwanza baada ya timu za Kurugenzi na Biashara kupanga matokeo na Kurugenzi kufungwa mabao 10-0 ambayo yangeiwekea Biashara mazingira ya kusonga mbele na kupanda Daraja la Kwanza. Endelea...

Inaaminika kwamba matukio ya upangaji matokeo hasa katika miaka ya 1980, yalikuwa yakichangiwa na ukweli kwamba timu nyingi zilikuwa chini ya taasisi za serikali.

Kwa mfano mkoani Mbeya, Kurugenzi ilikuwa chini ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wakati Biashara ilikuwa chini ya Mamlaka ya Biashara ya Mkoa (RTC) wakati Usagishaji ilikuwa chini ya Shirika la Usagishaji (NMC), zote hizi ni taasisi za serikali. Hali ilikuwa hivyo hivyo kwa mikoa mingine.

Mchezaji mmoja wa Kurugenzi aliliarifu gazeti hili jinsi mechi yao dhidi ya Biashara ilivyopangwa ili kuisaidia Biashara na kuibana Tukuyu isipate nafasi ya kutamba Ligi Daraja la Pili na baadaye kushiriki Ligi ya Kanda ambako mshindi hupanda na kucheza Ligi Daraja la Kwanza (Sasa Ligi Kuu).

“Tukuyu walikuwa na timu imara na Mbeya kulikuwa na ushindani kati ya Tukuyu na baadhi ya timu, baadhi yetu tuliarifiwa mapema kuhusu mpango wa kuisaidia Biashara na kuwapa nafasi ya kutufunga mabao 10-0,’’ alisema mchezaji huyo ambaye pia alikuwa mwajiriwa wa serikali.

Said Hamad El-Maamry alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT-sasa TFF) baada ya FAT kubaini kuwapo kwa matukio ya upangaji matokeo katika ligi za chini, mwaka 1985 aliviagiza vyama vya soka vya wilaya na mikoa kuchukua hatua dhidi ya timu ambazo zinapanga matokeo ya mechi zao.

El-maamry ambaye kwa sasa ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), aliwaarifu waandishi wa habari azimio hilo ambalo lilifikiwa katika mkutano mkuu wa FAT uliofanyika mkoani Tabora.

Alisema kwamba uamuzi huo ulifikiwa baada ya wajumbe wengi wa mkutano mkuu wa FAT kutoa malalamiko yao kuhusu kuongezeka kwa vitendo vya upangaji matokeo katika ligi za chini.

Inapofikia hatua wajumbe wa mkutano mkuu ambao ni wawakilishi kutoka mikoa yote ya Tanzania wanalalamikia vitendo vya upangaji matokeo maana yake ni kwamba tatizo ni kubwa.

Kwa hali hiyo, ni wazi kwamba kuna wachezaji wengi wa soka nchini wenye vipaji ambao wamenyimwa fursa za kuonyesha vipaji vyao na kung’ara katika ligi kubwa nchini kama ambavyo ingetokea kwa timu ya Tukuyu ambayo mwaka 1986 ilitwaa taji la Ligi Daraja la Kwanza. Tukuyu pengine wasingefikia hatua hiyo kama si MRFA kuingilia kati na kufuta matokeo ya mechi ya Kurugenzi na Biashara.

Kwa maana nyingine kina Godwin Aswile na wenzake wa Tukuyu wasingeweza kutamba hadi Ligi Daraja la Kwanza na kusajiliwa na timu za Yanga, Simba na hata kuwa wachezaji tegemeo wa timu ya taifa.

Simba kushuka daraja

Mwaka 1987, historia mpya katika soka la Tanzania ilikuwa mbioni kuandikwa, wakati ambao Simba, moja ya klabu kongwe nchini iliyoanzishwa mwaka 1936 ilipokuwa katika hatari ya kushuka daraja, kutoka Daraja la Kwanza na kucheza Daraja la Pili.

Katika kipindi hicho klabu ya Simba ilikuwa na matatizo na mizozo ya mara kwa mara kati ya viongozi na wanachama wao, wanachama walikuwa wakitaka ufanyike mkutano wa dharura kuinusuru klabu, huku wengine walikuwa wakitaka mkutano na uchaguzi mkuu.

Viongozi wa Simba wakiongozwa na Jabir Shikamkono walikuwa katika kipindi kigumu na wenye hofu ya kuitisha mkutano wa dharura kwani mkutano huo ungeweza kutumiwa na wanachama waliokuwa na hasira kuwaondoa madarakani.

Kwa upande mwingine, timu ilikuwa ikicheza vibaya katika mechi zake za Ligi Daraja la Kwanza, wakati ligi hiyo ikiwa na timu 10, katika mechi 16 Simba iliambulia pointi 14, ilishinda mechi sita na kutoka sare mbili, mechi nyingine zote ilifungwa. Kila mechi ya ushindi wakati huo ilikuwa ina pointi mbili.

Habari kubwa iliyotawala vyombo vya habari ni kuhusu uwezekano wa Simba kushuka daraja, ni vipi wanachama na wapenzi wa Simba walikuwa wamejiandaa kuiona timu yao ikicheza kwa mara ya kwanza Ligi Daraja la Kwanza, hadhi ya Simba ilikuwa imeanza kuporomoka.

Ili kukwepa kushuka daraja, Simba walihitaji pointi moja na mabao mengi kutegemeana na mechi nyingine za mwisho za ligi hasa kwa timu ambazo kama Simba nazo zilikuwa katika mkakati wa kujinasua na janga la kushuka daraja.

Mechi za mwisho ilikuwa ni kati ya Nyota Nyekundu waliokuwa wakicheza na Pamba, RTC Kigoma na Biashara Mwanza mjini Kigoma na Reli dhidi ya Coastal Union. Baada ya kubaini kwamba nafasi yao ya kubaki Ligi Daraja la Kwanza ni ndogo, watu wa Simba waliamua kwamba ni lazima wapange matokeo ya mechi yao ya mwisho na Tukuyu iliyochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam (sasa Uwanja wa Uhuru).

Kufanikiwa kubaki Ligi Daraja la Kwanza kungeweza kuepusha matatizo ambayo yalianza kuikumba timu hiyo.

Hata hivyo, hawakuwa Simba peke yao waliokuwa wakikabiliwa na janga la kushuka daraja, Biashara Mwanza nao wakaweka mikakati ya kupanga matokeo na RTC Kigoma na Reli na Coastal.

 Pamba wao walikuwa wakipambana kutwaa taji na timu za Yanga na Majimaji ambazo zilikuwa katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi. Katika mechi hizo za mwisho, Yanga walikuwa wakicheza na Majimaji.

Shabiki mmoja wa Pamba aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika timu hiyo, alimwarifu mwandishi wa makala haya jinsi ambavyo watu wa Pamba walivyoamua kufanya kikao na watu wa Nyota Nyekundu, kikao hicho kilifanyika Mwanza Hoteli ili kuhakikisha timu hizo zinabebana.

“Waliomba msaada kwa imani kwamba Yanga wangeweza kupoteza mechi yao dhidi ya Majimaji na hivyo Pamba wangeweza kubeba taji la Ligi Daraja la Kwanza mwaka 1987, mpango uliokuwapo ni kwamba Pamba walitakiwa kuifunga Nyota Nyekundu 6-5, matokeo ambayo yangeisaidia Nyota Nyekundu isishuke daraja kwa faida ya mabao ya kufunga, pia Pamba ingejiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa taji la ligi.

Hata hivyo, wakati yote hayo yakiendelea, Nyota Nyekundu walikuwa na mpango mwingine tofauti baada ya kupewa taarifa hizo.

Nini kitaendelea, usipitwe na mwendelezo wa taarifa hii ya uchunguzi kuhusu upangaji matokeo, laana ambayo inaendelea kuliangamiza taratibu soka la Tanzania.

Itaendelea Jumamosi ijayo…