Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulikofikia mgogoro wa Gymkhana, mwekezaji uwanja wa Racket

MGOGORO Pict

Muktasari:

  • Dar es Salaam Gymkhana Club ni klabu kongwe na kubwa ya michezo na masuala ya kijamii inayomiliki na kuendesha viwanja vya michezo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Uongozi wa Klabu ya Gymkhana ya Dar es Salaam, Dar es Salaam Gymkhana Club (DGC) umemzuia mwekezaji aliyejenga viwanja vya mchezo wa Racket, kampuni ya East Africa Racket Sports Club Limited (EARSC), kuendelea na shughuli hizo.

Klabu hiyo kongwe na kubwa ya michezo na masuala ya kijamii jijini Dar es Salaam, inayomiliki na kuendesha viwanja vya michezo mbalimbali, imechukua uamuzi huo huku ikiwa na amri ya Mahakama ya Rufani inayoizuia kutekeleza uamuzi wake wa kumfukuza mwekezaji huyo mpaka rufaa yake itakapoamuliwa.

Hata hivyo, licha ya amri hiyo ya mahakama, uongozi wa Gymkhana umeizuia kampuni hiyo kuendelea na shughuli zake kwa madai kuwa japo imeruhusu wasiondolewe lakini haijasema kuwa waendelee na shughuli zake.

Katibu wa Gymkhana, Imani Alfayo alipoulizwa kuhusiana na mgogoro huo madai ya kupuuza amri ya mahakama, alijibu kwa ufupi tu kuwa uamuzi uko wazi.

“Angalia kwenye ripoti za mahakamani, kuna hukumu ambayo iko wazi. Wewe kaangalie mahakama ilichokisema na walichokisema, halafu utapata jibu lake. Mahakama imesema wazi kabisa, go and look at the court ruling, iko wazi,” alisema Alfayo.

Alipoelezwa kuwa katika uamuzi huo wanachokisema kuwa mahakama imeamuru wawepo tu lakini wasifanye biashara ndicho hakionekani, alihoji kuwa kwani mahakama imesemaje kisha akakata simu na hakupokea tena licha ya kupigiwa mara kadhaa.

Wakili anayemwakilisha mwekezaji huyo kwa sasa, Dk Onesmo Kyauke,  amelieleza Mwananchi kuwa kinachofanywa na uongozi huo wa Gymkhana ni utoto.

Amesema kuwa mwekezaji huyo alipanga hapo kwa ajili ya kufanya biashara, hivyo haiingii akilini kusema kuwa mahakama imezuia asiondolewe kwanza lakini asifanye biashara, na kwamba ingekuwa hivyo wasingekuwa na sababu ya kuiomba mahakama iamuru wasiondolewe.

"Kwa hiyo ni utoto tu ambao hawa jamaa wanajaribu kuufanya kwani hakuna tafsiri ya namna hiyo duniani," amesema Dk Kyauke.

Amefafanua kuwa ni sawa na mtu aliyepanga kwenye nyumba, mahakama inazuia usiondolewe kwanza lakini mwenye nyumba anamzuia kulala kwa maelezo kuwa mahakama imesema tu kuwa asiondolewe lakini haijasema aendelee kulala.

Hivyo amesema kwa kuwa wameshapata amri ya mahakama inayowaruhusu kuendelea na shughuli zao mpaka rufaa yao itakapoamuliwa, basi wataingia kwa sababu wana haki hiyo.

"Wakati mwingine ukishakuwa na haki unaruhusiwa kutumia hata nguvu ya kawaida. Kwa hiyo sisi tunaingia kama wanataka wao ndio waende mahakamani wakaombe tafsiri. Waende waseme sasa mbona hawa jamaa wanaendelea na biashara, otherwise (vinginevyo) watakuwa wanataka tu kusababisha fujo,” amesisitiza Wakili Kyauke. 

Dk Kyauke amesema kuwa licha ya mwekezaji huyo kutumia gharama kubwa kufanya uwekezaji, kiasi cha Sh2.5 bilioni, lakini sasa wanataka kumwondoa kabla ya mkataba tena bila hata fidia.

“Mkataba unasema kuwa wakivunja wanapaswa kumlipa fidia ya fedha alizowekeza lakini sasa hawataki kumlipa fidia bali wanataka tu aondoke," amesema Dk Kyauke.

Kwa mujibu wa Meneja Msaidizi wa EARSC, Abdallah Manyua, kampuni hiyo iliingia mkataba na Gymkhana kukodisha eneo na kujenga viwanja vya mchezo wa Racket uliosainiwa na Wadhamini wa Gymkhana kwa miaka mitano, kuanzia 2024 mpaka 2029. 

Amesema kuwa wamefanya uwekezaji mkubwa kwa kujenga viwanja vya kisasa lakini baada ya kuingia uongozi mpya wa Gymkhana unataka kuwafukuza kwa madai kuwa mkataba wao wa upangaji katika eneo hilo una kasoro.

"Wanadai kuwa tulioingia nao mkataba huo waliingia kwa maslahi yao na si kwa niaba ya kampuni," amesema Manyua.

Mshauri wa masuala ya uchumi wa kampuni hiyo, Dada Juju, amesema kuwa eneo hilo ndilo sehemu pekee ya michezo katika viwanja vya Gymkhana iliyojengwa vizuri na kwa thamani kubwa, uwekezaji unaofikia Sh2.5 bilioni.

"Kabla ya sisi kulichukua na kuliendeleza ilikuwa ni sehemu ambayo watu walikuwa wanajisaidia haja ndogo", amesema Juju na kuongeza kuwa ingawa walikuwa bado hawajaanza kuingiza faida, wamekuwa wakilipa kodi ya Sh1 milioni kila mwezi kwa ajili ya mazingira.

Kutokana na mgogoro huo, mwekezaji huyo alilazimika kufungua kesi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi dhidi ya Wadhamini wa Dar es Salaam Gymkhana Club na Dar es Salaam Gymkhana Club.

Pia aliomba na kupata amri ya zuio, ambapo Mahakama hiyo katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Mohamed Gwae, iliamuru hali iendelee kuwa kama ilivyokuwa mpaka kesi hiyo itakapoamuliwa.

Baadaye kesi hiyo ya Ardhi namba 97 ya 2026, iliondolewa mahakamani Julai 21, 2026, kabla ya kusikilizwa kutokana na masuala ya kiufundi, baada ya mahakama kukubaliana na pingamizi la awali lililoibuliwa na walalamikiwa.

Siku hiyo hiyo wajibu maombi walimwandikia mwekezaji huyo wakimtaka akabidhi eneo hilo likiwa wazi ndani ya siku saba.

Mwekezaji huyo aliwasilisha Mahakama ya Rufani notisi ya kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi na amri ya Mahakama Kuu kuifuta kesi hiyo. 

Pia aliwasilisha maombi ya kusitisha utekelezaji barua hiyo ya wajibu maombi kumtaka aondoke ndani ya siku saba akidai kwamba amewekeza fedha nyingi na kujenga sifa njema katika eneo hilo, ambavyo viko katika hatari ya kupotea endapo utekelezaji unaokusudiwa hautasitishwa.

Ingawa wajibu maombi (walalamikiwa) waliibua pingamizi, lakini Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Ignas Kitusi, Septemba 8, 2026 ilitupilia mbali pingamizi hilo.

Badala yake ilikubaliana na hoja za maombi ya mwombaji na ikatoa amri ya kuwazuia wajibu maombi kumwondoa mwekezaji huyo mpaka rufaa yake itakapoamuliwa.

Lakini Septemba 12, 2026 wafanyakazi wa kampuni hiyo walipokwenda ofisini katika viwanja hivyo, wakazuiwa na walinzi wa Gymkhana kufanya kazi yoyote.