Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukweli penalti ya Kagere

WAKATI tukio la penati tata iliyoipa Simba ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa likizua mjadala, wadau wa soka wamesema kuwa penati hiyo ilitolewa kimakosa na mwamuzi Elly Sasii.

Wakizungumza na Mwanaspoti kwa nyakati tofauti, baadhi ya waamuzi na wanasoka wa zamani wamesema kuwa ushahidi wa picha za video haikuwa penalti. Lakini hata kwenye mitandao ya kijamii Simba wamekuwa wakiwakera wenzao wa Yanga kwa kejeli kwamba; “mbona na nyie mlipewa ile ya Mwanza!”

Mwamuzi mkongwe Othuman Kazi alisema; “Kitu gani kimesababisha penati? Hassan Kabunda ule mpira hakuunawa na haujakwenda mkononi kwa namna yeyote ile, sasa sijui, Elly Sasii aliona kitu gani kama mpira kufuata mkono hakuna labda kama kulikuwa na tukio lingine lakini kwangu ‘handball’ kulikuwa hakuna.”

Kiungo wa zamani wa Kariakoo Lindi, Jemedari Said alisema; “Waamuzi wanatakiwa kuwa na uono mzuri wa mpira sasa kama Sasii alikuwa hajaona vizuri tukio lile, basi amekosea kutoa penati maana hakuna mchezaji yeyote ambaye aligusa mpira kwa mkono.

Lakini kinachoshangaza, makosa haya ya waamuzi yamekuwa yakizinufaisha zaidi timu kubwa na kuziumiza timu ndogo. Hapa tunapaswa kujiuliza kwamba kwa nini hatuoni waamuzi wakikosea kwa kuzipa penati za namna hii timu ndogo na badala yake kubwa ndio zinapata?

Kinachoumiza hawa KMC hii ni mechi ya pili wanaumizwa na uamuzi tata dhidi ya timu kubwa. Mechi dhidi ya Yanga,Yanga walipata penati ambayo haikustahili kwa bahati mbaya makosa haya yanakuwa ndio yanabadilisha matokeo ya mchezo,”alisema.

Kiungo wa zamani wa Simba, Amri Kiemba alisema ingawa haikustahili kuwa penati, mazingira ya tukio lenyewe yalimpa ugumu refa kuamua.

“Kikubwa mtu unatakiwa kuvaa uhusika wa refa, mazingira ya tukio na muda ambao tukio limetokea. Kwa yale mazingira hata mimi ningeweza kutoa penati,”alisema mchezaji huyo.

Kwa lile umbile la mchezaji kwa wakati ule, bila shaka lilimpa wakati mgumu refa kuamua na ikumbukwe kwamba alikuwa na muda mfupi wa kutafsiri na kuamua.”

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema; “Jambo la muhimu ni kuwa tumepata ushindi na pointi tatu. Ushindi tumeupataje na je penati ilistahili au haikustahili hilo sio jukumu langu kulizungumzia,” alisema Vandenbroeck.Mwenyekiti wa kamati ya waamuzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Soud Abdi alisema kuwa kama kuna tatizo lolote kwa mwamuzi, zipo mamlaka za kufanyia kazi.

“Kitaaluma nitakuwa siko sahihi nikianza kukomenti maana huwezi jua yeye aliona nini hadi akachukua uamuzi aliouchukua, lakini kama kuna utofauti au changamoto yoyote nadhani kuna kamati zinazohusika juu ya mambo ya namna hiyo.

“Ukiona mtu anatoa ushauri au anakosoa wakati yeye ni mwamuzi basi ujue anafanya makosa,”alisema Soud.

Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison alisema; “Tunaamini mamlaka husika zinaona haya na watachukua hatua stahiki.”

Penati hiyo iliyozua utata ilitolewa na mwamuzi Sasii katika dakika ya 74 kwa kile kilichoonekana na wengi kama refa huyo alihisi mmojawapo kati ya wachezaji wawili wa KMC, Hassan Kabunda na Israel Patrick alinawa mpira katika eneo la hatari la timu yake.

Hata hivyo picha za marudio ya runinga zinaonyesha kuwa hakukuwa na mchezaji yeyote wa KMC aliyenawa mpira wa kucheza rafu ambayo ingepelekea kuadhibiwa kwa pigo la penati.

Tukio hilo ni muendelezo wa nuksi waliyonayo KMC dhidi ya timu za Simba na Yanga msimu huu kwani zote zimebahatika kupata penati zisizostahili pindi zilipokabiliana nao. Ikumbukwe Oktoba 25 mwaka huu, Yanga walipata penati ya utata dhidi ya KMC iliyotolewa na refa Ramadhan Kayoko baada ya kudai Sarpong wa Yanga alifanyiwa madhambi katika eneo la hatari lakini hata hivyo picha za marudio za luninga zilionyesha kuwa mshambuliaji huyo hakuchezewa rafu.