Tuzo mbili zambeba Yassir Zanzibar
Muktasari:
- Yassir anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Ndijani kisiwani Unguja, amesema tuzo hizo mbili zimemuongezea nguvu ya kupambana na kujiamini.
MCHEZAJI wa Mpira wa Mikono Zanzibar, Yassir Juma Iddi, amesema tuzo mbili za mchezaji bora alizozipata katika mashindano ya UMITASHUMTA mwaka 2022 na 2023 zimempa alichokitamani muda mrefu.
Amesema tuzo hizo zimempa umarufu kwa wengine kujua kipaji chake na kuongeza kiwango cha uchezaji ili jina lake liendelee kung’ara kwa kila siku.
Yassir anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Ndijani kisiwani Unguja, amesema tuzo hizo mbili zimemuongezea nguvu ya kupambana na kujiamini.
“Tuzo hizo zimeniaminisha kuwa endapo nitafanya mazoezi kwa bidii nina uwezo wa kufika mbali zaidi na kufanya mambo makubwa,” amesema.
Amesema, tuzo hizo hakuzipata kwa bahati mbaya badala yake ni jitihada zake pamoja na kufuata maelekezo ya makocha wake akiwemo Kombo Ali Kombo na Daudi Martin Samson wamekuwa msaada kwake.
Ameongeza kuwa, anapenda kucheza mpira wa mikono kwa sababu namna ya mchezo huo unavyochezwa ni mzuri lakini umemsaidia kuwa imara katika masomo yake darasani.