Mchuano mkali vtuma vipya Mzizima Dabi
Muktasari:
- Msimu huu, Simba na Azam zimefanya usajili wa mastaa kadhaa kwa lengo la kuongeza nguvu katika maeneo ambayo makocha wao waliona yalikuwa na mapungufu. Hata hivyo, baada ya mechi za mwanzo, swali kubwa linabaki kuwa moja nani ameanza kuonyesha thamani ya usajili wake?
DABI ya Mzizima si vita ya Simba na Azam pekee, bali ni pambano ambalo kila msimu huja na sura mpya, matarajio mapya na presha kubwa kwa wachezaji wanaotua katika timu hizo.
Msimu huu, Simba na Azam zimefanya usajili wa mastaa kadhaa kwa lengo la kuongeza nguvu katika maeneo ambayo makocha wao waliona yalikuwa na mapungufu. Hata hivyo, baada ya mechi za mwanzo, swali kubwa linabaki kuwa moja nani ameanza kuonyesha thamani ya usajili wake?
SIMBA, MAKGALWA AMEWASHA
Simba imeingia msimu huu ikiwa na sura kadhaa mpya, ikiwamo Keletso Makgalwa, winga wa kushoto aliyesajiliwa kutoka Sekhukhune United ya Afrika Kusini.
Makgalwa tayari ameanza kutoa ishara anaweza kuwa mmoja wa silaha muhimu za Simba, baada ya kufunga bao katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mighty Wanderers.
Winga huyo aliingia akitokea benchi na dakika ya 87 akafunga bao la tano la Simba katika ushindi mkubwa wa mabao 6-0. Huo ni mwanzo unaoweza kumpa nguvu zaidi katika mechi inayofuata dhidi ya Azam.
Simba pia imeongeza nguvu katika maeneo mengine kupitia usajili wa Ibrahim Doumbia, mshambuliaji wa kati mwenye nguvu na kasi, ambaye anatarajiwa kuongeza ushindani kwenye safu ya mbele licha ya kutokufunga bao hata moja mpaka sasa.
Kikosi hicho pia kimeongeza ubunifu na ukabaji wakiwamo Ibraheem Jabaar, kiungo wa kati mkabaji kutoka Stellenbosch FC, huku Kelvin Nashon ambaye anaongeza ubunifu katikati baada ya kuwasili akitokea Singida SC.
Upande wa kulia, Simba imeongeza nguvu wakiwamo Bakari Msimu, winga machachari aliyesajiliwa kutoka Coastal Union.
Katika safu ya ulinzi, usajili wa Nathaniel Chilambo anaongeza ladha nyingine katika Dabi ya Mzizima, kwani beki huyo wa kulia ametua Simba moja kwa moja akitokea Azam FC, mpinzani wao mkuu.
Simba pia imeongeza nguvu mbele kupitia Ismail Mohamed Mgunda, mshambuliaji mwingine wa kati anayetarajiwa kuongeza ushindani na chaguo kwa benchi la ufundi.
AZAM WAMEANZA KUSUBIRI
Tofauti na Simba ambayo tayari imepata mabao kutoka kwa baadhi ya sura zake mpya, Azam bado inasubiri washambuliaji na mawinga wake wapya wafungue akaunti zao za mabao katika Ligi Kuu ya NBC au michuano ya kimataifa.
Azam imefanya usajili mkubwa, ikiwamo Henri Stanic, beki wa kati wa kimataifa kutoka Ubelgiji aliyewahi kucheza Stellenbosch FC, pamoja na Idumba Fasika, beki mzoefu aliyewahi kucheza Al-Ahly ya Libya.
Katika kiungo, Azam imeongeza nguvu wakiwamo Donovan Makoma kutoka Birkirkara FC ya Malta, huku Kipré Zunon, maarufu Kipre Junior, akirejea katika klabu hiyo baada ya kucheza MC Algiers ya Algeria.
Hata hivyo, macho mengi yako kwenye safu ya mbele ambako Azam imeongeza Henoc Molia, mshambuliaji mwenye umri wa miaka 22 kutoka FC Saint Eloi Lupopo ya DR Congo.
John Mano naye amesajiliwa kutoka Al-Akhdar ya Libya kuongeza chaguo la mshambuliaji wa kati, wakati Hassan Mubiru amekuja kutoka SC Villa ya Uganda kwa lengo la kuongeza kasi na ubunifu pembeni.
Azam pia imeongeza nguvu upande wa kushoto wa ulinzi kupitia Taiwo Abdulrafiu, beki kutoka Nigeria aliyesajiliwa kutoka Rivers United.
KIPRE, MOLIA, MANO
Kwa Azam, changamoto kubwa sasa si ubora wa majina yaliyosajiliwa, bali ni muda ambao wachezaji hao watahitaji kuzoea mfumo wa timu na kuanza kubadilisha nafasi wanazopata kuwa mabao.
Kipre Junior ana uzoefu wa soka la Tanzania na anajua presha ya kucheza katika timu kubwa, hivyo kurejea kwake kunaweza kuwa silaha muhimu kwa Azam.
Molia anabeba matarajio makubwa kutokana na umri wake na uzoefu alioupata DR Congo, wakati Mano anatarajiwa kuongeza ushindani wa moja kwa moja katika eneo la mshambuliaji wa kati.
Hapo ndipo Dabi ya Mzizima inaweza kuwa kipimo kizuri cha thamani ya usajili wao.
NANI ANAONGOZA?
Kwa kuangalia mwanzo huu wa msimu, Simba inaonekana kuwa mbele kidogo kwa upande wa mchango wa moja kwa moja wa sura zake mpya kwenye mabao, hasa baada ya Makgalwa kufunga dhidi ya Mighty Wanderers.
Azam, kwa upande wake bado inasubiri mlipuko wa mabao kutoka kwa washambuliaji na mawinga wake wapya.
Lakini hiyo haimaanishi usajili wa Azam umeshindwa. Msimu bado ni mrefu na thamani halisi ya mchezaji haipimwi kwa mechi chache pekee.
Dabi ya Mzizima ndiyo itakayotoa jibu kubwa zaidi kama Simba itaendelea kupata mabao kutoka kwa mastaa wake wapya au Azam itafungua ukurasa mpya na kuanza kuona usajili wake ukiwaka.