BAADA ya kupita siku 74, ambazo ni sawa na miezi miwili na siku 14 au wiki 10 na siku nne au dakika 106,560 na sekunde 6,393,600, hatimaye leo tunashuhudia mechi kali na ya kuvutia kati ya Azam FC dhidi ya Simba maarufu ‘Mzizima Derby’.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa saa 1:00 usiku, kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, jijini, Dar es Salaam, ni ya kisasi na rekodi kwa timu hizo, kutokana na matokeo ya mwisho waliyokutana na mwenendo wao hadi sasa msimu huu.
Timu hizo zinakutana tena ikiwa imepita siku 74, tangu mara ya mwisho kwao zilipokutana katika fainali ya Kombe la CRDB, msimu wa 2025-2026, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Kisiwani, Pemba na Simba kushinda kwa bao 1-0, Julai 4, 2026.
Katika mechi hiyo, bao la ushindi kwa Simba lilifungwa na kiungo nyota wa Azam FC, Yahya Zayd aliyejifunga dakika ya 62 na kuipa ubingwa wa kwanza wa CRDB, baada ya kupita miaka minne, tangu mara ya mwisho ilipolichukua msimu wa 2020-2021.
Baada ya mechi hiyo ya fainali, timu hizo zinakutana tena ikiwa ni pambano linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka kutokana na ubora wa wachezaji wa pande mbili, kabla ya kupisha kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Mechi ya leo ni ya 37 ya Ligi Kuu Bara kwa timu hizo kukutana, tangu kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, kilipopanda daraja rasmi baada ya kuifunga Majimaji ya Songea mabao 2-0, kwenye Ligi ya Taifa, Julai 27, 2008.
Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, mabao ya Azam FC yalifungwa yote na aliyekuwa nahodha na nyota wa kikosi hicho, John Bocco, ambaye aliifungia mabao 84, ya Ligi Kuu kuanzia msimu wa 2008-2009 hadi 2016-2017.
Tangu mwaka 2008, timu hizo zimekutana katika mechi 36 za Ligi Kuu Bara, ambapo kati yake, Simba ndio mbabe zaidi baada ya kushinda mara 15, wakati kwa upande wa Azam FC imeshinda mara saba, huku michezo 14, iliyobaki kwao ikiisha kwa sare.
Katika mechi hizo 36, walizokutana za ‘Mzizima Derby’, Simba imefunga jumla ya mabao 48 ya Ligi Kuu, huku kwa upande wa kikosi cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC kimefunga mabao 33, jambo linaloonyesha ushindani mkubwa kati yao.
Moja ya swali kubwa linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka Tanzania kujibiwa, ni jinsi ambavyo Azam FC inakabiliwa na rekodi ngumu ya kuivunja, kutokana na mwenendo mzuri wa kikosi hicho cha Simba cha kutopoteza katika Ligi Kuu Bara.
Rekodi ngumu inayosubiriwa ni ya kuivunja rekodi ya Simba ambayo tangu mara ya mwisho ilipochapwa na Azam FC, mabao 2-0, katika Ligi Kuu Bara, Desemba 7, 2025, ambao ni msimu wa 2025-2026, haijapoteza hadi sasa ikiwa ni mwendelezo pia mzuri.
Katika mechi hiyo iliyopigwa, Desemba 7, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini, Dar es Salaam, Azam FC ndio timu iliyoifunga Simba kwa mabao ya Jephte Kitambala dakika ya 81 na Idd Seleman ‘Nado’ dakika ya 88 na hadi leo haijapoteza.
Tangu Desemba 7, 2025 ambao ni msimu wa 2025-2026, hadi sasa msimu wa 2026-2027, Simba imecheza jumla ya mechi zake 30, za Ligi Kuu Bara, ambapo kati ya hizo imeshinda 23 na kutoka sare saba, huku ikifunga jumla ya mabao 52 na kuruhusu 10.
Simba ndio timu yenye matokeo mazuri kwa maana ya ushindi wa asilimia 100, baada ya kushinda mechi zote tano ilizocheza msimu huu wa 2026-2027, ikiwa na pointi 15, ambazo ni sawa na za vinara, Yanga inayoongoza ila zikitofautiana kwa mabao.
Kabla ya mechi ya jana ya Yanga dhidi ya Geita Gold, iliyochezwa kwenye Uwanja wa KMC, Complex, Dar es Salaam, mabingwa hao watetezi walikuwa wanaongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa tu, baada ya zote kushinda michezo mitano.
Kwa upande wa Azam FC iliyocheza mechi sita hadi sasa msimu huu, imekuwa na mwenendo wa kusuasua, japo ni miongoni mwa timu zenye matokeo mazuri inapocheza nyumbani, jambo linaloongeza mvuto na ushindani mzuri kwa miamba hiyo yote miwili.
Katika mechi sita ilizocheza Azam FC, tatu imecheza nyumbani na kushinda zote, ikizifunga TRA United mabao 2-1, Agosti 20, 2026, (2-1) v Pamba Jiji, Agosti 23, 2026 na (2-0) v Namungo FC, Septemba 7, 2026, ikiwa ni mwendelezo mzuri kwao.
Mechi za nyumbani zinaipa nguvu Azam FC, tofauti na rekodi za ugenini, ambapo imetoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Polisi Tanzania, Agosti 15, 2026, (2-2) v Geita Gold, Agosti 28, 2026 na ushindi wa (2-0), v Kagera Sugar, Agosti 31, 2026.
Kwa upande wa Simba iliyoshinda mechi zote tano msimu huu, mbili ni za nyumbani, ikianza kwa kuifunga Coastal Union ya jijini, Tanga kwa mabao 2-0, Agosti 27, 2026, kisha baada ya hapo ikaichapa pia Geita Gold mabao 2-0, Agosti 31, 2026.
Katika mechi za ugenini, Simba imecheza tatu na kushinda zote, ikiichapa Kagera Sugar mabao 2-0, Agosti 16, 2026, (2-1) v Pamba Jiji, Agosti 19, 2026, kisha ikaichapa Singida Black Stars 2-1, Agosti 22, 2026 na kuendeleza rekodi ya kuvutia.
Miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa kwa Azam FC ni watatu hadi sasa kutokana na mchango wao ndani ya kikosi hicho, ambao ni Abdul Suleiman ‘Sopu’, Idd Seleman ‘Nado’ na Hassan Mubiru, ambao wote kiujumla wamehusika na mabao tisa kati ya 11.
Katika mabao 11, yaliyofungwa na Azam FC, Sopu amefunga mabao manne, wakati kwa upande wa Idd Seleman ‘Nado’, amefunga moja na kuasisti moja, huku Mganda Hassan Mubiru akihusika na mabao matatu, baada ya kufunga moja na kuasisti mawili.
Kwa upande wa Simba, moja ya nyota hatari na wa kuchungwa leo, ni Libasse Gueye, ambaye hadi sasa amehusika kwenye mabao sita kati ya tisa yaliyofungwa na timu hiyo msimu huu, baada ya kufunga moja na kuchangia matano kwa maana ya kuasisti.
Kiwango cha Libasse Gueye, ndicho kikamfanya kuchaguliwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa Agosti na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), akiwashinda Maxi Mpia Nzengeli wa Yanga na Oscar Mwajanga wa Mbeya City alioingia nao fainali.
Mbali na Libasse, mwingine ni Clatous Chama aliyefunga mabao matatu ya Ligi Kuu, huku akifunga pia mawili katika ushindi wa mabao 6-1, dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi, kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 13, 2026.
Licha ya makocha wa timu zote mbili kufanya mabadiliko ya mara kwa mara, ila kikosi cha Azam FC kinachoweza kuanza leo ni Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Henri Stanic na Twalibu Nuru wataounda safu ya kujilinda kikosini humo.
Kwa eneo la viungo, huenda likaongozwa na mkongwe, Himid Mao Mkami atakayeshirikiana na Yahya Zayd na Feisal Salum ‘Fei Toto’, huku Gibril Sillah, Abdul Suleiman ‘Sopu’ na Idd Seleman ‘Nado’ wakitegemewa kwenye kutengeneza mashambulizi.
Kwa upande wa Simba, huenda kikosi kikaongozwa na Djibrilla Kassali, Nathaniel Chilambo, Anthony Mligo, Ismael Olivier Toure na Rushine De Reuck, watakaounda safu ya kujilinda ya kikosi hicho inayofundishwa na Kocha Mkuu, Steve Barker.
Katika eneo la kiungo huenda tukamshuhudia Yusuph Kagoma na Neo Maema, huku Libasse Gueye, Elie Mpanzu, Clatous Chama na Alain Anicet Oura wakitegemewa kuongoza mashambulizi, kutokana na viwango vyao walivyovionyesha kwenye mechi zilizopita.
Akizungumza jijini, Dar es Salaam, Kocha Mkuu wa Azam FC, Mkongomani Florent Ibenge amesema licha ya ugumu wa mechi hiyo ila wamejipanga kuhakikisha wanapata matokeo mazuri nyumbani, ili kujitengeneza nafasi nzuri ya ushindani huko mbeleni.
“Tunakutana na timu nzuri iliyotoka kufanya vizuri katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, haitokuwa rahisi kutokana na ushindani uliopo msimu huu, hivyo, tupo tayari kwa changamoto hiyo mpya mbele yetu,” amesema Ibenge.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema ushindi wa mabao 6-1, walioupata dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi, kwenye hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, umewapa morali zaidi, licha ya ushindani watakaokutana nao.
“Azam FC ni timu nzuri na imekuwa na matokeo mazuri pia hasa kwa mechi ilizocheza nyumbani, tunahitaji kutoa kilichokuwa bora zaidi kwa mashabiki zetu kutokana na matarajio yao kwetu, kabla ya kupisha mapumziko haya ya FIFA,” amesema Barker.