Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mzizima Dabi yenye sura mbili

MZIZIMA Pict

Muktasari:

  • Pambano hilo limebeba historia ndefu ya ushindani baina ya timu hizo ambazo mara ya mwisho zilikutana Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Julai 4, 2026 na Simba kushinda bao 1-0.

MZIZIMA Dabi inarudi tena leo Jumatano, wakati Azam itakapokuwa mwenyeji wa Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ukiwakutanisha wawili hao waliomaliza nafasi ya pili na tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Pambano hilo limebeba historia ndefu ya ushindani baina ya timu hizo ambazo mara ya mwisho zilikutana Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Julai 4, 2026 na Simba kushinda bao 1-0.

Huu utakuwa mchezo wa kwanza wa ligi kwa timu hizo kukutana msimu huu, lakini historia ya tangu zilipoanza kukutana kwenye Ligi Kuu Bara mwaka 2008 inaonyesha kuwa hakuna upande unaoweza kuingia uwanjani ukiwa na uhakika wa matokeo. Kuna sura mbili za Mzizima Dabi tunakwenda kushuhudia leo.

Kwa upande mmoja, Simba inaingia katika dabi hiyo ikiwa na mwanzo mkali wa msimu baada ya kushinda mechi zote tano za ligi ilizocheza. Kwa upande mwingine, Azam inaingia ikiwa na rekodi nzuri ya kutopoteza nyumbani kwa muda mrefu, jambo linaloongeza uzito wa mchezo huo.

Historia ya mechi 36 za ligi kati ya timu hizo inaipa Simba faida kubwa kwa jumla, kwani imeshinda mechi 15, Azam imeshinda saba, huku mechi 14 zikimalizika kwa sare. Simba imefunga mabao 48 dhidi ya 33 ya Azam, ikiwa ni tofauti ya mabao 15.

Kwa lugha nyingine, katika historia hiyo, Simba imeshinda zaidi ya mara mbili ya Azam, lakini idadi kubwa ya sare pia inaonyesha kwamba Mzizima Dabi si mchezo ambao upande mmoja huwa unatawala kila wakati.


KISA 01

SIMBA INAONGOZA HISTORIA

Tangu msimu wa 2008-2009, Simba na Azam zimekutana mara 36 katika Ligi Kuu Bara. Katika mechi hizo, Simba imeshinda 15, sare 14 na Azam ikiondoka na ushindi mara saba.

Hiyo inaifanya Simba kuwa na asilimia kubwa zaidi ya ushindi katika historia ya Mzima, lakini pia kuna jambo moja muhimu, karibu nusu ya mechi zote 36 zimekwisha kwa sare.

Mechi 14 kati ya 36 zimekwisha bila mshindi, sawa na karibu asilimia 39 ya kukutana kwao.

Hizi ni takwimu zinazopaswa kupewa uzito na makocha pamoja na wachezaji kwa sababu inaonyesha kwamba tofauti ya nguvu kwenye karatasi si lazima iwe sawa na kinachotokea ndani ya dakika 90.

Katika baadhi ya vipindi, timu hizo zimekuwa zikishindana kwa ukaribu mkubwa kiasi kwamba hakuna iliyoweza kupata bao la ushindi.


MECHI 14 ZA SARE

Sare imekuwa sehemu kubwa ya historia ya Mzizima Dabi.

Katika mechi 36, zilizokwisha kwa sare ni 14, huku matokeo hayo yakihusisha aina mbalimbali za mabao.

Kati ya sare hizo, tano zimekuwa za 0-0, maana yake hakuna timu iliyoweza kufungua lango la mwenzake.

Sare hizo za bila bao zilitokea katika misimu ya 2011-2012, 2015-2016, 2017-2018, 2018-2019 na 2025-2026.

Hivyo, mechi tano kati ya 36, sawa na karibu asilimia 14 ya kukutana kwao, zimekwisha bila bao.

Sare nyingine zimekuwa na mabao, ikiwamo 1-1 na 2-2, hakuna sare yenye mabao mengi zaidi ya hapo.

Sare kubwa zaidi zilizowahi kutokea katika orodha hiyo ni 2-2, zilizotokea katika misimu ya 2012-2013, 2015-2016, 2020-2021 na 2024-2025.


IBENG 05

MECHI ZISIZOKUWA NA BAO

Iwapo mchezo wa leo utaisha 0-0, hautakuwa jambo jipya katika historia ya Mzizima Dabi.

Takwimu zinaonyesha kuwa timu hizo zimekutana mara tano na kushindwa kufungana.

Mchezo wa kwanza wa aina hiyo ulikuwa Septemba 11, 2011, Azam ilipokuwa mwenyeji. Miaka minne baadaye, Desemba 25, 2015, zilikutana tena katika mchezo uliomalizika kwa matokeo hayo. Hali hiyo ilijirudia Septemba 9, 2017, kisha Mei 13, 2019, Simba ikiwa mwenyeji.

Mchezo wa mwisho kati ya hiyo mitano ulikuwa Aprili 5, 2026, wakati Azam ilipokuwa mwenyeji.

Hivyo, katika mechi zao za karibuni kabisa, Azam na Simba tayari zilionyesha namna dabi hii inavyoweza kuwa ngumu kwa washambuliaji kutikisa nyavu.


IBENG 04

MABAO MATANO NDANI YA DAKIKA 90

Ingawa zipo mechi tano zilizomalizika bila bao, historia hiyo pia inaonyesha kuwa Mzizima Dabi inaweza kubadilika na kuwa mchezo wa mabao.

Mechi yenye mabao mengi zaidi katika historia yao ni iliyozaa mabao yalifika matano. Cha kuvutia zaidi ni kwamba mechi hizo mbili zote ziliishia kwa matokeo ya 3-2.

Mchezo wa kwanza ulikuwa Januari 23, 2011, wakati Simba ikiwa mwenyeji ilipoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Azam. Hayo yalikuwa matokeo makubwa kwa Azam katika historia ya dabi hiyo.

Mchezo mwingine wenye mabao matano ulikuwa Machi 4, 2020, Azam ikiwa mwenyeji lakini ikapoteza kwa mabao 3-2 dhidi ya Simba.

Katika mechi mbili zilizowahi kuwa na mabao mengi zaidi, jumla ya mabao 10 yalifungwa, huku kila timu ikifunga matano.

Hii inaonyesha sura mbili tofauti za dabi hiyo, kuna nyakati ambazo mabeki na makipa hutawala mchezo na kuufanya uishie 0-0, lakini pia kuna nyakati ambapo mashambulizi huzaa mabao ya kutosha.


KISA 02

SIMBA NA USHINDI MKUBWA

Katika historia ya mechi hizo 36, ushindi mkubwa zaidi wa Simba dhidi ya Azam ni 3-0. Simba imepata ushindi huo mara mbili.

Ushindi wa kwanza ulikuwa Machi 30, 2009, wakati Simba ilipoifunga Azam 3-0 ikiwa Azam ndiyo mwenyeji. Miaka kadhaa baadaye, Mei 9, 2024, Simba ilirudia ushindi huo huo wa 3-0, pia Azam ilikuwa mwenyeji.

Hivyo, mara mbili Simba imeweza kumaliza mchezo dhidi ya Azam kwa tofauti ya mabao matatu bila yenyewe kuruhusu bao.


AZAM NA USHINDI WAKE MKUBWA

Kwa upande wa Azam, ushindi wake mkubwa zaidi dhidi ya Simba katika rekodi hiyo ni 2-0. Azam imepata ushindi huo mara mbili.

Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 4, 2008, katika mechi ya kwanza kukutana kwao, Azam iliposhinda 2-0 ikiwa ugenini dhidi ya Simba. Mara ya pili ilikuwa Desemba 7, 2025, Simba ilipokuwa mwenyeji lakini Azam ikashinda tena kwa mabao 2-0.

Hivyo, Azam imewahi kuifunga Simba kwa tofauti ya mabao mawili bila kuruhusu bao, lakini haijawahi kupata ushindi wa tofauti ya mabao matatu katika mechi hizo 36.

Hii ni tofauti muhimu katika historia ya dabi hiyo, kwani Simba ina ushindi mkubwa zaidi wa 3-0, wakati Azam rekodi yake bora ni 2-0.


IBENG 03

AZAM IKIWA NYUMBANI

Sehemu nyingine muhimu ya mchezo wa leo ni rekodi ya Azam inapokuwa mwenyeji.

Katika mechi zao 36, Azam imeishinda Simba mara mbili tu ikiwa mwenyeji. Ushindi wa kwanza ulikuwa Oktoba 28, 2013, Azam ilipoifunga Simba 2-1. Ushindi wa pili ulikuwa Oktoba 27, 2022, Azam iliposhinda 1-0.

Hiyo ina maana kwamba katika mechi 18 ambazo Azam imekuwa mwenyeji dhidi ya Simba, imeshinda mbili pekee.

Hizi ni takwimu zinazoipa Simba sababu ya kujiamini inapokwenda Azam Complex, lakini si takwimu zinazoweza kuamua mchezo wa leo peke yake.

Sababu ni kwamba Azam imekuwa na uwezo wa kupata sare nyumbani dhidi ya Simba, huku baadhi ya mechi zikiwa ngumu sana kwa wageni.

Changamoto ya Azam leo si kuvunja tu ubabe wa Simba katika historia ya jumla, bali pia kuboresha rekodi yake yenyewe inapokuwa mwenyeji.


UBABE WA SIMBA UGENINI

Kinyume chake, Simba imeonyesha uwezo mkubwa zaidi inapocheza ugenini dhidi ya Azam.

Katika mechi 18 ambazo Azam imekuwa mwenyeji, Simba imeshinda mara nane.

Ushindi huo wa mara nane ni mara nne ya ushindi ambao Azam imeupata dhidi ya Simba ikiwa mwenyeji. Hizi ndiyo takwimu zinazofanya mchezo wa leo kuwa na mvuto mkubwa.

Simba haitaingia Azam Complex kama timu inayokwenda kujilinda kwa sababu tu iko ugenini, historia inaonyesha imewahi kuwa mgeni na mara kadhaa kuondoka na pointi zote tatu.

Miongoni mwa ushindi wake wa kuvutia zaidi ugenini ni ule wa 3-0 mwaka 2009, 3-1 mwaka 2019, 3-2 mwaka 2020 na 3-0 mwaka 2024.

Pia Simba ilishinda 2-0 mwaka 2024 na 2-0 mwaka 2025 katika mechi zilizochezwa Azam ikiwa mwenyeji kwa mujibu wa orodha iliyotolewa.


IBENG 02

MZIZIMA DABI ILIYOPITA

Msimu uliopita pia ulikuwa na sura mbili tofauti. Desemba 7, 2025, Azam ilienda ugenini na kushinda kwa mabao 2-0, lakini Aprili 5, 2026, timu hizo zilipokutana tena Azam Complex, hazikufungana na mchezo ukaisha 0-0.

Matokeo hayo mawili ya msimu mmoja yanaonyesha jinsi ambavyo mchezo huu unaweza kubadilika kutoka ushindi hadi suluhu.

Azam inaweza kutumia ushindi wa 2-0 kama sehemu ya kujiamini, wakati Simba inaweza kutumia kumbukumbu ya sare ya 0-0 na rekodi yake ya jumla kama sababu ya kuamini kuwa inaweza kupata matokeo.

Pia Simba inaweza kuingia na nguvu ya kuichapa Azam katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, huku Azam ikihitaji kulipa kisasi.


SIMBA IMEANZA NA MOTO

Tofauti nyingine ya mchezo wa leo ni namna timu hizo zilivyoanza msimu huu. Simba imeanza ligi kwa nguvu kubwa ikiwa imeshinda mechi zote tano ilizocheza. Hiyo inaipa alama muhimu pamoja na kujiamini kabla ya kuingia katika dabi.

Azam inahitaji kutumia nguvu ya kucheza nyumbani na rekodi yake ya kutopoteza muda mrefu katika uwanja wake.

Kwa mujibu wa takwimu, Azam haijapoteza nyumbani tangu ilipofungwa 2-1 na Yanga Aprili 10, 2025.

Baada ya kipigo hicho, imecheza mechi 20 za nyumbani bila kupoteza, ikishinda 14 na kutoka sare tatu dhidi ya Simba, Yanga na Fountain Gate, zote zikiisha 0-0. Hii inaonyesha kuwa Azam Complex imekuwa eneo ambalo wapinzani wamekuwa wakihitaji kufanya kazi kubwa kupata ushindi.

Hivyo, mchezo wa leo unakutana na rekodi mbili zinazovutia, Simba ikiwa na ushindi wa asilimia 100 katika mechi zake tano za mwanzo wa ligi, huku Azam ikiwa na ngome ya nyumbani ambayo imekuwa ngumu kuvunjwa kwa muda mrefu.


KISA 03

TAKWIMU ZINAIPA SIMBA FAIDA, LAKINI...

Ukiangalia historia yote, Simba ndiyo yenye sababu nyingi zaidi za kujiamini.

Ina ushindi 15 dhidi ya saba wa Azam, imefunga mabao 48 dhidi ya 33 na imeweza kushinda mara nane ugenini dhidi ya Azam, wakati wenyeji hao wameshinda mara mbili tu nyumbani.

Lakini kuna takwimu nyingine inayoweza kuleta tahadhari kwa Simba, nayo ni sare 14.

Katika michezo 14 iliyomalizika kwa sare, tano haikuwa na bao ukiwemo wa mwisho kukutana kwao kwenye ligi. Hivyo, licha ya Simba kuwa na historia nzuri zaidi, hakuna msingi wa kusema mchezo wa leo utakuwa rahisi kwao.

Azam inatambia silaha ya kucheza nyumbani muda mrefu bila ya kupoteza, tangu Aprili 2025, lakini inapokutana na Simba, imepata ushindi mchache zaidi ambao ni mara mbili.

Simba yenyewe silaha kubwa ni ubora wa matokeo yake katika historia ya dabi hiyo, uwezo wa kushinda ugenini na mwanzo wake wa msimu ambao umejaa ushindi wa asilimia 100.