Tshabalala atoa kauli ya ubingwa Yanga
Muktasari:
- Tshabalala amesema kwamba, hatua ya timu hiyo kupunguza tofauti ya pointi kati yao na Simba kubaki mbili kutoka tano za awali, ni jambo lisilokubalika na kwamba wanatakiwa kuamka haraka.
BEKI wa Yanga, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ amevunja ukimya katika ya timu hiyo, akitamka maneno mazito yatakayowaamsha wachezaji wenzake ndani ya kikosi hicho, akitaka washtuke haraka kama wanautaka ubingwa.
Tshabalala amesema kwamba, hatua ya timu hiyo kupunguza tofauti ya pointi kati yao na Simba kubaki mbili kutoka tano za awali, ni jambo lisilokubalika na kwamba wanatakiwa kuamka haraka.
Beki huyo wa kushoto ambaye anamiliki mabao matatu Ligi Kuu Bara msimu huu akiwa anaitumikia Yanga akitokea Simba, amesema licha ya Yanga kuongoza ligi lakini wanatakiwa kuamka haraka kuepuka kufanya makosa ambayo yatazidi kuwapa presha wakati wanapambana kutetea ubingwa wa ligi hiyo zikibaki mechi saba.
“Nikweli tulikuwa tunaongoza ligi kwa tofauti ya pointi tano lakini sasa zimepungua na kubaki mbili baada ya kupoteza mechi dhidi ya Dodoma Jiji, hii sio hatua nzuri kwetu,” amesema Tshabalala.
Ameongeza: “Kitu muhimu ni sisi wachezaji kuamka haraka kama tunataka kubeba ubingwa, hatutakiwi kufanya makosa hayo tena, tunatakiwa kupambana kila mechi tusiangushe pointi na hili linawezekana kutokana na ubora wetu.”
Yanga kesho Ijumaa itakuwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ikisaka pointi tatu, itakapoikaribisha Singida Black Stars, huku Simba iliyo nafasi ya pili, leo jioni itakuwa uwanja wa ugenini kupambana dhidi ya Coastal Union.
Endapo Simba ikishinda leo dhidi ya Coastal Union, itaongoza ligi kwa tofauti ya pointi moja ikifikisha 55, ikiishusha Yanga yenye 54.