Kitawaka! TP Mazembe, Esperance, Al Ahly
Muktasari:
- Mabingwa mara nne wa Afrika, Esperance ya Tunisia, ni miongoni mwa timu zinazokabiliwa na mtihani mgumu baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Swehly SC ya Libya. Timu hizo zitakutana tena leo Jumamosi, huku Esperance ikihitaji ushindi wa kugeuza matokeo na kuendelea kuwania nafasi ya hatua ya makundi.
CAIRO, MISRI: Vigogo wa soka barani Afrika wanakabiliwa na presha kubwa katika mechi za marudiano za raundi ya pili ya awali za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho msimu wa 2026/27, huku baadhi yao wakihitaji ushindi ili kuepuka kuaga mashindano hayo mapema.
Mabingwa mara nne wa Afrika, Esperance ya Tunisia, ni miongoni mwa timu zinazokabiliwa na mtihani mgumu baada ya kupoteza mchezo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Swehly SC ya Libya. Timu hizo zitakutana tena leo Jumamosi, huku Esperance ikihitaji ushindi wa kugeuza matokeo na kuendelea kuwania nafasi ya hatua ya makundi.
Nayo TP Mazembe ya DR Congo, iliyotwaa ubingwa wa Afrika mara tano, italazimika kufanya kazi kubwa itakapokutana na Club Africain ya Tunisia Jumapili. Timu hizo zilitoka sare ya mabao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliopigwa Lubumbashi, hivyo bado kila upande una nafasi ya kufuzu.
MC Alger ya Algeria na Petro Atlético ya Angola pia ni miongoni mwa vigogo vinavyotajwa kukabiliwa na kazi ya kurekebisha matokeo ya mechi za kwanza ili kusonga mbele katika mashindano hayo.
Wakati baadhi ya timu zikipambana kuokoa kampeni zao, nyingine zinaingia kwenye marudiano zikiwa na faida ya matokeo mazuri ya mechi za kwanza.
RS Berkane ya Morocco inaongoza kwa mabao 2-0 dhidi ya Star Sport Academy ya Sierra Leone kabla ya mchezo wa marudiano, huku Al Hilal ya Sudan ikilenga kulinda faida kama hiyo dhidi ya Sidama Bunna ya Ethiopia Jumapili.
Colombe Sportive ya Cameroon nayo iko katika nafasi nzuri baada ya kuichapa Teungueth FC ya Senegal mabao 2-0 ugenini, matokeo yanayoipa matumaini makubwa ya kufuzu hatua ya makundi.
Kwa upande wa Misri, Pyramids FC na Zamalek zitakuwa nyumbani leo Jumamosi zikilenga kukamilisha kazi baada ya kupata ushindi wa ugenini wa bao 1-0 kila moja dhidi ya El Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini na APR FC ya Rwanda.
ASEC Mimosas ya Ivory Coast itakuwa na kibarua cha kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani dhidi ya MAS de Fès ya Morocco baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 1-1 katika mchezo wa kwanza.
Nayo Horoya AC ya Guinea itasafiri kwenda Sudan kukutana na Al Merriekh ikiwa na faida ya bao 1-0, huku FC Nouadhibou ya Mauritania ikihitaji kugeuza matokeo baada ya kufungwa mabao 2-1 na FC San Pedro ya Ivory Coast katika mchezo wa kwanza.
Timu 15 zitakazofuzu kupitia mechi hizo za marudiano zitajiunga na Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, itakayoshirikisha timu 16 msimu wa 2026/27.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika, jumla ya mechi 14 za marudiano za raundi ya pili ya awali zimepangwa kuchezwa kuanzia Ijumaa hadi Jumapili, huku USM Alger ya Algeria ikiwa tayari imefuzu hatua ya makundi baada ya wapinzani wake, Panthers FC ya Equatorial Guinea, kujiondoa kwenye mashindano.
Hata hivyo, mchezo kati ya CR Belouizdad ya Algeria na AS Douanes ya Mauritania bado unasubiriwa, huku ratiba yake ikitarajiwa kuthibitishwa.
Baadhi ya timu zinaingia katika michezo hiyo zikiwa na kazi kubwa ya kufanya ili kuepuka kuondolewa, huku nyingine zikilenga kulinda faida iliyopatikana katika mechi za kwanza na kutimiza azma ya kufuzu hatua ya makundi.
Nchini Tunisia, CS Sfaxien, mabingwa mara tatu wa Kombe la Shirikisho, itakuwa na kibarua cha kuiondoa Académie de Football Amadou Diallo ya Ivory Coast baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo wa kwanza uliochezwa Abidjan.
AS FAR ya Morocco nayo italazimika kutafuta ushindi itakapokuwa mwenyeji wa CO Korhogo ya Ivory Coast Jumapili, baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mchezo wa kwanza.
Al Ahly ya Misri itakuwa mwenyeji wa Kitara FC ya Uganda Jumapili ikiwa na faida ya ushindi wa mabao 2-1 iliyopata katika mchezo wa kwanza.
Wakati baadhi ya michezo ikitarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, timu nyingine zinaingia kwenye marudiano zikiwa na faida kubwa kutokana na ushindi wa ugenini.
Al Ahly Tripoli ya Libya ilipata ushindi wa mabao 4-0 ugenini, matokeo yanayoipa nafasi nzuri ya kufuzu. AS Maniema Union ya DR Congo nayo ilijiweka katika nafasi nzuri baada ya kushinda mabao 4-1 ugenini.
Black Bulls ya Msumbiji itakuwa na jukumu la kukamilisha kazi dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 ugenini katika mchezo wa kwanza.
AS Real Bamako ya Mali nayo imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele baada ya kuichapa ES Zarzis ya Tunisia mabao 3-1.
Kwa Tanzania, macho yataelekezwa katika mchezo wa Jumapili kati ya Singida Black Stars na Tusker FC ya Kenya. Singida italazimika kutumia vyema mchezo huo wa marudiano ili kufanikisha azma yake ya kutinga hatua ya makundi.
Kwa ujumla, mechi hizo zitapima uwezo wa timu katika kulinda matokeo, kutumia nafasi za kufunga na kukabiliana na presha ya ushindani wa soka la kimataifa.
Timu zitakazofuzu zitaungana na USM Alger katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2026/27, ambako vita ya kuwania ubingwa wa mashindano hayo itaendelea.
RATIBA
Ligi ya Mabingwa Jumamosi, Oktoba 24, 2026
Esperance de Tunis vs Swehly SC
Al Merriekh vs Horoya AC
Pyramids FC vs El Merriekh Bentiu
Zamalek SC vs APR FC
RS Berkane vs Star Sport Academy
Kesho, Jumapili
Simba SC vs 15 de Agosto
Colombe Sportive vs Teungueth FC
Al Hilal Omdurman vs Sidama Bunna
ASEC Mimosas vs MAS de Fes
Club Africain vs TP Mazembe
FC Nouadhibou vs FC San Pedro
Kombe la Shirikisho leo, Jumamosi
Azam FC vs ZED FC
AS Real Bamako vs ES Zarzis
Al Ahly Tripoli vs Welwalo Adigrat
Black Bulls vs Rayon Sports
CS Sfaxien vs Academie de Amadou
Kesho, Jumapili
AS Maniema Union vs Kabuscorp
AS Port Louis 2000 vs Durban City
ASKO de Kara vs FC Diarra
Al Ahly FC vs Kitara FC
Singida Black Stars vs Tusker FC
AS FAR vs CO Korhogo