TRA United yamnasa Manyama
Muktasari:
- Katika maboresho hayo, TRA tayari imemvuta aliyekuwa beki wa Azam FC, Edward Manyama akiwa mchezaji huru.
TRA United imekamilisha hesabu za kuvuta mastaa wawili ili kuongeza nguvu eneo la ulinzi na ushambuliaji, ikiwa ni za kujenga kikosi chenye wachezaji wazoefu kwa ajili ya msimu ujao wa 2026-2027.
Katika maboresho hayo, TRA tayari imemvuta aliyekuwa beki wa Azam FC, Edward Manyama akiwa mchezaji huru.
Si hivyo tu, TRA imeweza kumrudisha mmoja wa washambuliaji wake bora ambao waliacha rekodi nzuri wakati kikosi hicho kikiitwa Tabora United, Emmanuel Mwanengo kabla ya kutua Yanga msimu uliopita.
Mwanaspoti linafahamu kuwa, Yanga imemtoa Mwanengo kwa mkopo baada ya uwezekano wa yeye kupata namba ndani ya kikosi hicho kuzidi kuwa mgumu kutokana na watu wanaocheza eneo hilo kuwa tishio zaidi yake.
Taarifa za ndani zilisema uongozi unaamini Manyama atasaidia kuongeza ushindani kwenye kikosi kutokana na uzoefu wake wa kucheza katika timu mbalimbali za ligi kuu ikiwemo Azam FC.
“Ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na anafahamu mazingira ya ligi. Mazungumzo yanaendelea vizuri na tuna matumaini yatakamilika kwa mafanikio,” kilisema chanzo hicho.
“Mwanengo ni mmoja wa wachezaji wazuri, kutua kwake kwa mkopo kwanza kunampa faida kama mchezaji kwani naamini atapata nafasi ya kucheza kutokana uwezo aliokuwa nao.”
Manyama amewahi kuichezea JKT Ruvu Stars msimu wa 2013-2014 na baadaye alirejea tena 2015-2018, akatua Ruvu Shooting msimu mmoja 2018-2019, Namungo 2019-2021, kisha Azam FC 2021-2026.