Timuatimua ya makocha
Muktasari:
MSIMU uliopita wa Ligi Kuu Bara hadi kufikia tarehe kama ya leo, tayari makocha nane walikuwa wameachana na timu walizokuwa wakizifundisha.
MSIMU uliopita wa Ligi Kuu Bara hadi kufikia tarehe kama ya leo, tayari makocha nane walikuwa wameachana na timu walizokuwa wakizifundisha.
Kila kocha aliondoka kwa sababu zake huku wengi wao walikuwa wakitimuliwa kwa sababu ya mwenendo mbovu wa timu kwa kupata matokeo mabaya huku wengine wakiondoka kwa kutofautiana na mabosi wake.
Msimu huu hadi Desemba Mosi, timu sita zilikuwa zimeachana na makocha nao kwa sababu hizo hizo kama zilivyo msimu uliopita.
Kuna mambo mengi yanachangia hadi kutokea timuatimua hizo hasa kutokana na mabadiliko ya kanuni ambayo timu zinapungua kwenye ligi hivyo kuwafanya viongozi kushindwa kuwa wavumilivu na matokeo hayo.
Mwanaspoti kama mdau mkubwa wa michezo nchini linakupa makocha ambao hadi sasa wametimuliwa na wengine kuachana na timu zao kwa sababu mbalimbali.
Zlatko Krmpotic -Yanga
Siku 35 tu zimemtosha kuishi Bongo. Kocha Zlatko Krmpotic tayari aliondoka nchini akirudi kwao Yugoslavia baada ya kutimuliwa na mabosi wa klabu hiyo.
Wengi waliona kama ni uamuzi wa kushangaza lakini kwa hali ya mambo na maisha ya kocha huyo kuondolewa lilikuwa ni suala la muda tu hasa baada ya kushinda 3-0 mchezo dhidi ya Coastal Union.
Alisaini mkataba wa miaka miwili kuiongoza Yanga, Agosti 29 lakini Oktoba 3, baada ya mchezo wa Coastal Union pale Uwanja wa Mkapa akafutwa kazi na kuwa kocha wa kwanza kutimuliwa msimu huu.
Maka Mwalwisi - Ihefu SC
Aliiwezesha timu hiyo kupanda Ligi Kuu msimu huu, baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi A Ligi Daraja la Kwanza (FDL) sawa na Dodoma Jiji FC iliyoongoza na kupanda moja kwa moja.
Ihefu ilipenya kupitia hatua ya mtoano kwa kuichapa Transit Camp hatua ya awali kisha kuisambaratisha Mbao FC hatua ya mwisho.
Mwalwisi alichukua kikosi hicho mzunguko wa pili wa FDL akiwa anatoka kwenye kikosi cha Mbeya Kwanza, akipokea mikoba ya Salhina Mjengwa aliyetimuliwa.
Oktoba 6, 2020 ilikuwa siku yake ya mwisho ndani ya vijana hao wa Mbogo Mji na sasa nafasi yake ipo chini ya Zubery Katwila ambaye bado hana maajabu.
Zubery Katwila - Mtibwa Sugar
Oktoba 18, 2020 zilianza kuenea tetesi za mkongwe huyo kuachana na Mtibwa timu ambayo alidumu nayo kwa muda mrefu tangu akiwa mchezaji wa kikosi hicho.
Baada ya saa kadhaa uongozi wa wakata miwa walithibitisha kuachana na Katwila japo hakuna pande iliyoweka wazi kama Mtibwa ndio iliyoachana na kocha au Katwila ndiye aliyeamua kuikacha Mtibwa.
Hata hivyo tetesi za chini ya kapeti zilieleza mabosi wa timu hiyo ilikuwa ikimvutia kasi Katwila na kumtimu kutokana na matokeo mabaya.
Kwa sasa Mtibwa Sugar inanolewa na Vincet Barnabas aliyekuwa kocha wa msaidizi kwa muda mrefu baada ya kufanya vizuri akiwa na timu ya vijana ya timu hiyo.
Amr Said - Mbeya City
Ukipenda unaweza kumuita ‘Stam’ nyota wa zamani wa Simba hali ndani ya kikosi cha Mbeya City ilikuwa mbaya kuanzia msimu uliopita ambapo iliponea kwenye mechi za mchujo na msimu huu imeanza vibaya.
Oktoba 20 uongozi wa Mbeya City ulimfungashia virago ‘Stam’ ikiwa baada ya timu hiyo kucheza michezo saba ikiwa mkiani huku ikivuna alama moja baada ya suluhu na Prisons.
Siku ambayo inamtimua kocha huyo ilitoka kuchezea kichapo cha mabao 2-1 mbele ya Mwadui, nafasi yake ilichukuliwa na Mathias Wandiba aliyekuwa msaidizi wake.
Hitimana Thierry - Namungo FC
Amedumu na timu hiyo tangu ikiwa FDL na alipoisaidia kupanda Ligi Kuu baada ya uongozi wa Namungo kumtimua Fulgence Novatus aliyetimkia Gwambiana FC.
Hitimana alitua hapo akitoka kutimuliwa Biashara United, lakini akafanikiwa kufanya maajabu na Namungo sio tu kuipandisha Ligi Kuu bali kuisaidia kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na kuiwezesha kucheza michuano ya Caf msimu huu.
Mwanzo wa msimu huu, Hitimana alikuwa akiwatupia lawama mabaosi wake kwa kufanya usajili ambao ulikuwa sio pendekezo lake ikiwa pamoja na kumuacha mfungaji bora kwa misimu yote miwili wa timu hiyo, Reliants Lusajo aliyesajioliwa na KMC.
Novemba ikiwa siku yake ya mwisho kuwa na vijana hao kutoka Ruangwa na sasa timu ipo chini ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye ameiongoza kwenye michezo miwili.
Morocco ameiongoza Namungo kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga na kutoka nao sare ya bao 1-1 kisha akaiongoza kwenye mchezo wa Kombe la Shirikishoa barani Afrika dhidi ya Al Rabit ya Sudan Kusin na kuicha mabao 3-0 Uwanja wa Chamazi.
Aristica Cioaba - Azam FC
Ndiye kocha aliyetufungia mwezi Novemba, siku moja baada ya Azam FC kulala bao 1-0 dhidi ya Yanga Uwanja wa Chamazi, uongozi haukuvumilia maumivu hayo.
Novemba 26, Cioaba pamoja na kocha wa viungo, Costel Birsan walitimuliwa nafasi yake ilichukuliwa na Bahati Vivier ambaye awali alikuwa kocha wa vijana lakini kutimuliwa kwa Idd Nassoro ‘Cheche’ kulimpandisha cheo na sasa anashika usukani.
Cioaba alitua kwenye viunga hivyo kwa mara ya pili Oktoba mwaka jana akichukua mikoba ya Etienne Ndayiragije aliyepata kazi ya kukinoa kikosi cha Taifa Stars.
Hadi anaachana na Azam, Cioaba aliiongoza kwenye michezo 50, huku akishinda michezo 28, sare michezo 11 na kupoteza michezo 11 na kuiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya tatu ikiwa na alama 70.
Cioaba anaondoka Azam ikiwa nafasi ya pili baada ya kuoingoza michezo 12, ikishinda michezo nane, ikipoteza mitatu na sare ikiambulia michezo moja na kuvuna alama 25.
MSIMU ULIOPITA
Kiti cha ukocha sio cha mchezo mchezo, wengine husema eti kocha anaajiliwa ili atimuliwe. Msimu uliopita tarehe kama ya leo makocha nane vibarua vyao vilikuwa vimeota mbawa.
Msimu uliopita mambo yalikua balaa, Athuman Bilali ‘Bilo’ alianza kufunguliwa mlango wa kutoka akiwa na kikosi cha Biashara United na sasa ndio kocha msaidizi wa Gwambina FC.
Fred Felix ‘Minziro’ aliachana na Singida United nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhani Nswanzurimo, hata hivyo Minziro alitua Pamba na baadaye kupata kazi Alliance na huko maisha hayakuwa mazuri na baadaye kujiunga na Mbao ambayo alishuka nayo daraja.
Biashara United kabla ya kumchukua, Francis Baraza ilitoka kumtimua Stam, wengine waliochana na timu zao ni pamoja na Ndayiragije aliyekua Azam na kuta Taifa Stars.
Mwinyi Zahera na benchi lote la ufundi la Yanga lilifumuliwa na Charles Mkwasa alitangazwa kushika nafasi kwa wiki mbili huku uongozi ukisaka kocha mpya.
Novemba 9,2019 Jackson Mayanja alitimuliwa KMC, wakati Malale Hamsi akiachana na Ndanda, Novemba 30/112019 huku Patrick Aussems aliekuwa Simba akaacha na timu hiyo wakati mapema siku hiyo Juma Mwambusi akitangaza kuachana na Mbeya City.
Baada ya kuvuka Novemba, makocha wengine waliohama au kutimuliwa alikuwa Stam kwa mara nyingine akiachana na Ndanda FC, Sulemani Matola akitoka Polisi Tanzania na kwenda Simba Desemba 10.
Luc Eymael Kocha akichukua mikoba ya Mkwassa naye akatimuliwa, huku Haruna Harerimana akiachana na Lipuli na kwenda kuchukua nafasi ya Mayanja pale KMC lakini kabla yake alikua, Hamad Ali kwa muda Lipuli ikiwa chini ya Samwel Moja.