Tiketi za umrah kwa washindi wa marathon
Muktasari:
- Mbali na zawadi hizo, waandaaji wameandaa zawadi maalumu kwa watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwapa faraja na kuwahamasisha kushiriki.
TAASISI ya Kidundo Charity imeandaa mbio za marathon zitakazofanyika Desemba 6, 2026, kwa lengo la kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi na kujiandaa kwa ibada ya Umrah.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kidundo Charity Marathon, Khalid Iddi Haji maarufu kama Kidundo, amesema mbio hizo zitahusisha makundi ya vijana na watu wazima, huku washiriki wakitakiwa kukimbia au kutembea kulingana na kundi lao.
Amesema vijana wenye umri wa miaka 18 na kuendelea watashiriki mbio za kukimbia kilomita 10, huku watu wazima wenye umri wa miaka 45 na kuendelea wakishiriki mbio za kutembea kilomita tano.
Kidundo amesema washindi watapata zawadi zikiwemo tiketi nne kwenda kufanya ibada ya Umrah, huku washiriki wengine watakaoshinda wakipatiwa fedha za kuwasaidia kuanzisha shughuli za kujipatia kipato.
“Tunatoa zawadi hizo kuwapa hamasa vijana na wazee kujiandaa na ibada ya Umrah na kuikumbusha jamii umuhimu wa kufanya mazoezi,” amesema na kufafanua ada ya usajili kwa kila mshiriki itakuwa Sh35,000.
Katibu wa taasisi inayojihusisha na usafirishaji wa mahujaji, Abdul Maulid Haji amesema ibada ya hija inahitaji utayari wa kiafya na kimwili, jambo lililowasukuma kuanzisha mbio hizo ili kuhamasisha wananchi kuzingatia afya zao.
Amesema taasisi hizo zinalenga kuwahamasisha zaidi vijana kushiriki ibada ya Umrah na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo.
Abdul alisisitiza kuwa mbio hizo zitakuwa wazi kwa watu wa dini na makabila yote. Amesema zawadi zitakuwa za aina mbili, tiketi za Umrah na fedha, hivyo mshindi asiye Muislamu atapatiwa fedha badala ya tiketi.
Mbali na zawadi hizo, waandaaji wameandaa zawadi maalumu kwa watu wenye ulemavu kwa lengo la kuwapa faraja na kuwahamasisha kushiriki.