Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TDS, Spotlight mzigoni Dar Youth Cup

Muktasari:

  • TDS, ambayo kwa sasa ndiyo inaongoza Kundi A ikiwa na pointi tatu na ndiyo timu pekee iliyopata ushindi mabao mengi katika mechi za ufunguzi zilizopigwa wikiendi iliyopita, wiki hii itakuwa na kibarua kizito mbele ya Spotlight. Katika mechi ya kwanza ya kundi hilo, Spotlight ilitoshana nguvu kwa kutoka suluhu ya 0-0 dhidi ya West FA.

MASHINDANO ya vijana wenye umri chini ya miaka 18 ya Dar Youth Cup yanatarajiwa kuendelea leo kwenye viwanja vya Ufundi, Lugalo, huku macho na masikio ya mashabiki wengi yakiwa kwa timu ya TDS ambayo mechi yake ya kwanza ilitoa kichapo cha mabao 9-1 dhidi ya Kakakuona.

TDS, ambayo kwa sasa ndiyo inaongoza Kundi A ikiwa na pointi tatu na ndiyo timu pekee iliyopata ushindi mabao mengi katika mechi za ufunguzi zilizopigwa wikiendi iliyopita, wiki hii itakuwa na kibarua kizito mbele ya Spotlight. Katika mechi ya kwanza ya kundi hilo, Spotlight ilitoshana nguvu kwa kutoka suluhu ya 0-0 dhidi ya West FA.

Mashabiki wengi wana hamu ya kuiona TDS ambayo ni timu maalum iliyoanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika mpango wa utambuzi na uendelezaji wa vipaji kutokana na kiwango bora ilichoonyesha katika mechi ya kwanza. Mbali na kufunga mabao hayo mengi, muda mwingi wa mchezo walikuwa kwenye nusu ya uwanja ya Kakakuona.

Abiud Richard Faru, ambaye hadi sasa ndiye mchezaji pekee aliyefunga hat-trick, naye ni miongoni mwa mastaa wanaotazamiwa kuvutia kundi kubwa la mashabiki wanaofuatilia mashindano hayo. Mechi yao dhidi ya Spotlight inatarajiwa kupigwa saa 10:00 jioni, Jumapili.

Hata hivyo, ligi hiyo itaanza kurejea Jumamosi ambapo kutakuwa na mechi mbili za Kundi B, linaloongozwa na Newlife Academy yenye alama tatu, sawa na Bulls FA.

Newlife, ambayo katika mechi ya kwanza iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Magnet Academy, leo Jumamosi, saa 8:00 mchana itaumana na Brothers Jr, ambayo katika mechi yake ya kwanza ilichapwa mabao 2-0 na Bulls.

Utamu katika kundi hili unaletwa na mechi nyingine kati ya Magnet na Bulls itakayopigwa saa 10:00 jioni. Ikiwa Bulls na Newlife zitashinda mechi zao, kinara wa kundi atapatikana katika mechi ya mwisho pale Bulls na Newlife zitakapokutana.

Jumapili, mbali na mechi kati ya TDS na Spotlight ambayo itakuwa ya mwisho kwa siku hiyo, mchezo wa kwanza utakuwa kati ya Kakakuona ambayo haijaambulia alama yoyote hadi sasa dhidi ya West FA yenye pointi moja.

Mechi hii, ambayo itafungua dimba kwa raundi ya pili ya Kundi A, itatoa nafasi kubwa kwa timu itakayoshinda kupanda angalau nafasi moja kutoka pale ilipo. Hivyo, inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na umuhimu wake kwa timu zote mbili.