Tanzanite Queens kusaka muujiza mbele ya Canada leo!
Muktasari:
- Mechi hiyo itachezwa Stadion Miejski, Bielsko-Biała, kuanzia saa 12:00 jioni kwa Tanzania. Hadi sasa Brazil inaongoza Kundi B ikiwa na pointi sita, England inafuata na pointi nne, Canada ina pointi moja, wakati Tanzania iko mkiani bila pointi.
BAADA ya Timu ya taifa ya Tanzania kwa wasichana U-20, Tanzanite Queens kupoteza mechi mbili mfululizo za Kundi B la Kombe la Dunia kwa wanawake leo itakuwa na dakika 90 ngumu za jasho na damu kuamua hatma ya kufuzu hatua ya 16 bora.
Mechi hiyo itachezwa Stadion Miejski, Bielsko-Biała, kuanzia saa 12:00 jioni kwa Tanzania. Hadi sasa Brazil inaongoza Kundi B ikiwa na pointi sita, England inafuata na pointi nne, Canada ina pointi moja, wakati Tanzania iko mkiani bila pointi.
Brazil iliifunga Tanzania 4-1 kwenye mchezo wa kwanza, kabla England kuichapa 5-1 kwenye mchezo wa pili.
Hivyo Tanzanite bado ina nafasi ya kufanya vizuri na kufuzu hatua inayofuata kwani mfumo wa mashindano ya timu 24, timu mbili za juu kutoka kila kundi zinaingia moja kwa moja hatua ya 16 bora, huku nafasi nne zikibaki kwa timu bora zitakazomaliza nafasi ya tatu. Hivyo Tanzania inahitaji ushindi dhidi ya Canada, pia itahitaji matokeo ya makundi mengine na tofauti ya mabao kuangaliwa kwa umakini.
IEPUKE HAYA
Tanzanite isiruhusu wapinzani wake kupata bao la mapema kwani hiyo ni moja ya changamoto iliyoonekana kwenye mechi mbili zilizopita.
Dhidi ya Brazil, Tanzania ilianza vizuri kwa vipindi fulani lakini Brazil ilitumia ubora wake kubadili mchezo. Dhidi ya England, tatizo likawa kubwa zaidi baada ya Tanzania kuruhusu mabao mapema, jambo lililowafanya Waingereza kupata nafasi ya kuutawala mchezo.
Kwa Canada, Tanzania inahitaji dakika 15 za kwanza kuwa za nidhamu. Wanapaswa kwanza kuhakikisha safu ya ulinzi imesimama imara, viungo vinadhibiti eneo la kati na mipira inayopotea isigeuke kuwa mashambulizi ya haraka ya Canada.
Mechi mbili zilizopita zimeonyesha wazi kuwa Tanzania inapopandisha wachezaji wengi kushambulia, nafasi nyuma yao inaweza kuwa tatizo.
England ilitumia nafasi hizo kwa ufanisi mkubwa na kupata ushindi wa 5-1. Canada yenyewe ilifunga bao moja dhidi ya England na kulazimisha sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza, kabla ya Brazil kuichapa 3-0.
Hivyo, Tanzanite lazima iwe makini na mipira ya pembeni, pasi za haraka nyuma ya mabeki na mashambulizi ya kushtukiza.
Tanzania ikitaka kushinda, haiwezi kucheza kwa kukimbizana na mpira dakika zote 90.
Inahitaji kutulia viungo wanapaswa kuwa na uwezo wa kushikilia mpira, kubadilisha upande wa mashambulizi na kuwalazimisha Canada kukimbia bila mpira.
Hapo ndipo nafasi za Winifrida Gerald, Mary Siyame na wachezaji wengine wa mbele zinaweza kuwa muhimu.
Gerald tayari amefunga bao moja kwenye mashindano haya, alipopachika penalti dhidi ya Brazil, hivyo Tanzania inahitaji wachezaji wake wa mbele kutumia nafasi chache watakazopata kwa ufanisi.
Kocha mkuu wa kikosi hicho, Bakari Shime amesema “Hakuna namna ni mechi ngumu leo tunayokwenda kukutana nayo, lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri na naimani kwa timu ilivyocheza mechi zilizopita tunayo nafasi.”