Serikali yazishauri Halmashauri kujenga viwanja vya soka
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamasha la kitaifa la utamaduni litakalofanyika mkoani Morogoro. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Halmashauri nyingi zimekuwa zikikimbilia kujenga fremu za maduka kwa lengo la kupangisha na kupata mapato wakati wanaweza kujenga viwanja vya mpira ambavyo vitawafanya waweze kukusanya fedha nyingi lakini pia kuibua vipaji.
Morogoro. Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amezishauri halmashauri za miji, Manispaa na majiji kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanja vya michezo hasa soka badala ya kuwekeza kwenye kujenga fremu za maduka mara kwa mara.
Msigwa ametoa ushauri huo leo Jumapili, Agosti 23, 2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamasha la nne la kitaifa la utamaduni litalofanyika kuanzia Agosti 25 Hadi 29 mwaka huu katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Amesema halmashauri nyingi zimekuwa zikikimbilia kujenga fremu za maduka kwa lengo la kupangisha na kupata mapato wakati wanaweza kujenga viwanja vya mpira ambavyo vitawafanya waweze kukusanya fedha nyingi lakini pia kuibua vipaji.
"Viwanja vingi hapa nchini vinamilikiwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) isipokuwa zipo halmashauri ambazo tayari zimeiona fursa kwa kujenga viwanja kama Halmashauri ya Kinondoni. Hii biashara ya kujenga fremu za maduka, tuachie watu binafsi," amesema Msigwa.
Katika hatua nyingine, Msigwa amezitaka halmashauri zote hapa nchini kuacha tabia ya kubadilisha matumizi ya maeneo ya michezo na burudani na kusema kuwa maeneo hayo yametengwa kwa ajili ya kubaini na kukuza vipaji.
"Michezo ina faida nyingi. Leo hii kuna wachezaji wanalipwa mishahara mikubwa na wengine wanauzwa kwenda kucheza nje ya nchi. Na serikali kwa kutambua hilo, imeweka fedha nyingi kwenye kuboresha viwanja ili viwe na hadhi," amesema Msigwa.
Akizungumzia michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, Msigwa amesema kuwa baadhi ya watu wamekuwa na mashaka kwamba michuano hiyo haiwezi kufanyika hapa nchini, ambapo amesema maneno hayo ni ya upotoshaji.
"AFCON ipo na haijahamishwa. Tayari maandalizi ya viwanja na mazingira yote yanaendelea. Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshalipa ada ya ushiriki Dola 30 milioni (Sh80 bilioni), hivyo wananchi wakiwemo wafanyabiashara na wenye makampuni kujiandaa Kwa kutafuta fursa zitokanazo na ujio wa michuano hiyo," amesema Msigwa.
Akizungumzia tamasha hilo la utamaduni amesema lilianzishwa mwaka 2021 na madhumuni yake ni kukuza utamaduni wa Mtanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo mavazi, ngoma, chakula na tamaduni nyingine.
Wakati huo huo Msigwa ameeleza mchakato wa kupata vazi la Taifa ambapo amesema kwa sasa bado halijapatika na kumekuwa na ugumu katika kulipata kutokana na kuwepo kwa makabila zaidi ya 160 hapa nchini.
"Nchi yetu inamakabila zaidi ya 160 na kila kabila lina vazi lake. Utachukua vazi gani kulifanya liwe la Taifa? Hali kadhalika tumepata ugumu pia wa kupata mdundo wa Taifa maana kila kabila lina ngoma zake na midundo yake," amesema Msigwa.