SuperSport yaitema Gor Mahia
Wachezaji wa Dream Team wakifanya mazoezi kujiweka tayari kwa pambano la fainali ya Pamba Roho dhidi ya Massive FC litakalofanyika Uwanja wa Bomani, Likoni kesho Jumapili. PICHA NA HAMISI NGOWA
MWANDISHI WETU KITUO maarufu cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini kimesusa kurusha moja kwa moja mechi yoyote itakayohusisha klabu ya Gor Mahia kwenye Ligi Kuu Kenya. Ofisa Mtendaji Mkuu wa KPL Jack Oguda alithibitisha wiki hii kwamba kituo hicho hakitajihusisha na mechi yoyote ya Gor kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu. Hatua hiyo imefikiwa baada ya mechi mbili zilizohusisha Gor zilizorushwa 'live' mzunguko wa kwanza kuvunjika kutokana na vurugu za mashabiki. Oguda alisema uamuzi huo unaweza kubadilika endapo Gor wataandika barua kwa SuperSport na KPL kuomba radhi na kuahidi kudhibiti mashabiki wake. Mwezi uliopita mashabiki wapatao 8,000 wa Gor Mahia walifukuza kila mtu aliyekuwa mbele yao huku wakipiga mawe magari yaliyokuwa yameegeshwa sehemu za karibu ya Uwanja wa Nyayo mbali na kuvunja vifaa kadhaa vya uwanja huo. Vurugu hizo zilitokea wakati wa mechi ya nusu fainali ya Nane Bora baina ya Gor Mahia na Ulinzi ambapo mashabiki hao walidai timu yao ilinyimwa bao na penalti huku Ulinzi ikiwa mbele kwa bao 1-0.