Sultan Juma arejea Alliance Queens
Muktasari:
- Kocha huyo anarudi katika timu hiyo akipewa kibarua kizito cha kuhakikisha anaifikisha Alliance Girls inamaliza kwenye nafasi nne za juu ikiwa ni malengo ya msimu huu.
ALIYEWAHI kuwa Kocha Mkuu wa Ceasiaa Queens msimu uliopita, Sultan Juma amerejea rasmi ndani ya kikosi cha Alliance Girls baada ya kusaini mkataba wa miezi sita wa kuifundisha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake.
Kocha huyo anarudi katika timu hiyo akipewa kibarua kizito cha kuhakikisha anaifikisha Alliance Girls inamaliza kwenye nafasi nne za juu ikiwa ni malengo ya msimu huu.
"Mkataba wangu ni wa miezi sita na malengo makuu tuliyojiwekea na uongozi ni kuhakikisha tunaipigania timu na kumaliza kwenye nafasi nne za juu za msimamo wa ligi," amesema Sultan.
Urejeo wa kocha huyo unakuja wakati timu hiyo ikikabiliwa na changamoto ya kuondokewa na wachezaji wawili muhimu walioondoka kikosini, wote wakicheza eneo la golikipa.
Makipa hao ni Husna Mtunda aliyetimkia JKT Queens, pamoja na Rhobi Daudi aliyejiunga na Yanga Princess.
Akizungumzia pengo la makipa hao, Kocha Sultan amesema: "Kuna wachezaji wameondoka wawili na wote ni eneo la golikipa. Lakini tunaamini kwenye vijana waliopandishwa kwa sababu hii ndiyo sera na mpango wa timu kila msimu wa kutoa nafasi kwa vipaji vya ndani."
Kocha huyo aliyewahi kuibuka na tuzo ya kocha bora wa mwezi June anajiunga na timu hiyo ambayo msimu wa 2025/26 aliondoka dirisha dogo akisaidia kufika hadi nafasi ya nne kabla ya kutimka.