Amri Kiemba, Domayo waula Kagera Sugar
Muktasari:
- Mbali na maboresho ya benchi la ufundi, pia Kagera Sugar imefanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa kikosi hicho baada ya kufikia makubaliano ya kumteua Ofisa Mtendaji Mkuu mpya yaani (CEO), Mohamed Mkangala.
KATIKA kuendelea kuboresha benchi la ufundi la Kagera Sugar, uongozi wa timu hiyo umefikia makubaliano ya kuwachukua viungo waliowahi kutamba Simba, Yanga, Azam na Taifa Stars, Amri Kiemba na Frank Domayo kuwa wasaidizi wa Cedric Kaze.
Mbali na maboresho ya benchi la ufundi, pia Kagera Sugar imefanya mabadiliko ya uongozi wa juu wa kikosi hicho baada ya kufikia makubaliano ya kumteua Ofisa Mtendaji Mkuu mpya yaani (CEO), Mohamed Mkangala.
Mkangala aliyehudumu kama Mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu katika Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), amechukua nafasi ya Mkenya Ronald Okoth, ambaye kwa sasa amepangiwa majukumu mengine, akiwa ndiye meneja wa timu hiyo.
Okoth amepewa jukumu hilo akichukua nafasi ya Bernard Samson Sikira aliyeondoka tangu, Septemba 21, 2026, baada ya mabosi wa kikosi hicho kuvunja benchi lote la ufundi lililokuwa linaongozwa na Kocha Mkuu, Juma Kaseja.
Kaseja alikiongoza kikosi hicho kurejea Ligi Kuu Bara msimu wa 2025-2026, baada ya kushuka 2024-2025.
Kwa msimu wa 2026-2027, Kaseja aliiongoza Kagera Sugar katika mechi sita za Ligi Kuu bila ya ushindi baada ya kutoa sare mbili na kupoteza nne, huku kikosi hicho kikifunga mabao matano na kuruhusu 14, akikiacha nafasi ya 15 na pointi mbili kwenye msimamo.
Kiemba na Domayo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wachambuzi wa soka huku wakisomea ukocha, wanakwenda kumsaidia Kaze kukiweka sawa kikosi hicho ili kisirejee Ligi ya Championship.