Kagera Sugar yashusha vyuma vitatu benchi la ufundi
Muktasari:
- Kiemba na Domayo wanaungana na kocha mkuu Cédric Kaze aliyetambulishwa Septemba 21, 2026, akichukua mikoba ya Juma Kaseja.
KAGERA Sugar imeendelea kuimarisha benchi lake la ufundi baada ya leo Septemba 30, 2026 kumtambulisha Amri Kiemba kuwa kocha msaidizi namba moja wa timu hiyo, huku Frank Domayo akiwa kocha msaidizi namba mbili.
Kiemba na Domayo wanaungana na kocha mkuu Cédric Kaze aliyetambulishwa Septemba 21, 2026, akichukua mikoba ya Juma Kaseja.
Makocha hao wanaingia katika benchi hilo wakati Kagera Sugar ikiwa tayari imecheza michezo sita ya Ligi Kuu ya NBC msimu huu, ikiwa haijapata ushindi baada ya kupoteza michezo minne na kutoka sare mara mbili.
Matokeo hayo yameifanya Kagera Sugar kushika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi mbili.
Kiemba, mwenye leseni ya ukocha ya CAF B Diploma, anaingia Kagera Sugar akiwa na uzoefu mkubwa wa soka la Tanzania, baada ya kuwahi kucheza katika klabu mbalimbali zikiwemo Moro United, Simba, Yanga, Azam FC, Miembeni na Stand United, pamoja na timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Akiwa mchezaji, Kiemba alicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji na alijijengea jina kutokana na uwezo wake wa kutawala mchezo, kutoa pasi za usahihi na kutengeneza nafasi za mabao.
Mbali na shughuli za ukocha, Kiemba amekuwa akifanya kazi ya uchambuzi wa soka kupitia Azam Media.
Kwa upande wa Domayo, ni kiungo aliyewahi kuzitumikia klabu za JKT Ruvu Stars, Yanga, Azam FC na Namungo, pia akicheza Taifa Stars, kabla ya kuingia katika jukumu lake jipya la ukocha.
Katika timu ya Taifa, Domayo alicheza mchezo wake wa kwanza wa Taifa Stars Mei 26, 2012, katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi, na baadaye akawa sehemu ya kikosi cha Tanzania kilichoshiriki fainali za AFCON 2019 nchini Misri.
Ujio wake Kagera Sugar unaongeza wataalamu wazawa wenye uzoefu wa soka la Tanzania katika benchi hilo, wakishirikiana na Kaze na Kiemba katika juhudi za kuirejesha timu hiyo kwenye ushindani wa Ligi Kuu.
Wakati huo huo, Kagera Sugar imemtambulisha Kefa Mabala kuwa mchambuzi wa video wa timu hiyo, hatua nyingine katika maboresho ya benchi la ufundi.
“Tunayo furaha kumtambulisha Kefa Mabala, Mchambuzi wa Video. Karibu kwenye familia ya Kagera Sugar,” imesema taarifa ya klabu hiyo.
Mabala atakuwa na jukumu la kusaidia benchi la ufundi katika uchambuzi wa michezo, mwenendo wa wachezaji pamoja na kutengeneza taarifa za kiufundi zitakazosaidia maandalizi ya timu kabla na baada ya michezo.
Mabadiliko hayo ya benchi la ufundi yanakuja katika kipindi ambacho Kagera Sugar inatafuta kubadili mwenendo wake baada ya kuanza vibaya msimu wa 2026-2027 wa Ligi Kuu ya NBC.