Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Steven Mapunda: Alia Tambwe kuwa Mfungaji Bora

Muktasari:

  • Kati ya vituko vya nguri huyo uwanjani ni pamoja na tabia aliyokuwa nayo ya kuwapangua mabeki wote wa timu pinzani na kubaki na lango na asifunge bao na badala yake anawasubiri mabeki, kisha anawapiga chenga na kupachika bao wavuni.

JINA lake halisi ni Steven Mapunda, kiungo, winga na mshambuliaji wa nafasi zote za mbele wa timu ya Majimaji ya Songea, Simba na Taifa Stars ingawa mashabiki wa soka wa miaka ya mwanzoni ya 1990 walimpachika jina la ‘Garrincha’.

Wanazi wa soka wa Majimaji, walimpachika jina hilo ambalo pia lilikubaliwa na washabiki wa mchezo huo wa mikoa mingine, wakimfananisha na mshambuliaji hatari wa timu ya Taifa ya Brazil na Botafogo, Manuel Francisco dos Santos ‘Garrincha’.

Garrincha huyo wa Brazil wa miaka ya 1960 ambaye aliiwezesha Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1958 na 1962 kabla hajatundika daruga 1973, alifahamika na wengi kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kupiga chenga na kupachika mabao sanjari na vituko vingi, ndani na nje ya uwanja.

Kati ya vituko vya nguri huyo uwanjani ni pamoja na tabia aliyokuwa nayo ya kuwapangua mabeki wote wa timu pinzani na kubaki na lango na asifunge bao na badala yake anawasubiri mabeki, kisha anawapiga chenga na kupachika bao wavuni.

Nje ya uwanja, Garrincha huyo wa Brazil anatajwa kuwa ni mlevi, dereva mwendawazimu anapokuwa barabarani na pia akihusishwa na ajali zisizo na idadi na zingine zikiwa zimechukua uhai wa ndugu na jamaa zake ambao alipata kuwa nao katika gari wakati wa ajali.

Garrincha wa Stars na Majimaji alipachikwa jina hilo kutokana na uwezo uliofananishwa na mchezaji huyo uwanjani lakini akiwa tofauti na Mbrazili huyo wa Botafogo kwani Mapunda, hanywi wala havuti sigara na kikubwa zaidi alikuwa akifanya mazoezi yasiyo ya kawaida ili kujiweka katika kiwango kinachotakiwa.

Nyota huyo anasema hali hiyo ndiyo iliyomfanya akapata heshima wakati akisakata soka miaka ya 1990 huku akibadilishana kuongoza kwa ufungaji wa mabao katika Ligi Kuu kwa zaidi ya miaka mitano na Edibily Lunyamila wakati huo akiwa Yanga. Ni nini siri ya mafanikio hayo?

Misingi ya  soka

Siri kubwa ya mafanikio katika soka na hata ilivyotokea kwake binafsi anasema ni kuwa na nidhamu nje na ndani ya uwanja na kutambua kuwa soka ndio ilikuwa ajira yake.

“Hakuna kitu kikubwa kama nidhamu, kazi yako lazima uiheshimu,” anasema na kuongeza kuwa mchezaji ili awe na mafanikio uwanjani ni lazima atambue kuwa kile anachokifanya kina misingi na maadili yake ambayo lazima yafuatwe.

Anasema mchezaji lazima ajue kwa nini anacheza soka? Nini malengo yake? Na wapi anaenda katika ulimwengu wa soka hali ambayo anasema itamsaidia kuwa na maisha mazuri hata baada ya kutundika daruga na kikubwa Taifa litakuwa limenufaika naye na atakuwa na heshima mbele ya jamii tofauti na ilivyo sasa kwa wachezaji wengi wa soka nchini ambao ni ndoto kucheza katika viwango vyao kwa msimu zaidi ya mmoja.

“Ndio maana wachezaji wa kigeni ‘mapro’ wameliteka soka la Bongo na mbaya zaidi sasa ndio wanaoongoza kwa ufungaji wa mabao jambo ambalo ni aibu ya Taifa,” anasema na kuongeza kuwa matokeo ya mfumo wa aina hiyo ni kuwa klabu zinakuwa na wachezaji wazuri lakini si timu ya Taifa.

Suala la wachezaji wa Kibongo kushindwa kuwa na namba za kudumu katika klabu zao na hata timu ya Taifa anasema linatokana na kupuuzwa kwa misingi ya soka na kutokufuatwa kwa maadili ya mchezo wenyewe hivyo kuwafanya walio wengi kutokuwa na viwango vya kueleweka.

“Kocha anataka viwango, na wakati wetu kulikuwa na ushindani mkubwa wa vipaji na iwapo utatetereka kocha anakuita na kukueleza kasoro zako akitaka uzifanyie kazi na wakati mwingine anakueleza wazi kuwa kiwango chako kinashuka,” anasema Garrincha.

Anasema hali hiyo ilikuwa inawasukuma wao kipindi hicho kulazimika kufanya mazoezi ya ziada ili kujiweka katika kiwango kinachokubalika na mbaya zaidi kulikuwa na vipaji lukuki ambavyo vinasubiri utetereke na vingine vinajifua kila siku ili kujipandisha na kufika ulipo wewe.

Kutokana na hali hiyo unakuwa unajua nini ufanye ili ubaki katika kiwango chako au vinginevyo unajua wazi kuwa siku zako katika klabu zinahesabika na unakuwa huna wa kumlaumu, lakini kwa sasa wachezaji wetu wameshindwa kuleta tofauti ndio maana wageni wamejaa.

Anasema utakuta mchezaji analilia kusajiliwa Simba au Yanga lakini msimu ukimalizika wa ligi naye ameisha, kocha anatafuta mchezaji mwingine wa kujaza nafasi yake hali ambayo inatokana na walio wengi kushindwa kujua wanataka nini.

Garrincha, ambaye umbo lake na kile alichokuwa anafanya uwanjani havikuwa vinafanana, anasema kuwa na wachezaji hadi watano wa kigeni katika klabu ya Ligi Kuu Bara ni matusi na kejeli kubwa kwa wachezaji wenyewe na hata TFF na athari zake zinaonekana timu ya Taifa.

Nyota huyo wa zamani anasema kuwa ingawa kuna wachezaji wa kigeni wakati huo waliwahi kujitokeza lakini hata hivyo hawakung’aa hali ambayo haikutoa nafasi kwa wengine na anatoa mfano wa mchezaji, William Fuhnbullah kutoka Liberia.

“Fahnbullah alikuja nchini akacheza kama mchezaji wa kawaida na muziki alioukuta mwenyewe alikubali,” anasema na kuongeza kuwa sasa hali ni tofauti jambo ambalo kama litaachwa lilivyo ni wazi kuwa mafanikio timu ya Taifa yatabaki ndotoni na Watanzania watabaki kuwa wanyonge mbele ya timu za mataifa mengine.

Udhaifu TFF

Garrincha anasema ingawa shirikisho hilo linaongozwa na mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa lakini wengine ambao wapo katika kamati tofauti ni wababaishaji na si watu wa mpira hali ambayo inalifanya shirikisho na soka kwa ujumla wake kushindwa kupiga hatua za maana.

“Ukiacha Tenga katika nafasi ya urais, hebu niambie ni nani mwingine ambaye aliwahi kucheza soka? Hakuna, watu wapo pale kwa maslahi yao na ndio wamebaki maofisini kuandika andika tu, hawaendi viwanjani,” anasema.

Mshambualiji huyo nguri wa zamani anasema udhaifu wa TFF pia unaonekana wakati wa kuisimamia timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, mara nyingi timu imekuwa ikiachwa mikononi mwa kocha bila msaada wa watendaji wengine wa shirikisho hilo kubaki wamejifungia maofisini.

“Soka linahitaji watu wahangaikaji nje na ndani ya uwanja watakaopita huku na huko kuhakikisha mambo yanaenda sawa, soka lina mambo mengi na si uwanjani pekee,” anasema na kuongeza kuwa kwa wachezaji ukiacha mambo mengine lakini pia wanatakiwa kuandaliwa kisaikolojia.

Itaendelea Jumanne.

Mwandishi anapatikana katika 0767826468