Stars yachechemea Morocco
Muktasari:
- Stars iliuanza mchezo huo vizuri na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 39, baada ya Cyprian Kachwele kuifungia Tanzania bao la kuongoza akimalizia pasi ya Feisal Salum na kuwafanya vijana hao wa kocha Miguel Gamondi kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
TAIFA Stars imeshindwa kutunza bao la kuongoza baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Madagascar katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, uliopigwa leo, Jumanne kwenye Uwanja wa d'Honneur, Meknes nchini Morocco.
Stars iliuanza mchezo huo vizuri na juhudi zake zilizaa matunda dakika ya 39, baada ya Cyprian Kachwele kuifungia Tanzania bao la kuongoza akimalizia pasi ya Feisal Salum na kuwafanya vijana hao wa kocha Miguel Gamondi kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Baada ya mapumziko, Madagascar ilirejea ikiwa na sura tofauti, ikiongeza mashambulizi kwa lengo la kusawazisha. Presha hiyo ilizaa matunda dakika ya 50, Nicolas Fontaine alipofunga bao la kusawazisha.
Bao hilo liliufanya mchezo huo kuwa wazi zaidi huku kila upande ukitafuta nafasi ya kupata bao la ushindi.
Dakika ya 67, Gamondi alilazimika kufanya mabadiliko ya kwanza baada ya Miano van den Bos kuumia, nafasi yake ikachukuliwa na Haji Mnoga katika kuimarisha kikosi kilichokuwa kikikabiliwa na presha ya Madagascar.
Mabadiliko mengine mawili yakafuata dakika mbili baadaye, Kachwele alitolewa na kuingia Simon Msuva huku Feisal Salum naye akitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Charles M'Mombwa, katika jitihada za kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji.
Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuzaa matunda kwa Stars ambayo iliambulia pointi moja katika mchezo huo.
Stars ilianza kampeni yake ya kusaka tiketi ya AFCON 2027 kwa kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Guinea-Bissau katika mchezo wa kwanza uliochezwa nyumbani, hivyo sare ya Madagascar kuwa matokeo ya pili katika kundi hilo.
Kwa matokeo hayo, Stars inaendelea kushika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi moja, nyuma ya Guinea-Bissau na Nigeria ambazo zilikuwa na pointi tatu kila moja kabla ya kukutana.
Huku Tanzania ikiendelea kuwa na matumaini ya kufanya vizuri katika michezo iliyosalia ambayo ni sehemu ya maandalizi ya fainali hizo ambazo watakuwa wenyeji kwa kushirikiana kwa pamoja na Kenya na Uganda.