Stars: Rekodi zipo ili zivunjwe
LICHA ya rekodi baina ya timu ya taifa Tanzania (Taifa Stars) na Algeria kuwabeba waarabu bado timu hiyo ina nafasi ya kupindua meza leo Juni 8, saa 1:00 usiku katika mchezo wa pili hatua ya makundi.
Mechi hiyo ni kufuzu kombe la mataifa Afrika (AFCON), 2023. itapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa huku Stars wakiingia na kumbukumbu nzuri ya kutoka sare ya bao 1-1, kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Niger.
Wapinzani wa Stars (Algeria) wameanza vizuri safari hii ya kufuzu baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya timu ya taifa ya Uganda.
Mara ya mwisho Stars ilikutana na Algeria ilikuwa 2019, katika hatua ya makundi kombe la mataifa Afrika lililofanyika Misri na Stars ilifungwa mabao 3-0, mchezo wa mwisho hatua ya makundi.
Stars wanatakiwa kuingia kwa nidhamu kubwa kwenye mchezo wa leo usiku haswa kuwaheshimu Algeria kuweka mipango mikakati sahihi ya kuhakikisha wanawazuia kisha yale mapungufu yao kwenda kuyatumia na kushambulia.
Kama Stars watataka kucheza kwa kuajiachia na kuacha kuwaheshimu Algeria kisa wapo nyumbani wanaweza kupoteza mechi hiyo mapema kwani ukweli usiyo pingika Algeria ni taifa kubwa lenye maendeleo katika soka timu yao ya taifa, klabu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja.
Katika kuhakikisha hilo walitwaa ubingwa wa mataifa Afrika 2019, wamekuwa na mafanikio mengi kama timu ya taifa, klabu zao na mchezaji mmoja mmoja kimsingi wanahitajika kuheshimika.
Katika mchezo wa leo Stars inaweza kupata ahueni kutokana na Algeria kumkosa mchezaji wao nyota mwenye mafanikio kwa hivi karibuni, Riyad Mahrez.
REKODI ZA HIVI KARIBUNI
Ukiachana na mechi hiyo ya kwenye hatua ya makundi Afcon, hivi karibuni Stars walicheza mechi ya kirafiki na Algeria Machi 22, 2018 na kukubali kufungwa mabao 4-1.
Kabla ya hapo Novemba 17, 2015 walicheza mechi ya mzunguko wa pili kufuzu kombe la dunia nchi Algeria na Stars walikubali kufungwa kwa kipigo kikubwa cha mabao 7-0.
Mechi ya mzunguko wa kwanza kufuzu kombe la dunia ilichezwa Novemba 14, 2015 Stars wakiwa Uwanja wa Benjamin Mkapa licha ya kutangulia mabao mawili dakika tisini zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
UBASHIRI WA KIKOSI
Stars (4-3-3), Aishi Manula, Kibwana Shomary, Bakari Nondo, Dickson Job, Mohammed Hussein, Mzamiru Yassin, Novatus Dismas, Feisal Salum, Saimon Msuva, George Mpole na Mbwana Samatta.
Algeria (4-3-3), Rais M'Bolhi, Aissa Mandi, Ahmed Touba, Ramy Bensebaini, Houcine Benayada, Ismaël Bennacer, Hisham Boudaoui, Ramiz Zerrouki, Yacine Brahimi, Islam Slimani na Youcef Belailli.