SMG: Yanga Princess inarudi
Muktasari:
- Kauli ya kocha huyo inakuja baada ya Yanga Princess kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-1 dhidi ya Kilimanjaro Wonders, Novemba 17, kwenye Uwanja wa KMC. Ushindi huo umekuwa muhimu kwa kikosi hicho katika kurejesha hali ya kujiamini baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens.
KOCHA wa Yanga Princess, Said Maulid ‘SMG’ amesema anafurahishwa na maendeleo ya kikosi chake, akieleza kuwa wachezaji wameanza kuzoeana na kuelewana vizuri uwanjani, jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Kauli ya kocha huyo inakuja baada ya Yanga Princess kuibuka na ushindi mnono wa mabao 7-1 dhidi ya Kilimanjaro Wonders, Novemba 17, kwenye Uwanja wa KMC. Ushindi huo umekuwa muhimu kwa kikosi hicho katika kurejesha hali ya kujiamini baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya JKT Queens.
SMG amesema anaona mabadiliko katika namna wachezaji wake wanavyoshirikiana uwanjani, akiamini kadiri muda unavyokwenda, kikosi hicho kitaendelea kuimarika na kuwa na ushindani zaidi.
Ameongeza kuwa ushindi huo umeongeza kujiamini kwa wachezaji, hasa wanapopata nafasi za kufunga, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza umakini na utulivu wanapokuwa mbele ya lango la wapinzani ili kuwa na safu imara zaidi ya ushambuliaji.
"Kujiamini kwa wachezaji kumeongezeka kwa kiwango kikubwa, na jambo hili litawasaidia kuwa watulivu zaidi wanapopata nafasi za wazi katika michezo ijayo ya ligi," amesema SMG.
Amesema kupoteza mchezo mwingine wa nyumbani baada ya matokeo mabaya waliyokuwa wameyapata kungekuwa pigo kubwa kisaikolojia kwa wachezaji, hivyo ushindi dhidi ya Kilimanjaro Wonders umekuwa muhimu katika kurejesha morali na kujiamini ndani ya kikosi.
Katika mechi nne ilizocheza msimu huu, Yanga Princess imeshinda tatu na kupoteza moja, ikiwa imefunga mabao 12 na kuruhusu mawili pekee.