SMG aibua mapungufu Yanga Princess
Muktasari:
- Kauli ya SMG inakuja wakati Yanga Princess ikiwa imeanza vizuri msimu huu, baada ya kuifunga Geita Queens mabao 2-0 na Bunda Girls mabao 3-0, kabla ya kukutana na JKT Queens na kupoteza kwa bao 1-0.
Kocha wa Yanga Princess, Said Maulid ‘SMG’, amesema licha ya kikosi chake kuonyesha ubora na mabadiliko ya kiuchezaji, bado kuna mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi haraka, akitaja eneo la makipa kuwa miongoni mwa maeneo yenye changamoto.
SMG amesema baadhi ya wachezaji waliojiunga na timu hiyo wakitokea katika klabu ndogo bado hawajazoea presha ya kucheza katika timu kubwa kama Yanga, hivyo benchi la ufundi linaendelea kuwajenga ili waweze kukabiliana na matarajio yaliyopo ndani ya klabu hiyo.
“Tumeona wachezaji wengi wametoka kwenye timu ndogo, ile presha ya kucheza timu kubwa bado hawajaizoea, hivyo tunajaribu kuwatengeneza waendane na presha ya Yanga,” amesema SMG.
Kocha huyo alieleza kuwa changamoto hiyo imeonekana zaidi katika eneo la makipa, ambao baadhi yao bado wanahitaji kuzoea mazingira ya ushindani na matarajio ya klabu hiyo.
Alitaja pia mawasiliano kati ya kipa na mabeki wake kuwa eneo jingine linalohitaji kuboreshwa, akisisitiza umuhimu wa mlinda mlango kuwa na sauti na kutoa maelekezo kwa wachezaji wanaomzunguka ili kuhakikisha safu ya ulinzi inacheza kwa mpangilio.
“Changamoto iliyopo kwa golikipa ni kuwa anakuwa kimya, hazungumzi na mabeki wake. Hiyo ni sehemu ya changamoto. Mpira huwezi kuwa mkamilifu, tutazungumza naye awe na sauti ili aweze kuwapanga mabeki wake,” amesema.
Kauli ya SMG inakuja wakati Yanga Princess ikiwa imeanza vizuri msimu huu, baada ya kuifunga Geita Queens mabao 2-0 na Bunda Girls mabao 3-0, kabla ya kukutana na JKT Queens na kupoteza kwa bao 1-0.