Nyota Simba asubiri dili Ulaya
Muktasari:
- Akizungumza baada ya kurejea nchini, Msimu alisema anaishukuru Simba kwa kumpa nafasi ya kwenda kuonyesha kipaji chake nje ya mipaka ya nchi, jambo ambalo limemuongezea motisha ya kuzidi kupambana, licha ya ushindani uliopo kikosini humo.
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Bakari Msimu amerejea nchini Tanzania baada ya kuhitimisha wiki moja tangu alipoondoka na kwenda kufanya majaribio katika Klabu ya SKN St. Polten, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Austria (Austrian 2. Liga).
Akizungumza baada ya kurejea nchini, Msimu alisema anaishukuru Simba kwa kumpa nafasi ya kwenda kuonyesha kipaji chake nje ya mipaka ya nchi, jambo ambalo limemuongezea motisha ya kuzidi kupambana, licha ya ushindani uliopo kikosini humo.
“Tulikuwa wachezaji 10, kutoka mataifa mbalimbali tulioenda kufanya majaribio na Tanzania nilikuwa mchezaji peke yangu, nashukuru nilionyesha kipaji changu na kwa sasa nasubiria majibu kutoka kwao ndio maana nimerudi nchini,” alisema Msimu.
Wakati Msimu akizungumza hayo, ila mmoja wa kiongozi wa Simba aliliambia Mwanaspoti mchezaji huyo atarudi Austria katika dirisha dogo la Januari 2027, ili kujiunga na timu hiyo, ikiwa kila kitu kitaenda vizuri, kwa maana ya ishu ya maslahi.
Kiungo huyo aliyejiunga na Simba Julai 21, 2026, akitokea Coastal Union, ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza kutokana na ushindani wa nyota wenzake, wakiwemo, Libasse Gueye, Elie Mpanzu na Alain Anicet Oura wanaoonyesha kiwango kizuri.
Kwa msimu wa 2025-2026, nyota huyo alionyesha kiwango kizuri na kuchangia mabao matano ya Ligi Kuu Bara kati ya 31, ya kikosi kizima cha Coastal Union ya jijini Tanga, baada ya kufunga matatu na kuasisti mawili na kuivutia Simba kumsajili.
Msimu aliandika rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi msimu wa 2025-2026, katika Ligi Kuu Bara akiwa na Coastal Union, ilipoichapa Tanzania Prisons mabao 4-1, katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, Februari 10, 2026. Katika mechi hiyo iliyokuwa kali na ya kuvutia, Msimu alifunga bao la mapema zaidi lililochukua sekunde ya 58, ikiwa ni rekodi ya Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, wakati kikosi hicho cha Coastal kilipoifunga Prisons ugenini mabao 4-1.