Sita zimewarudisha Mashujaa darasani
Muktasari:
- Mashujaa itakuwa na mechi dhidi ya Azam FC utakaochezwa Oktoba 24, 2026 kabla ya kukutana na Yanga Oktoba 27, 2026.
KIPIGO cha mabao 6-1 kutoka kwa Simba kimekuwa pigo kubwa kwa Mashujaa, lakini kocha wa timu hiyo, Amani Josiah, amesema amechukua hatua za haraka kurejesha hali ya wachezaji wake kwa kufanya vikao vya ndani pamoja na mafunzo ya darasani na uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah amesema baada ya kipigo hicho, aliona umuhimu wa kuzungumza na wachezaji wake ili kuwaondolea maumivu ya kisaikolojia na kuwafanya warejee katika hali ya kawaida, badala ya kuendelea kubeba matokeo hayo katika michezo inayofuata, hivyo kuanza kuwafundisha darasani.
Amesema vikao hivyo vimemsaidia kuwakumbusha wachezaji wajibu wao na namna wanavyopaswa kukabiliana na matokeo mabaya, akisisitiza kuwa kipigo walichokipata hakipaswi kuwa kielelezo cha kiwango chao katika mechi zote za msimu.
“Nimezungumza na wachezaji wangu na tumefanya vikao vya ndani, mafunzo ya darasani pamoja na yale ya uwanjani. Tulihitaji kukaa pamoja, kuangalia tulipokosea na namna ya kurekebisha makosa yetu ili hali kama hiyo isijirudie,” amesema Josiah ambaye picha ilisambaa mitandaoni akiwafundisha wachezaji wake kwa kutumia ubao.
Ameongeza kuwa amewataka wachezaji wake kusahau kipigo walichopata kutoka kwa Simba na kuelekeza nguvu zao katika kurekebisha makosa yaliyojitokeza, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarika kisaikolojia na kurejea uwanjani wakiwa na ujasiri.
Amesema licha ya changamoto kubwa waliyoipata wanapaswa kuhakikisha hawarudii makosa hayo hasa katika safu ya ulinzi. Katika michezo minane ambayo Mashujaa imecheza imeshinda mara nne na vipigo vinne ikiwa imefunga mabao tisa na kuruhusu 13, huku ikikusanya pointi 12.
Mashujaa itakuwa na mechi dhidi ya Azam FC utakaochezwa Oktoba 24, 2026 kabla ya kukutana na Yanga Oktoba 27, 2026.