Bwenzi: Simba, Yanga namba ipo
Muktasari:
- Bwenzi ambaye anacheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu sasa amekuwa mmoja wa wachezaji wanaong’ara pindi anapokutana na timu kubwa akifunga mabao bora yanayoacha mshangao kwa wadau na mashabiki wa soka nchini.
"BADO kuzitumikia." Hiyo ni kauli ya nyota wa Mashujaa FC, Selemani Bwenzi akielezea furaha ya kuzifunga Simba na Yanga mabao ya kideoni, na safari yake ya kuzichezea timu hizo kubwa na kongwe nchini.
Bwenzi ambaye anacheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa tatu sasa amekuwa mmoja wa wachezaji wanaong’ara pindi anapokutana na timu kubwa akifunga mabao bora yanayoacha mshangao kwa wadau na mashabiki wa soka nchini.
Kama haitoshi, licha ya kufanya vizuri, mchezaji huyo mzaliwa wa Tandale jijini Dar es Salaam amekuwa katika sintofahamu ya kukutana na aibu ya vipigo vizito katika timu anazozichezea dhidi ya vigogo hao jambo analodai humchanganya sana akili.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Bwenzi anaeleza siri ya kuwafunga makipa Djigui Diarra wa Yanga na Mahamadou Kassali wa Simba, huku akieleza kwa uwezo alionao anaweza kukipiga kwa vigogo wa Kariakoo na akaonyesha vitu vya maana zaidi uwanjani.
SIMBA, YANGA NAMBA IPO
Kama ilivyo kawaida kwa wachezaji wote nchini kutamani kuvaa uzi wa Wekundu au Jangwani, Bwenzi naye ni moja ya ndoto na malengo yake kutamani kucheza moja ya timu hizo kubwa.
Anaeleza kuwa licha ya kutoka familia ya wapenda soka nchini, lakini hakuna aliyefikia kiwango cha kucheza mpira wa ushindani, hivyo anatamani kufanya makubwa hadi kucheza soka nje ya nchi.
“Nyumbani Baba na Kaka walicheza japokuwa si kwa kiwango cha juu, hakuna aliyefika huku hivyo natamani nivuke mipaka, pale Simba na Yanga nikipata nafasi namba ni uhakika.
“Kimsingi ni kuendelea kulinda kiwango hiki ikiwa ni kula na kulala vizuri, kuachana na sterehe zisizo na faida, kutobweteka na kumtanguliza Mungu kila hatua ili kufikia ndoto hizi,” anasema.
YAO AMLIZA
Kiungo huyo mwenye uwezo wa kucheza pia winga, anasema kwa muda aliocheza Ligi Kuu Bara hawezi kumsahau beki wa Yanga, Yao Kouassi kwa kazi ngumu anayompa kila wanapokutana uwanjani.
Anaeleza kuwa amekutana na mabeki wengi wenye uwezo, akili ya mpira na ushindani lakini kila anapokutana na Yanga na kuona jina Yao, huwa mapigo ya moyo yanamuenda kasi. “Kila nikikutana naye najua moto utawaka. Jamaa anajua sana na sijawahi kupata wepesi au urahisi uwanjani. Mabeki ni wengi bora, ila kwa yule jamaa ni noma sana,” anasema.
SIRI YA MABAO YAKE
Bwenzi akiwa katika kikosi cha Ken Gold misimu miwili iliyopita, licha ya timu yake kutokuwa na matokeo mazuri, lakini nyota huyo alionesha kiwango bora kilichowakuna wengi uwanjani.
Akiitumikia timu hiyo iliyoshuka daraja msimu huo wa 2024/25, Bwenzi alifunga bao bora na la kideoni akipiga mpira kuanzia katikati ya uwanja na kumtungua Diara ambaye alijaribu kuruka bila mafanikio.
Katika mchezo huo uliopigwa Februari 2, 2025 katika uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam, Ken Gold ilikubali kulala kipigo cha mabao 6-1 huku bao la Bwenzi likitosha kuwafariji vijana hao wa wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Kama haitoshi, nyota huyo alifanya maajabu tena juzi wakati Mashujaa ikiloa kipondo cha mabao 6-1 dhidi ya Simba, huku bao la kideoni likifungwa na mchezaji huyo aliyepiga shuti nje ya hatari na kumtungua Kasali wa Simba.
Akielezea siri ya mabao hayo, Bwenzi anasema kazi yake ni mpira na anafanya hivyo kuonesha uwezo na ubora wake kwa muda anaopewa nafasi ya kucheza uwanjani kwakuwa vita ya namba ni kubwa kikosini.
Hata hivyo anaeleza kuwa kila kitu kinatokea kwa wakati pale Mungu anapoamua kumpandisha mtu, akieleza kuwa bado anayo safari ndefu kufikia malengo licha ya kwamba anashukuru kwa kile anachofanya.
“Kupata nafasi kwenye timu yenye mastaa wengi si kazi ndogo, ndio maana ninapokuwa benchi silaumu ila napopata nafasi natumia muda huo kufanya kitu cha tofauti, nashukuru Mungu kunibeba," anasema Bwenzi.
“Nikiwa nje ya uwanja huwa nasoma mchezo siangalii video ya mtu bali naanzia mazoezini halafu nakuja kufanya uwanjani kwenye mechi, nashukuru yote haya ni ushirikiano na kuaminiwa na kocha.”
KUZIFUNGUA SIMBA, YANGA
Nyota huyo asiye na mambo mengi uwanjani, anaeleza kuwa kila mchezaji haswa timu za kawaida hutamani kuzifunga Simba na Yanga kwakuwa ndizo kubwa kwa hapa nchini.
Anasema hatua ya kuwafunga makipa wakubwa, Diarra na Kassali ni mafanikio makubwa kwake na si kuwafunga tu, bali kuwatesa kwa mabao bora ambayo kwa kiasi kikubwa yanampa nguvu kufanya kazi.
“Ni furaha kubwa kuzifunga hizi timu na mabao mazuri ambayo yanawatesa makipa wao, kila mchezaji anatamani kuzifunga hizo timu kubwa hapa nchini, hii ni mafanikio makubwa kwangu,” anasema.
ALIA NA VIPIGO
Bwenzi anasema licha ya kiwango bora anachoonesha pale anapokutana na timu kubwa za Yanga na Simba, lakini imekuwa ni maumivu sana kwake kukumbana na vichapo vizito.
Anasema akiwa Ken Gold msimu wa 2024/25 akicheza kwa ubora na kufunga bao zuri dhidi ya Diara, lakini walikufa kipondo cha mabao 6-1 lakini kama haitoshi dhidi ya Simba akiichezea Mashujaa wakala kichapo kama hicho.
“Kwakweli sielewi ni kitu kinanichanganya sana akili, tunapambana na ninajitoa kadri niwezavyo kuipambania timu lakini najikuta tunafungwa idadi kubwa ya mabao, mtu mwingine anaweza kuchukulia kawaida.
“Yaani baada ya mechi nakaa pembeni najiuliza inakuaje, mabao sita si machache, lakini nashukuru nachukulia kama sehemu ya mchezo na matokeo ya mpira najipanga na mechi inayofuata” anasema mchezaji huyo.
MASHUJAA YA KIMATAIFA
Kiraka huyo anasema moja ya msimu bora kwa Mashujaa ni huu kutokana na mwanzo mzuri walionao, muunganiko, mipango na malengo ya jumla kuanzia uongozi, benchi hadi wachezaji.
Anafichua kuwa kabla ya kuanza msimu, walikaa vikao kadhaa na kupeana mipango ya ligi msimu huu na kwamba kinachofanyika si bahati mbaya bali ni utekelezaji wa mikakati.
“Moja ya msimu bora ni huu wa 2026/27, timu imeimarika na imeunganika, hiki kinachofanyika ni utekelezaji tu na matarajio yetu ni kuona tunamaliza nafasi nne za juu na kucheza kimataifa mwakani,” anasema.
ALIKOANZIA KUKIWASHA
Nyota huyo alianza soka muda mrefu akicheza zaidi ‘ndondo’ huko Dar es Salaam kabla ya Namungo kumuita na kumpiga benchi msimu mzima, ambapo baadaye Ken Gold walimvuta na kumpaisha Ligi Kuu.
Hata hivyo licha ya kuwa na kiwango bora, alijikuta akishuka na timu hiyo japokuwa Mashujaa waligundua uwezo wake na kumvuta kikosini ambapo ndipo anakiwasha kwa sasa.
“Kitu ambacho siwezi kusahau ni kuwekwa benchi msimu mzima pale Namungo, lakini nashukuru nilijifunza vingi na nilipotua Ken Gold wakaniamini kunipa namba na sasa nilipo maisha ni tofauti riziki inapatikana,” anasema mchezaji huyo.