Sintofahamu Yanga Princess ikicheza bila ya Edna Lema
Muktasari:
- Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimeithibitishia Mwanaspoti kuwa, kocha huyo mwenye uzoefu kwenye soka la wanawake tayari ameshawaaga wachezaji wake na kuondoka kambini, kufuatia kipigo kizito cha mabao 3-0 walichokipata Septemba 30 kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba Queens, kwenye mchezo wa nusu fainali.
MAMBO yameharibika! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kocha Mkuu wa Yanga Princess, Edna Lema, kubwaga manyanga ghafla na kuacha benchi la ufundi la timu hiyo katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wa Ngao ya Jamii unaoendelea leo hii Uwanja wa KMC Complex.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimeithibitishia Mwanaspoti kuwa, kocha huyo mwenye uzoefu kwenye soka la wanawake tayari ameshawaaga wachezaji wake na kuondoka kambini, kufuatia kipigo kizito cha mabao 3-0 walichokipata Septemba 30 kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba Queens, kwenye mchezo wa nusu fainali.
Habari zinasema kuwa, pamoja na matokeo hayo mabovu dhidi ya Simba Queens, sababu kubwa iliyomsukuma Edna kuamua kuachia ngazi ni mgogoro na kutoelewana kwa baadhi ya viongozi wa juu wa timu hiyo.
"Edna hayupo benchi leo kwa sababu tayari ameshawaaga mabinti na kuondoka. Matokeo ya kufungwa na Simba yamechangia, lakini ukweli ni kwamba kulikuwa na mgogoro mkubwa kati yake na viongozi. Mambo hayakuwa sawa kabisa klabuni," kilieleza chanzo hicho.
Viongozi wanaamini kocha huyo hana uwezo wa kushindana na vigogo wengine kwenye soka la wanawake kama Simba Queens na JKT Queens ambao wametawala ligi hiyo kwa miaka mingi.
Lakini kwa kocha huyo alikuwa na msimamo na kuamini kuwa sababu ya timu kutofanya vizuri yeye hausiki bali inachangiwa na uongozi wa timu ambao hawako siriazi na timu hiyo.
Mwanaspoti lilipojaribu kumtafuta Kocha Edna pamoja na viongozi wa Yanga Princess ili kuzungumzia uamuzi huo wa ghafla, jitihada hazikuzaa matunda baada ya simu zao za mkononi kuita bila kupokelewa.
Mpasuko huo unakuja wakati Yanga Princess ikipambana kujenga kikosi cha ushindani msimu huu, huku kuondoka kwa Edna kukiacha maswali mengi juu ya hatima ya benchi la ufundi la Wananchi hao.