Amani Josiah anachofanya ni sahihi
Muktasari:
- Kwa wanamichezo, nidhamu inahitajika sana kwani ndiyo inayoleta ufanisi na matokeo mazuri uwanjani na kinyume na hapo, timu au mwanamichezo husika atafanya vibaya tu na hivyo kufanya malengo yasitimie.
NIDHAMU ndiyo kitu cha msingi katika maisha ya binadamu na inapokosekana inaweza kukwamisha mambo mengi.
Kwa wanamichezo, nidhamu inahitajika sana kwani ndiyo inayoleta ufanisi na matokeo mazuri uwanjani na kinyume na hapo, timu au mwanamichezo husika atafanya vibaya tu na hivyo kufanya malengo yasitimie.
Sasa hapa kijiweni tumesikia huko Mashujaa FC, kocha Amani Josiah ameanza kuwanyoosha wachezaji watovu wa nidhamu kwa kuwapa adhabu mbalimbali kulingana na uzito wa makosa yao.
Kuna ambao amewapa adhabu ya kufanya mazoezi binafsi na kuna wengine kawaondoa katika mipango yake kwa kipindi fulani baada ya kufanya utovu wa nidhamu kwenye timu.
Hili ni jambo jema sana na kijiwe kinampa pongezi nyingi Kocha Amani Josiah na benchi lake la ufundi kwa kuchukua hatua za kuwashughulikia wachezaji watovu wa nidhamu katika kikosi cha Mashujaa FC.
Itafanya wachezaji wasiichukulie poa Mashujaa na wakawa wanajiamulia wanavyotaka wao bali watambue wapo chini ya timu iliyo ndani ya taasisi ya ulinzi na usalama ambayo msingi wake mkubwa ni nidhamu.
Kingine itajenga heshima kwa makocha wazawa ambao wamekuwa wakichukuliwa poa sana na wachezaji wetu raia wa hapa nyumbani kwa vile tu wanaishi nao mitaani na wanaongea lugha inayofanana huku wakikutana katika vijiwe mbalimbali.
Na wachezaji wetu wa Kitanzania nao wanapaswa kujitafakari bhana wakati mwingine na kubadilika kwa kuachana na mambo ya kijinga na kisela kama hayo ya utovu wa nidhamu.
Hayawasaidii chochote zaidi ya kuwaharibia tu ndoto zao katika soka ingawa wenyewe hawajifunzi na kuendelea kurudia rudia.