Simba, Yanga kuishusha Mwadui
ZIMEBAKI mechi chache mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara umalizike ambapo Mwadui FC inayocheza leo Ijumaa Desemba 18 dhidi ya Polisi Tanzania ipo katika hali mbaya na hatma ya kubaki ipo mikokoni mwa timu tatu kubwa.
Mwadui imecheza mechi 15 imekusanya pointi 10 baada ya kushinda mechi tatu, sare moja na kupoteza michezo 10 hivyo inaning'inia mkiani.
Uongozi wa Mwadui FC umefanya uchaguzi wao na kuelezea kuwa mechi ambazo zinawaweka kwenye wakati mgumu ni tatu za mzunguko wa pili wa ligi dhidi ya Simba, Azam na Yanga.
Mwenyekiti wa klabu hiyo Noordin Seleman amezungumza na Mwanaspoti Online leo Ijumaa Desemba 18, 2020 kutoka Kishapu mkoani Shinyanga kuwa baada ya mabadiliko yaliyofanywa jana Alhamis uongozi utaanza na kazi moja kuhakikisha timu inabaki kwenye ligi.
"Ili tuwe salama na kuwemo kwenye ligi msimu ujao ni lazima tukusanye pointi 35 lakini tuna mtihani mzito wa kupata pointi tisa kutoka kwenye timu tatu zinazogombania ubingwa za Azam, Simba na Yanga.
"Kiukweli mechi hizo ni ngumu sana kwetu, Azam na Simba tutacheza nao nyumba lakini Yanga tutawafuata, ni kazi ngumu ila tutapambana kupata ushindi maana kila timu ambao tupo kwenye hatari tunapambana kujinasua," amesemaSeleman
Kuhusu usajili, alisema kuwa wiki ijayo Jumatatu Desemba 21, 2020 wataanza usajili rasmi kuboresha kikosi chao ili kiwe na ushindani mkubwa mzunguko ujao.
"Tungeanza wiki hii lakini tunasubiri mechi ipite ila Jumatatu tutaanza rasmi, lazima kikosi kiboreshwe ili kutimiza malengo yetu, kocha anakuja keshokutwa Jumapili lakini si kwa ajili ya kusaini mkataba ataangalia kwanza kikosi kama ataweza kukibeba," amesema