Prime
Simba yamshusha mrithi wa Neo Maema
SIMBA imeanza kutekeleza mpango mbadala wa kuimarisha safu yake ya kiungo baada ya mazungumzo ya kumrejesha nchini kiungo wa Afrika Kusini, Neo Maema kushindwa kuzaa matunda huku Mothusi Cooper raia wa Botswana akipewa nafasi na Kocha Steve Barker katika michuano ya Kagame huko Kigali, Rwanda.
Hatua hiyo inaonyesha namna viongozi wa Simba walivyokuwa wamejiandaa kwa mazingira yoyote katika dirisha hili la usajili. Wakati Maema alikuwa chaguo la kwanza kwa benchi la ufundi kutokana na kuifahamu vizuri timu hiyo baada ya kuitumikia kwa mkopo msimu uliopita, klabu haikutaka kubaki na chaguo moja.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kuwa, mazungumzo kati ya Simba na Maema yalisimama katika hatua za mwisho baada ya kushindikana kufikiwa mwafaka kuhusu maslahi binafsi ya mchezaji pamoja na baadhi ya vipengele vya mkataba mpya.
Chanzo cha kuaminika ndani ya Simba kimesema kocha Barker alikuwa ameonyesha wazi kuwa angependa Maema aendelee kuwa sehemu ya kikosi kutokana na mchango aliouonyesha msimu uliopita, lakini uamuzi wa mwisho ulikwama mezani.
"Kocha alikuwa anamuhitaji kwa sababu anamfahamu vizuri na aliridhishwa na kiwango chake. Tatizo halikuwa upande wa benchi la ufundi, bali mazungumzo ya kimkataba hayakufikia makubaliano yaliyokuwa yanahitajika. Ndiyo maana klabu imeanza kuangalia njia nyingine mapema ili isipoteze muda," kilisema chanzo hicho.
Maema, ambaye kwa sasa yupo Afrika Kusini, inaelezwa anaendelea kusikiliza ofa kutoka kwa klabu mbalimbali huku Simba ikisubiri kuona kama kutakuwa na mabadiliko yoyote, ingawa kwa sasa uwezekano wa kurejea kwake unaonekana kupungua kadri siku zinavyosonga.
Ndani ya mazingira hayo ndipo jina la Cooper lilipoibuka. Kiungo huyo wa kimataifa wa Botswana mwenye umri wa miaka 29, amewasili Kigali ambako Simba imeweka kambi kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame iliyoanza Julai 24, 2026, akipewa nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi hicho ili benchi la ufundi limfanyie tathmini kabla ya uamuzi wa mwisho.
Cooper si mchezaji asiyejulikana katika ukanda wa kusini mwa Afrika. Amecheza katika klabu za Botswana ambazo ni Township Rollers, Jwaneng Galaxy, Gaborone United pamoja na MC Oujda ya Morocco huku pia akiwa mmoja wa wachezaji ambao wamekuwa wakicheza timu ya taifa ya Botswana.
Mmoja wa wachambuzi wa soka nchini Botswana, Kagiso Phatsimo ambaye amekuwa akifuatilia maendeleo ya Cooper kwa miaka kadhaa, amesema Simba inaweza kupata kiungo mwenye uwezo mkubwa wa kucheza katika mifumo tofauti endapo atafanikiwa kuwashawishi makocha.
"Cooper ana uzoefu mkubwa, anaweza kucheza kama kiungo wa kati, lakini pia anajua kuunganisha safu ya kiungo na ushambuliaji. Kama atapata muda wa kuzoea mazingira ya Tanzania, naamini ana uwezo wa kucheza kwenye kiwango kinachohitajika na Simba," amesema mdau huyo.
Tofauti na Maema ambaye tayari alikuwa amezoea mfumo wa Simba, Cooper atalazimika kwanza kuwathibitishia makocha kupitia mazoezi na mechi za majaribio kabla ya uongozi kufanya uamuzi wa kumpa mkataba.
Hata hivyo, hatua ya Simba kumleta Cooper haimaanishi moja kwa moja kuwa tayari amechukua nafasi ya Maema, bali ni ishara kwamba klabu haitaki kujikuta ikichelewa kupata mbadala iwapo mazungumzo na kiungo huyo wa Afrika Kusini yatafungwa rasmi.
Katika soka la kisasa, dirisha la usajili linahitaji maamuzi ya haraka. Klabu nyingi huandaa majina mawili au matatu kwa kila nafasi ili kuhakikisha mpango mmoja ukishindikana, mwingine unaanza kutekelezwa bila kupoteza muda.
Ndicho kinachoonekana kufanywa na Simba. Wakati mlango wa Maema ukiendelea kubaki wazi kwa kiwango kidogo, viongozi wa klabu hiyo tayari wameanza kuangalia kesho kwa kumpa Cooper nafasi ya kuonyesha kama anaweza kuwa jibu jipya katika safu ya kiungo ya Wekundu wa Msimbazi kuelekea msimu mpya.