Prime
Simba yakaribia kukamilisha usajili wa Ngoma
Muktasari:
- Habari za uhakika ambazo mwanaspoti imezipata ni kuwa kiungo huyo ambaye miezi mwili iliyopita alivunja mkataba wake na Al Hilal ya Sudan, alitua nchini jana alfajiri na kisha kupokelewa na baadhi ya maofisa wa Simba kisha kupelekwa katika mojawapo ya hoteli za kifahari iliyopo Posta Mpya, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Simba inakaribia kukamilisha usajili wa nyota wa Al Hilal ya Sudan, Fabrice Luamba Ngoma kwa ajili ya kuimarisha kikosi chake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano 2023/2024.
Habari za uhakika ambazo mwanaspoti imezipata ni kuwa kiungo huyo ambaye miezi mwili iliyopita alivunja mkataba wake na Al Hilal ya Sudan, alitua nchini jana alfajiri na kisha kupokelewa na baadhi ya maofisa wa Simba kisha kupelekwa katika mojawapo ya hoteli za kifahari iliyopo Posta Mpya, Dar es Salaam.
Mchana kiungo huyo alikutana na vigogo wa Simba katika ofisi ya kiongozi mmoja wa timu hiyo iliyopo katikati ya jiji, mazungumzo ambao hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, inaripotiwa yalikuwa yamefikia mahali pazuri tayari kwa kiungo huyo kuonekana katika jezi ya Simba msimu ujao.
"Dili la Ngoma limelazimika kufanyika harakaharaka kwa vile hadi anafika hapa alikuwa na ofa mezani ambazo kama tungechelewa ingekuwa ni vigumu kumpata. Ni mchezaji wa daraja la juu ambaye sidhani kama kuna timu ndani ya Afrika hii haitamani kuwa naye.
"Huu ni usajili ambao tunaamini utaongeza thamani katika kikosi chetu kama utakamilika kwani ana uzoefu wa mechi kubwa za mashindano ya kimataifa na ni kiongozi mzuri ndani na nje ya uwanja hivyo tunaamini ataongeza uimara katika idara yetu ya kiungo," alisema mmoja wa viongozi wa Simba.
Usajili wa Ngoma ukikamilika, utahitimisha kiu ya miaka minne ambayo Simba imekuwa nayo ya kumnasa kiungo huyo wa zamani wa AS Vita na Raja Casablanca mwenye umri wa miaka 29.
Mwaka 2019, Simba ilijaribu kumsajili Ngoma baada ya kukoshwa na kiwango alichoonyesha katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na AS Vita, lakini nyota huyo alitimkia Raja Casablanca ya Morocco.
Nguvu ya fedha ilionekana kuwazidi Simba mbele ya Raja Casablanca ambayo ilimnunua kiungo huyo kwa dau la takribani Euro 268,000 (Sh 706 milioni) ambalo ililipa kwa AS Vita ili iwaachie Ngoma aliyewahi kuchezea pia Mk Entacheite ya DR Congo na Ifeanyi Ubah ya Nigeria.
Baada ya kuitumikia Raja Casablanca kwa miaka mitatu, 2022, kiungo huyo alitemwa na kutimkia Al Fahaheel ya Kuwait akiwa mchezaji huru ambapo aliichezea kwa msimu mmoja na kutimkia Al Hilal iliyomnunua kwa dau linaloripotiwa kuwa Euro 400,000 (Sh 1.5 bilioni).
Hata hivyo machafuko ya kisiasa yaliyotokea huko Sudan miezi kadhaa iliyopita, yalichangia kumfanya mchezaji huyo na nyota wengine kadhaa kuvunja mikataba yao ya kuichezea timu hiyo iliyotwaa taji la Ligi Kuu nchini humo mara 29.
Usajili wa Ngoma unaonekana kulenga kuzipa pengo la nafasi ya kiungo wa ulinzi ndani ya kikosi cha Simba ambalo limetokana na kuonyeshwa mlango wa kwaheri kwa Erasto Nyoni, Jonas Mkude na Ismail Sawadogo.
Kusajiliwa kwa Ngoma mwenye uwezo pia wa kucheza nafasi ya beki wa kati na kiungo mshambuliaji, kunaonekna kumuongezea machaguo kocha wa Simba, Robertinho Oliveira katika nafasi ya kiungo wa ulinzi ambayo kwa sasa ana wachezaji wawili tu anaowategemea ambao ni Mzamiru Yassin na Sadio Kanoute.
Alipotafutwa kuthibitisha usajili wa mchezaji huyo, ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema muda ukifika mashabiki wa timu hiyo watafahamu kama ni kweli au sio kweli.
"Kwa sasa tumeshamaliza kuagana na wachezaji ambao hatutokuwa nao na kinachofuata ni kutangaza vyuma tulivyovisajili kwa ajili ya kuturudishia furaha msimu ujao.