Mossi atua rasmi MC Alger
Muktasari:
- Awali, Mwanaspoti ilifichua kuwa Mossi alikuwa katika hatua za mwisho za kujiunga na MC Alger baada ya mazungumzo kati ya klabu hizo kufikia pazuri huku zikisalia taratibu chache za kukamilisha dili hilo.
KAMA ilivyoripotiwa na Mwanaspoti siku chache zilizopita, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Mossi Nduwumwe, amekamilisha rasmi uhamisho wake kutoka Singida Black Stars kwenda kwa mabingwa wa Algeria, MC Alger.
Awali, Mwanaspoti ilifichua kuwa Mossi alikuwa katika hatua za mwisho za kujiunga na MC Alger baada ya mazungumzo kati ya klabu hizo kufikia pazuri huku zikisalia taratibu chache za kukamilisha dili hilo.
Sasa taarifa hizo zimethibitishwa rasmi baada ya MC Alger kumtambulisha nyota huyo kupitia kurasa zake rasmi za mitandao ya kijamii.
Klabu hiyo ilimkaribisha mshambuliaji huyo kwa ujumbe wa "Welcome to Mouloudia", ikithibitisha kumalizika kwa moja ya usajili uliokuwa ukifuatiliwa kwa karibu baada ya kiwango bora alichoonyesha akiwa Singida Black Stars msimu uliopita.
Mossi anaondoka Singida Black Stars akiwa amejijengea heshima ndani ya Ligi Kuu ya NBC ambapo licha ya kuichezea klabu hiyo kwa nusu msimu pekee baada ya kujiunga nayo mwezi Januari akitokea Flambeau du Centre FC ya Burundi, aliibuka mfungaji bora wa ligi kwa mabao 17.
Ndani ya kipindi hicho kifupi, mshambuliaji huyo aliweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga hat-trick mbili katika msimu wa 2025/26 huku mabao yake matatu dhidi ya Fountain Gate yakimhakikishia kutwaa tuzo ya mfungaji bora.
Uwezo huo ulimfanya kuvutia klabu mbalimbali kutoka nje ya Tanzania lakini MC Alger ndiyo imefanikiwa kupata saini yake huku ikijiandaa kutetea ubingwa wa Algeria na kushiriki mashindano ya CAF msimu ujao.
Kuondoka kwa Mossi pia kunathibitisha sababu ya kutokuwapo kwake kwenye kikosi cha Singida Black Stars kilichoweka kambi Kigali, Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya na michuano ya CECAFA Kagame, jambo ambalo Mwanaspoti pia ililiripoti wakati mazungumzo ya uhamisho yalipokuwa yanaendelea.