Simba mzigoni Ligi Kuu Bara
Muktasari:
- Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara kuanzia saa 10:00 jioni.
SIMBA inashuka dimbani leo Alhamisi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate unaotarajiwa kuwa mtihani mwingine kwa timu hiyo inayolenga kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo.
Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara kuanzia saa 10:00 jioni.
Wekundu wa Msimbazi wanaingia mchezoni wakiwa na kumbukumbu nzuri ya matokeo hivi karibuni ikiwamo ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Yanga, 6-1 dhidi ya Mashujaa na 6-1 dhidi ya 15 de Agosto katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya mchujo wa Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya marudiano kushinda 3-0.
Simba ina pointi 24 baada ya kucheza mechi nane za ligi ikishinda zaote, imefunga mabao 19 na kuruhusu manne.
Hata hivyo, mchezo wa leo hautakuwa rahisi kwa Simba ikizingatiwa kuwa Fountain Gate inahitaji matokeo mazuri ili kujiondoa katika eneo la chini la msimamo.
Fountain Gate inaingia kwenye mchezo ikiwa na pointi sita baada ya mechi nane, ikishinda mmoja, sare mbili na kupoteza mitano.
Kwa Fountain Gate ushindi dhidi ya Simba utakuwa matokeo mazuri katika jitihada za kubadilisha mwenendo wa msimu, ambapo inahitaji kutumia vizuri nafasi itakazopata na kuhakikisha haiipi Simba nafasi ya kucheza kwa uhuru katika eneo lake la ulinzi. Hii ni mechi ya kwanza Fountain kucheza Manyara ikitokea Arusha.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Steve Barker, amesema kuwa: “Tunajua mechi itakuwa ngumu kwa sababu mara ya mwisho matokeo yalikuwa sare ya bao 1-1 kwenye uwanja huo, hivyo tunakwenda kwa tahadhari kubwa ili tusipoteze alama.”
Kocha wa Fountain Gate, Fred Felix Minziro, amesema kuwa: “Timu yetu haina presha kwa sababu kila mtu anatarajia Simba ishinde, hivyo sisi tumejipanga vizuri kushangaza watu kwenye uwanja wa nyumbani na lengo letu ni kupata pointi tatu muhimu.”
PAMBA JIJI VS SINGIDA
Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Pamba Jiji inakutana na Singida Black Stars, huku wenyeji wakihitaji kuondoka katika eneo la chini la msimamo na wageni wakitaka kurejea kwenye ushindi wa ligi baada ya kukabiliwa na matokeo yasiyoridhisha katika baadhi ya michezo karibuni.
Pamba Jiji inaingia ikiwa na pointi sita baada ya mechi tisa, wakati Singida Black Stars ina pointi 11 baada ya kucheza mechi nane. Katika mechi tisa za ligi Pamba imeshinda moja, sare tatu na vipigo vitano, ikifunga mabao 10 na kuruhusu 15. Kwa upande wa Singida Black Stars inaingia mchezoni ikihitaji kupambana ili kupanda kwenye msimamo.
Singida ina mabao 14 ya kufunga na 11 ya kufungwa katika mechi nane za ligi, takwimu zinazoonyesha kuwa imekuwa na uwezo wa kupata mabao, lakini bado inahitaji kulinda matokeo yake.
Katika mechi zilizokutana Singida imekuwa na matokeo mazuri zaidi katika baadhi ya michezo yao ya hivi karibuni. Katika mchezo wa Mei 5, 2026, Singida iliifunga Pamba kwa mabao 3-1. Mchezo wa Novemba 8, 2025, ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwa Pamba, jambo la msingi litakuwa kuimarisha ulinzi na kutumia nafasi za kufunga itakazopata. Kwa Singida, changamoto itakuwa kuhakikisha inapata matokeo ya ligi bila kupoteza umakini baada ya majukumu yake ya kimataifa.
Kocha wa Pamba Jiji, Francis Baraza amesema kikosi chake hakijafanya vizuri katika mechi za nyumbani zilizopita, kikianza kwa sare kabla ya kupoteza dhidi ya Simba na TRA United, lakini anaamini matokeo yameanza kubadilika baada ya mchezo uliofuata. Amesema wanawaheshimu wapinzani wao kutokana na uzoefu wao wa mechi za kimataifa, lakini amewataka mashabiki kujitokeza kwa wingi kukipa nguvu kikosi hicho, akisisitiza kuwa ana imani na wachezaji wake kupata matokeo mazuri.
”Vijana wangu wana hali ya kujiamini wanapocheza nyumbani, hasa kwa sababu wameanza kushikana na mashabiki. Nina imani nao na ninachowaomba ni kujitahidi kupata mabao ya mapema na kuhakikisha tunazuia wapinzani wetu,” amesema.
Kocha Papy Kimoto wa Singida Black Stars, amesema: “Tunahitaji kuchukua pointi tatu ugenini ili kuendeleza hesabu zetu msimu huu.
“Tumetoka kucheza kimataifa, lakini haimaanishi tumechoka kwani timu inawachezaji wengi wakubwa, ingawa tutamkosa Jonathan Sowah kwa sababu ya kadi, ila tunakikosi kipana Hakuna kitakachokosekana.”
Muda huo wa saa 10:00 jioni, kuna mechi nyingine kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambapo TRA United itaikaribisha Geita Gold wakati Namungo ikiikaribisha Polisi Tanzania kuanzia saa 1:00 usiku.