Simba kwafukuta, Bodi ya Wadhamini ikiundwa kimyakimya
Muktasari:
- Katika Mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Bunju Arena, leo Jumapili, Agosti 2, 2026, Mangungu amewatangaza Salim Abdallah, Dk Bill Kiwia, Alhaj Ismail Mohamed, Amos Makalla, Adam Mgoyi, Hamad Abdallah na Hassan Hassanoo.
Wakati Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu akiunda Bodi mpya ya Wadhamini ya Klabu hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amesema uamuzi huo ni batili.
Katika Mkutano uliofanyika kwenye Uwanja wa Bunju Arena, leo Jumapili, Agosti 2, 2026, Mangungu amewatangaza Salim Abdallah, Dk Bill Kiwia, Alhaj Ismail Mohamed, Amos Makalla, Adam Mgoyi, Hamad Abdallah na Hassan Hassanoo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mangungu amesema kuwa uteuzi huo umezingatia katiba.
"Sasa hivi imetoa sharti lazima wawe saba na pungufu watano. Na katiba hiyohiyo ya Baraza la wadhamini pia imetoa sharti lazima wawe saba, pungufu watano. Na katiba hiyohiyo pia imetoa sharti kwa watu ambao wanastahili au wanafaa kuwa wajumbe wa baraza.
“Mojawapo lazima awe mwanachama, pili muadilifu na tatu watakaokuwa tayari kutumikia nafasi hiyo kwa niaba ya wanachama wote," amesema Mangungu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Crescentius Magori amesema kuwa mkutano huo uliotoa uamuzi huo ni batili.
“Tunapenda kuwataarifu Wanachama wote wa Simba kuwa hicho kilicho-fanyika Bunju siku ya leo siyo Kikao rasmi cha Mkutano maalum wa Simba. Hivyo maamuzi yote yaliyotangazwa huko ni batili na kinyume cha Katiba ya Simba.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Simba ya mwaka 2018 iliyofanyiwa marekebisho 2026, ibara ya 23, Mkutano Mkuu maalum utaandaliwa na Mwenyekiti wa Klabu kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi.
“Hivyo kesho tarehe 3/8/2026 kutakuwa na kikao cha Bodi kujadili agenda ya Mkutano Mkuu maalum wa Wanachama. Mtajulishwa siku maalum ya Mkutano huo,” imesema taarifa ya Simba.
Wakati hali ikiwa hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye ni mmoja wa waliouteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Udhamini ya Simba, Amos Makalla amekataa uteuzi huo akisema ni kinyume na katiba.
"Nimeona hii habari ya uteuzi kuwa mjumbe wa baraza la wadhamini laSimba. Mimi ni mwnachama wa klabu ya simba nafahamu vyema katiba ya Simba na mchakato wa kuwapata wajumbe wa baraza la wadhamini wa klabu ya Simba. Uteuzi huu ni batili, kwa sababu katiba ya Simba haikufuatwa na mimi binafsi sikushirikishwa," amesema Makalla.